FAINALI za Kombe la Dunia zitakazochezwa Brazil
zimebakiza siku chache kabla ya kuanza Alhamisi ijayo. Wakati mashabiki
wa soka duniani kote wakizisubiri kwa hamu, kuna mechi tano za
kukumbukwa kwenye historia ya fainali hizo zilizoanza mwaka 1930.
5. Ureno 5-3 Korea Kaskazini - Robo fainali 1966
Benfica ilikuwa kwenye kiwango cha juu kwa klabu
za Ulaya mwanzoni mwa miaka ya sitini ikiwa imeshinda mataji ya Ulaya
mfululizo. Nyota wake wengi waliunda kikosi cha Ureno kwenye fainali za
Kombe la Dunia za mwaka 1966. Iliwachapa mabingwa watetezi Brazil kwenye
nusu fainali kabla ya kufungwa na wenyeji England. Mastaa wake wawili
walikuwa kiungo Mario Coluna na straika Eusebio, ambaye alimaliza kuwa
mfungaji bora kwenye fainali hizo na mabao yake tisa.
Ureno ilishinda mechi zote tatu kwenye hatua ya
makundi, ikiwa imefunga mabao tisa kwa jumla na kuitupa nje Brazil.
Lakini, kubwa ni vile walivyoweza kutokea nyuma kwa mabao 3-0 na
kuichapa Korea Kaskazini 5-3 kwenye robo fainali, Eusebio akifunga mabao
manne pekee yake.
4. Ujerumani Magharibi 3-3 Ufaransa - Nusu fainali 1982
Zikiwa zimepita siku tatu tu tangu iliposhuhudiwa
mechi ya mabao matano kati ya Brazil na Italia, shughuli ilikuwa pevu
kwenye nusu fainali katika fainali hizo zilizofanyika Hispania.
Ujerumani Magharibi na Ufaransa zote zilikuwa
makini na zilikuwa na wachezaji mahiri akina Michel Platini, Alain
Giresse, Jean Tigana, Paul Breitner, Uli Stielike na Pierre Littbarski.
Bao la mapema la Littbarski la kuongoza lilifutwa
na penalti ya Platini na kufanya mechi kuwa na upinzani zaidi. Kwenye
mechi hiyo kulitokea tukio la kushangaza baada ya kipa wa Ujerumani,
Harald Schumacher, kugongana na beki wa Ufaransa, Patrick Battiston na
beki huyo kung’oka meno mawili. Cha ajabu mwamuzi hakupiga hata filimbi.
Mechi hiyo iliingia kwenye muda wa nyongeza na
mabao mawili yalifungwa ndani ya dakika sita, Marius Tresor na Giresse
na wakati ikionekana kama Ufaransa itafika fainali, lakini Ujerumani
ilisawazisha kupitia Karl-Heinz Rummenigge na Klaus Fischer kabla ya
mechi hiyo kufikia kwenye mikwaju ya penalti na Ujerumani ilishinda
baada ya kipa Schumacher kuwagomea Didier Six na Maxime Bossis mikwaju
yao kutinga kwenye wavu wake.
3. Ujerumani Magharibi 3-2 England - Robo fainali 1970
Kombe la Dunia mwaka 1970 lilishuhudia mechi
nyingi za maana na tatu zikitajwa kuwa makini zaidi. Moja ya mechi hizo
ni robo fainali kati ya Ujerumani Magharibi na England, ikiwa ni kama
mechi ya marudiano ya fainali ya mwaka 1966.
England, iliongozwa na mastaa wake makini waliokuwa na timu hiyo
tangu mwaka 1966, Bobby Moore, Bobby Charlton, Martin Peters na Geoff
Hurst walicheza kwa kiwango kizuri kwenye dakika za mwanzo na kuongoza
kwa mabao 2-0 yalifungwa na Alan Mullery na Peters.
Kipindi hicho Ujerumani ilikuwa timu ngumu na
ilikuwa na wakali kama Franz Beckenbauer, Wolfgang Overath na Gerd
Muller, kocha Helmut Schoen alimwingiza Jurgen Grabowski na kubadili
kila kitu. Beckenbauer akafunga la kwanza kwa jitihada binafsi, kabla ya
Uwe Seeler kufunga la pili na kufanya mechi hiyo kuingia kwenye muda wa
nyongeza. Wajerumani hawakushikika tena na Muller akafunga bao la
ushindi kwenye dakika 108.
2. Brazil 1-1 Ufaransa - Robo fainali 1986
Likija suala la ufundi wa ndani ya uwanja, fainali
hizo za Kombe la Dunia 1986 zilikuwa kiboko zaidi. Kile kikosi matata
za Ufaransa kilichotisha kwenye miaka ya themanini kikiwa na wakali kama
Platini, Giresse, Tigana na Dominique Rocheteau kilikuwa kwenye zama
zake za mwisho. Fainali hizo zilikuwa za mwisho pia kwa magwiji wa
Brazil, Socrates, Junior na Zico.
Brazil iliiongoza kwa bao la Careca, kisha
ilipoteza nafasi nyingi za kufunga kabla ya Platini kuisawazishia
Ufaransa. Mashabiki wakaanza kuimba nyimbo za Zico wakitaka aingizwe,
Tele Santana akafanya maamuzi na Zico akaingia uwanjani kufanya mambo
yake.
Staa huyo makini alisababisha penalti, lakini kwa
bahati mbaya alikosa mkwaju huo baada ya kipa Joel Bats, ambaye alikuwa
mchezaji bora wa mechi kuiokoa. Ilipofika zamu ya kupita penalti,
manahodha wote Socrates na Platini hawakufunga na mwisho, Ufaransa
ilishinda vita.
1. Italia 4-3 Ujerumani Magharibi - Nusu Fainali 1970
Hii ilikuwa mechi ngumu iliyofanyika Juni 17, 1970
na baada ya hapo ikatajwa kuwa ‘Mechi ya Karne’. Dakika 90 zilikuwa
ngumu sana, Italia iliongoza tu katika dakika nane kupitia kwa Roberto
Boninsegna aliyepiga shuti kali. Ujerumani ilicharuka kusawazisha na
staa wao Beckenbauer akicheza na majeruhi yake aliisawazishia timu hiyo.
Jambo hilo lilifanya mechi hiyo kuingia kwenye
muda wa nyongeza. Mabao matano yalifungwa ndani ya dakika 30 na kuifanya
mechi hiyo kuwa na matokeo ya ajabu. Muller aliitanguliza Ujerumani kwa
bao safi, kabla ya Tarcisio Burgnich na Gigi Riva kubadili kibao.
Muller akawarudisha Ujerumani mchezoni tena kwa kusawazisha kwenye
dakika 110. Lakini, mpira wa adhabu uliopigwa na Gianni Rivera uliamua
matokeo ya mwisho ya mchezo huo na hatimaye Italia kuibuka uwanjani
kidedea.
No comments:
Post a Comment