WAPINZANI wote wa Yanga kwenye Ligi Kuu Bara
wakisikia hii lazima wakatangaze. Mwenyekiti wa timu hiyo Yusuf Manji
amekubali kugombea tena kwenye uchaguzi ujao.Lakini hiyo siyo tamu sana, kali ni kwamba
ametamka kwa mdomo wake mbele ya mamia ya wanachama jijini Dar es Salaam
kwamba Mbrazili, Marcio Maximo aliyejenga heshima ya Taifa Stars na
soka la Tanzania, ndiye kocha mkuu mpya wa Yanga.
Akitumia dakika 31 katika hotuba yake ya awali
kwenye mkutano mkuu wa Yanga uliofanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la
maofisa wa Polisi, Osterbay, jana Jumapili, Manji alitangaza msimamo
wake wa kutogombea na kuthibitisha ujio wa Maximo. Lakini baadaye
akahamasishwa na kubadili mawazo.
Katika mkutano huo wa dharura uliokuwa na agenda
moja ya mabadiliko ya Katiba, alisema: “Tunamalizia mazungumzo katika
mambo madogo ya maslahi, nathibitisha rasmi kwamba atakuja hapa, nataka
kumleta Maximo ili aendane na hadhi ya Yanga hatuna matatizo naye
anatuelewa vizuri na sisi tunamjua ni rafiki yetu wanachama tulieni.
“Kuhusu usajili wa timu, tumebakiza wiki mbili
kumalizia kamati ya usajili inaendelea na kazi hiyo, hatutaki kusajili
wachezaji wengi tutasajili wachezaji watatu wa ndani na wawili kutoka
nje, kikosi chetu si kibaya tunafanya kujazia tu, tumemfunga Al Ahly
hapa kwetu hiyo sio timu mbovu hata kidogo hata hili la kijana wetu Okwi
(Emmanuel) tutalimaliza hakuna shida.”
Mara baada ya kumalizika kwa majadiliano ya
mabadiliko ya katiba ambayo yote yalipita kama ilivyotakiwa, ilipofika
katika kipengele cha mengineyo wanachama wa Yanga waliibua hoja upya ya
Manji kutogombea tena ambapo kwa pamoja walisimama na kusema
hawakubaliani jambo ambalo lilianzisha mchakato mwingine mpya.
Hoja hiyo iliibuliwa na Mwenyekiti wa Baraza la
Wazee wa Yanga Mzee Jabir Katundu ambapo baada ya wanachama kutoa
msimamo huo ilimlazimu Manji kuomba ridhaa ya yeye na kamati yake ya
utendaji kutoka nje ya ukumbi na kuwaachia wanachama hao kujadiliana kwa
uhuru ambapo msimamo ulibaki uleule kuwa aendelee kwa miaka minne
ijayo.
Kufuatia msimamo huo Manji aliporudi alipewa
majibu hayo na yeye kuombwa aongoze kwa mwaka mmoja zaidi baada ya
wanachama wa Yanga kubariki kubadilishwa kwa tarehe ya mkutano mkuu wa
uchaguzi ambao sasa utafanyika Juni 14 mwakani.
“Lengo letu la kubadilisha tarehe ya uchaguzi ni
kwa vile hatutaki kuleta vurugu katika timu yetu kwa sasa kupitia
uchaguzi mkuu kama ambavyo inaendelea kwa wenzetu sasa, endapo tutafanya
uchaguzi mwaka huu ni wazi utaangukia katika kipindi cha mashindano,
nitaendelea mpaka mwakani lakini pia kipindi hiki nitakuwa nafikiria kwa
kina kuhusu hili ni lazima nizungume na familia yangu,”alisema.
Katika hatua nyingine Manji alizungumzia suala la
ujenzi wa uwanja wao ambapo amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Said Meck Sadick kwa kutoa jibu la kupatikana kwa eneo la ujenzi na
kuwashawishi wanachama kutowapa kura madiwani watakaobainika kukwamisha
mpango huo.
No comments:
Post a Comment