RAIS Uhuru Kenyatta ameviagiza vyombo vya michezo kuhakikisha vinafanya uteuzi makini wa vikosi vitakavyoliwakilishi taifa kwenye Michezo ya Madola itakayofanyika Scotland ili kuleta ushindi katika kila kitengo.
Kenyatta alizungumza hayo juzi Jumapili akiwa Ikulu ya Mombasa alipopokea Mwenge wa Malkia wa Uingereza uliotua nchini kwa ajili ya kutembezwa kwa siku mbili kabla ya kutalii mataifa mengine 77 wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Msafara wa kutembeza mwenge huo uliongozwa na jagina wa mbio ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Olimpiki ya Kenya (NOCK), Kipchoge Keino, ambaye pia atauongoza ujumbe huo kuzuru mataifa jirani ya Tanzania na Uganda kwa shughuli sawia.
“Serikali yangu inazidi kujituma kwa kuweka mikakati mwafaka ya kuhakikisha kwamba sekta ya michezo ya taifa hili inaimarika. Mengi yanahitaji kufanywa na mashirikisho yote ya michezo ili kuviandaa vikosi mbalimbali vitakavyowakilisha taifa katika michezo ya Madola na yale ya Olimpiki kwa vijana chipukizi,” alisema.
“Taifa linahitaji ushindi katika kila mchezo tutakaoshiriki, ni suala la kujiandaa mapema kwa maandalizi stahili.”
Mwenge huo unapigia debe mashindano hayo yatakayoandaliwa Agosti huko Glasgow yakizikutanisha nchi zilizowahi kuwa makoloni ya Uingereza.
No comments:
Post a Comment