NI balaa. Ndivyo unavyoweza kusema kuhusiana na suala hili. Ni hivi mzozo unazidi kutokota miongoni mwa klabu za nchini kuhusiana na stahili wanayodai kuhusiana na uhamisho wa kiungo mkabaji wa Southampton, Victor Mugubi Wanyama, kutinga Ligi Kuu England.
Klabu kadhaa ambazo zimekuwa zikitarajia kupata fidia ya kukuza kipaji cha nahodha huyo wa Harambee Stars, zimesema bado hazijapokea fedha hizo wanazopaswa kupewa ikiwa ni miezi saba sasa tangu alipotua England akitokea Celtic ya Ligi Kuu Sctoland.
Uhamisho wa Wanyama wa dau la Sh1.68 bilioni, ulitoa matumaini makubwa kwa timu za nchini alizowahi kuchezea mwanasoka huyoc kwani zinaamini zinastahili kunufaika kwa mgawo wa fedha.
Hata hivyo matumaini ya klabu hizo yanaonekana kugeuka kuwa ndoto baada ya Chama cha Soka England (FA) kuchelewesha suala hilo kutokana na kuwepo na vuta nikuvute ya timu zipi ndiyo zina uhalali wa kupata mgawo.
Habari zinasema FA imeamua kusita, kwa kuwa taarifa za Wanyama zimekuwa na utata.
Novemba mwaka jana, FA iliripotiwa kukataa kupokea pasipoti ya Wanyama iliyowasilishwa mbele yake kwa mara ya pili kwa maelezo kuwa ilikuwa ikikinzana maelezo na ile ya awali iliyotumwa na mamlaka za soka nchini.
Nairobi City Stars ni miongoni mwa timu zinazotarajia kunufaika na Sh8 milioni kutokana na dili la Wanyama.
Ili kujihakikishia kupata fedha hizo, inadaiwa kuwa klabu hiyo kwa msaada wa wanasheria, imemwandikia barua Wanyama kumtaka asaidie katika kutatua tatizo hilo kwa kueleza kwa kina ni timu zipi alizozichezea nyumbani kabla ya milango ya neema kumfungukia na kujikuta Ulaya.
City, miongoni mwa timu zitakazoshiriki Ligi Kuu Kenya msimu huu, haina wadhamini. Kwa maana hiyo inazisubiri kwa hamu fedha hizo.
Fedha hizo ni zaidi ya zinazotolewa na Super Sport (Sh5 milioni kwa kila timu ya ligi kuu).
Timu nyinginezo zinazotolea macho mgawo wa fedha hizo ni pamoja na AFC Leopards, Mathare United na JMJ Academy.
No comments:
Post a Comment