BEKI wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe ambaye Wekundu hao wana wasiwasi mkubwa wa kuporwa na Azam, ameonekana mazoezini kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe akipasha ndani ya uzi wa Azam FC.
Kapombe kwenye mazoezi hayo binafsi, juu alitinga fulana ya Recreativo Libolo ya Angola, chini akatinga bukta ya Azam na huwa hakosekani katika mechi za Azam mara kwa mara.
Simba kupitia kamati yao ya usajili imesisitiza itamrudisha Kapombe Msimbazi.
Mwanaspoti linajua kwamba mchezaji huyo amezungumza na vigogo kadhaa wa Azam
ambao wamemwahidi mambo mazuri lakini hajasaini chochote mpaka sasa.
Kapombe alisema mazoezini hapo kuwa ndani ya siku 14 atakuwa ameshafahamu majaliwa yake katika maisha ya soka lakini kwa sasa anafanya mazoezi binafsi chini ya usimamizi wa aliyekuwa kocha msaidizi wa Simba, Richard Amatre.
Mwanaspoti lilimshuhudia Kapombe akifanya mazoezi hayo kwenye Uwanja wa TCC Chang’ombe. Mchezaji huyo yupo nchini tangu Novemba mwaka jana baada ya kukacha kurudi katika klabu ya AS Cannes ya Ufaransa iliyomsajili kutoka Simba, baada ya kutokulipwa mishahara yake ya miezi mitatu.
“Kuhusu mambo yangu ya usajili nadhani kwa sasa siwezi kuzungumzia nahofu nitaharibu kila kitu kwani mazungumzo bado yanaendelea kwa watu wangu na timu inayonihitaji.Baada ya wiki mbili nitakueleza kila kitu kuhusu mambo yangu yote yaliyonitokea,” alisema Kapombe.
“Kwa sasa nafanya mazoezi binafsi na kocha Amatre ili nijiweke fiti kabla ya kuanza kucheza ligi.” Akizungumza na Mwanaspoti, Amatre alisema; “Namfanyisha mazoezi Kapombe ili asipotee kwani asipofanya mazoezi ataporomoka uwezo.”
Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema mipango inakwenda vizuri kuhakikisha wanamrejesha kikosini Kapombe ili kuimarisha timu
No comments:
Post a Comment