Monday, 24 March 2014

Jose Mourinho adai mechi ya Arsenal iliisha dakika ya saba tu



LONDON, ENGLAND
JOSE Mourinho ana dharau sana. Ameidharau Arsenal baada ya kudai kwamba wapinzani wao hao walikuwa ‘chamtoto’ walipoikabili timu yake juzi Jumamosi na Mreno huyo anasema Chelsea ilimaliza mechi ndani ya dakika saba tu.
Kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu England, Mourinho aliiongoza Chelsea kuichapa Arsenal ya Arsene Wenger mabao 6-0 uwanjani Stamford Bridge na hivyo kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Mourinho alisema aliwaagiza wachezaji wake waivuruge Arsenal na staili yao ya uchezaji na hadi zilipotimia dakika saba za mwanzo baada ya mabao ya Samuel Eto’o na Andre Schurrle mechi ilikuwa imemalizika, kwa mujibu wa tambo zake.
“Nadhani tulianza vizuri sana, dakika saba tu tulikuwa mbele 2-0 na mechi iliishia pale,” alisema Mourinho.
“Tulianza mechi kwa nguvu sana na hatukutaka kuwapa nafasi Arsenal. Tulijaribu kuwakaba na kuwashambulia kwa haraka. Baada ya mabao yale mawili, ilikuja penalti na kadi nyekundu ambayo ilikuwa mbaya sana kwao. Nadhani mechi nzima ilikwisha kila kitu ndani ya dakika 10 za mwanzo.”
Kwenye mchezo huo, mwamuzi Andre Marriner alimtoa kimakosa kwa kadi nyekundu beki Kieran Gibbs, licha ya kwamba Alex Oxlade-Chamberlain ndiye aliyekuwa ametenda kosa wakati alipocheza kwa mkono makusudi dhidi ya shuti la Eden Hazard.
Mourinho alisema: “Namwonea huruma refa. Kulikuwa na watu wengi sana kwenye boksi na baada ya shuti la Hazard kulionekana mchezaji ameruka kama kipa. Msaidizi wangu mmoja alisema alikuwa (Mikel) Arteta, mwingine alisema Chamberlain na refa au msaidizi wake alisema Gibbs. Yalikuwa maamuzi magumu. Kuhusu penalti ilikuwa penalti na kadi nyekundu ilistahili. Bahati mbaya imetolewa kwa kijana asiyekuwa na hatia.”

No comments:

Post a Comment