Tuesday, 15 October 2013

HASLEY AWACHANA WAAMUZI EPL


Mark Hasley 
Kocha mstaafu, Mark Halsey amewachana baadhi ya waamuzi wa Ligi Kuu ya England (EPL), akisema wanaiharibu ligi na baadhi wanahitaji msaada.

Halsey (52) aliyestaafu mwishoni mwa msimu uliopita, anasema ni waamuzi wanane tu wanaoendelea na kazi wanaostahili kupuliza kipenga.
Waamuzi sita aliowataja kwamba hawakustahili kabisa kupewa kazi hiyo na wanatakiwa kuondoshwa au wapewe msaada wa haraka ni pamoja na Mike Jones na Jon Moss.
Wengie ni Kevin Friend, Lee Mason, Roger East na Neil Swarbrick. Friend amepata kulalamikiwa na wadau wengine kwa aina ya uchezeshaji na kutoa uamuzi usio wahaki.
Halsey anadai kwamba Jones ni mwamuzi mbaya kwa sababu anakosa ile haiba ya mamlaka wakati East haelekei kabisa kuwa kama refa wakati Friend ni yupo yupo tu.
Refarii huyu wa zamani anaamini kwamba wa kulaumiwa kwa kuvurunda waamuzi hao wa sasa ni taasisi inayosimamia waamuzi – Professional Game Match Officials Ltd (PGMOL).
Anadai kwamba taasisi hiyo inafanya waamuzi kuchezesha kama mchezo fulani wa kuigiza na kujenga mazingira ya woga na mateso.
“Hawawasaidii waamuzi dhaifu kuondokana na makosa yao na kupandisha viwango badala yake mfumo unajenga mazingira ya woga na kuwachanga waamuzi kwa maelekezo yanayowachanganya kutoka kwa viongozi tofauti,” anasema Halsey.
Anaamini kwamba waamuzi na wasaidizi wao wasiofaa huchaguliwa hata kusimamia mechi kubwa, jambo analosema ni aibu kubwa.
Hata hivyo, mwamuzi mwingine wa zamani,
Graham Poll amemandia mwenzake kwa kusema ameisaliti kazi iliyompa fedha nyingi katika maisha yake.
Halsey amekuja na orodha ya waamuzi na shutuma dhidi ya taasisi hiyo, siku chache baada ya kudai kwamba kocha wa zamani wa Manchester United, Alex Ferguson alikuwa akiwatumia waamuzi ujumbe kwenye simu kuhusu mechi walizokuwa wakisimamia, jambo lililopingwa vikali na Fergie.
Halsey ameingia mkataba na BT Sport kama mchambuzi wa soka, ambapo huwa kama jaji wakati mechi za EPL zikichezwa live.
Poll alikuwa na haya ya kusema dhidi ya Halsey: “Kwa asilimia 100 amesaliti kazi ambayo ilimlipa vizuri na asingepata maisha kama haya kutokana na kazi za awali ya umeneja bohari wala udereva teksi aliokuwa akifanya.
“Sisi kama waamuzi kwa kweli tumeshitushwa na kusikitishwa sana na hicho anachokifanya (Halsey).
“Hakujipa tafakari ya kutosha…anatakiwa ajitazame kwa kina mwenyewe lakini hatafanya hivyo, namjua, nimekuwa naye kwa miaka mingi, tabia yake ndiyo hiyo.”
Halsey anasema kiwango cha marefa katika ligi kuu kimeshuka sana, hali inayoshusha hadhi ya soka ya Uingereza kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment