Gareth Bale mshambuliaji wa Real Madrid |
MREMBO, Daniela Saurwald, ambaye ni mchumba wake hakuwapo hospitali sawa, lakini mama mzazi, Nancy, hakutaka kabisa kusubiri nyumbani.
Aliandamana na mumewe, Jorge, kumsindikiza mtoto wao Hospitali ya Northwestern Memorial huko Marekani. Daktari wa Real Madrid, Carlos Diez, alikuwapo na mwenzake wa timu ya taifa ya Argentina, Daniel Martinez, naye alikuwapo. Ni kutokana na uzito wa tatizo lililokuwa likimkabili mtu wao.
Daktari Fessler, ndiye aliyehusika kumpasua. Huyu ni Gonzalo Higuain, aliyelazimika kufanyiwa upasuaji misimu mitatu iliyopita kutokana na maumivu ya mgongo yaliyokuwa yakimsumbua na kutishia uhai wa soka lake.
Uzito wa maradhi yake ndio ulisababisha familia nzima ya Gonzalo kumsindikiza hospitali. Kocha Jose Mourinho akishinikiza afanyiwe upasuaji kwa sababu alimwonea huruma kutokana na hatima ya maisha ya soka la staa huyo wa Kiargentina walipokuwa pamoja Real Madrid.
Lakini, kwa sasa Gonzalo yupo Napoli kwenye Serie A na Mourinho amerudi Ligi Kuu England na kujiunga tena na Chelsea. Real Madrid imebaki na mkosi wake wa maradhi kama hayo kuwaandama wachezaji wake.
Agosti mwaka huu, Real Madrid, ilifanya kufuru baada ya kuvunja benki na kuandika historia mpya kwenye soka kwa kufanya usajili wa pesa nyingi zaidi duniani. Ni wakati walipomnasa winga wa Wales, Gareth Bale, kwa uhamisho wa Pauni 85 milioni.
Uhamisho ulikuwa gumzo Ulaya nzima na kuwafanya watu wengine wafike mbali na kuchambua mambo mengine ambayo yangeweza kufanywa kwa kutumia pesa hiyo ya usajili wa Bale.
Lakini hata mwaka ukiwa haujaisha, tayari Real Madrid inaonekana kama imeingia mkenge kwenye usajili huo uliowagharimu pesa nyingi.
Daktari asema Real Madrid imeliwa
Katika kusaka ukweli wa kitaalamu kuhusiana na maradhi ya mgongo yanayomsumbua Bale, gazeti maarufu jijini Madrid, MARCA lilifanya mahojiano na madaktari mbalimbali mahiri wa Kihispaniola.
Wakamfuata daktari mwenye hadhi kubwa, Avelino Parajon na akasema hivi: “Kama Real Madrid ilimsajili Gareth Bale ikidhani kwamba hili ni tatizo dogo tu, ilifanya kosa kubwa
“Tatizo hili huwezi kusema kwamba kesho tu atafanyiwa upasuaji na ataendelea kucheza kama ilivyotokea mara nyingi.
Lakini, kama ana tatizo la kutenguka visahani vya maungio ya mgongo si kitu unachoweza kukitambua na kukirekebisha kwa mara moja.”
Akaendelea: “Kama mtu anakuwa na matatizo hayo kwa umri wake (wa Bale) na kwa dalili zilivyo, ukweli hii ni dalili mbaya kwa mwanamichezo yeyote.”
Kumbe ni tatizo lake sugu
Wakati Real Madrid ikiendelea kusubiri majaaliwa ya staa wao mpya waliyemsajili kwa pesa nyingi apone maumivu ya mgongo, sasa imebainika kwamba maradhi yanayomkabili Bale yamekuwa yakimwandama kwa mrefu mrefu.
Makocha wa klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur katika kukabiliana na tatizo hilo, walimwaandalia mazoezi maalumu ili kuona kama ataondokana na maradhi hayo miaka mitatu iliyopita.
Lakini, staa huyo wa Wales, amedumu na tatizo hilo kwa muda mrefu tangu alipokuwa Southampton, hivyo Real Madrid itawagharimu pesa nyingi zaidi katika kumtafutia tiba sahihi mchezaji huyo ili aweze kuwa fiti.
Yaya Toure, Cazorla nao waugua
Bale atahitaji kusali ili itokee kama ilivyokuwa kwa beki wa Chelsea, John Terry, ambaye alikuwa na maradhi kama hayo, lakini baada ya kufanyiwa upasuaji alipona baada ya miezi mitatu tu.
Lakini, si Terry pekee, kiungo wa Ivory Coast na Manchester City, Yaya Toure, naye anasumbuliwa na mgongo. Tatizo kama hilo ndilo linalomsumbua kiungo mshambuliaji wa Arsenal, Mhispaniola Santi Cazorla.
Cazorla anafahamu uzito wa tatizo hilo na lilitibua mambo yake mengi na pengine kumfanya asicheze katika ubora wake.
Wachezaji wengine waliowahi kuteswa na maradhi kama hiyo ni kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon na kiungo Hamit Altintop, ambao walikutana na kisu ili kuwasaidia kutoka kwenye tatizo hilo. Yote hayo ni kutokana na kukosekana kwa tiba mbadala.
Acheza dakika 132 tu Real Madrid
Madaktari wa Real Madrid wanahaha kwa sasa kuhakikisha Bale anapona kabisa na kurudi uwanjani ili kuficha aibu ya bosi wao, Florentino Perez kumsajili kwa pesa nyingi, kumuuza Mesut Ozil na kisha kumkandia wakati mchezaji anayewatia jeuri ya kusema mengi kumbe ni mgonjwa kwa sasa.
Kama Bale ataendelea kukaa nje ya uwanja kutokana na maumivu hayo, Euro 100 milioni zilizotumika kwenye usajili wake zitakuwa hasara kubwa kwa Perez na Real Madrid.
Hadi sasa Bale amecheza dakika 132 tu kwenye kikosi cha Real Madrid. Alicheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Villarreal, kisha akacheza kwa dakika 20 tu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Galatasaray.
Alicheza dakika 10 dhidi ya Getafe na kwenye mechi dhidi ya mahasimu wao, Atletico Madrid, winga huyo alitumika kwa dakika 45 na baada ya hapo akakosekana uwanjani kutokana na kuumwa na hapo klabu ikaamua kumpumzisha.
Baada ya kucheza dakika 106 kwenye La Liga na 26 kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bale amefunga bao moja tu.
No comments:
Post a Comment