Friday, 8 November 2013

Wanasayansi wafichua siri ya Messi kumfunika Ronaldo

Utafiti uliofanywa na wanasayansi hao kutoka kwenye vyuo vikuu tofauti duniani umebainisha siri kubwa
 inayomfanya Messi azidi kumfunika Ronaldo kwa ujuzi wa ndani ya
 uwanja na jambo hilo ndilo linalomfanya staa wa Ureno (Ronaldo) awe
wa kushika nafasi ya pili nyuma ya Muargentina huyo

MADRID, HISPANIA
ACHANA na vita ya Barcelona na Real Madrid, mchuano wa tuzo ya Ballon d’Or (mwanasoka bora wa mwaka wa Fifa) na umahiri wa ndani ya uwanja. Wanasoka Lionel Messi na Cristiano Ronaldo vita yao ya sasa ni kufukuzia rekodi ya Raul kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Pamoja na kuwapo mchuano huyo, wako wanasayansi wanaosema kwamba, Messi staa wa Barcelona ataendelea kutamba.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi hao kutoka kwenye vyuo vikuu tofauti duniani umebainisha siri kubwa inayomfanya Messi azidi kumfunika Ronaldo kwa ujuzi wa ndani ya uwanja na jambo hilo ndilo linalomfanya staa wa Ureno (Ronaldo) awe wa kushika nafasi ya pili nyuma ya Muargentina huyo.
Madai ya wanasayansi
Wataalamu hao wamefanya utafiti wao na kufichua kwamba wachezaji wanaotumia mguu wa kushoto wana uwezo mkubwa kiakili na ndio maana Messi amemzidi uwezo Ronaldo.
Utafiti huo uliofanyika katika vyuo vikuu vya Oxford, St. Andrews na Bristol, unasema kwa kuwa Messi anatumia mguu wa kushoto, ubongo wake unafanya kazi kubwa sana anapokuwa ndani ya uwanja pengine mara mbili zaidi ya Ronaldo.
Wachezaji wanaotumia mguu wa kushoto ubongo wao unafanya kazi kwa haraka sana na kufanya mambo yasiyotarajiwa tofauti na ilivyo kwa wanaotumia mguu wa kulia.
Baadhi ya wachezaji waliotajwa kwenye utafiti huo wanaotumia mguu wa kushoto na kufanya mambo makubwa ndani ya uwanja ni pamoja na David Silva, Messi, Gareth Bale, Diego Maradona, Mesut Ozil na Ryan Giggs na kupitia nyota hao wachache, unaweza kutambua umakini na viwango vyao wanapokuwa uwanjani.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hiyo ndio sababu inayomfanya Ronaldo ashindwe kumfunika Messi kwa ujuzi na ubunifu wa ndani ya uwanja, licha ya wawili hao kutajwa kuwa ndio wanasoka walio kwenye ubora mkubwa wanaotamba duniani kwa sasa.
Kufukuzia rekodi ya Raul
Wakati wanasubiri Ballon d’Or Januari mwakani, Ronaldo na Messi kwa sasa wapo kwenye vita mpya ya kufukuzia rekodi ya mabao iliyowekwa na Mhispaniola, Raul Gonzalez Blanco, kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya
Staa huyo amefunga mabao 71 kwenye michuano hiyo mikubwa na alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 33 kabla hajastaafu soka.
Mabao yake yamebaki kuwa rekodi kwenye Ligi ya Mabingwa, ilimchukua mechi 144 staa huyo wa zamani wa Real Madrid na Hispania kuweka alama zake katika michuano hiyo mikubwa kabisa kwa ngazi za klabu barani Ulaya.
Wakati akiwa ameondoka zake kwenye soka, nyuma ameacha vita ya mafahari wawili wanaoshindania kuifukuzia rekodi yake. Watu hawa ni mahasimu wakubwa, Messi na Ronaldo.
Nani ataifikia rekodi ya Raul?
Msimu huu, Messi anacheza akiwa na umri wa miaka 26, wakati mpinzani wake ana miaka 28.
Mastaa hawa wana nafasi kubwa ya kuifikia rekodi ya Raul tena wakiwa pungufu kwa karibu mechi 50.
Achana na mbio za kuwania Mpira wa Dhahabu, vita hii ya Messi na Ronaldo kwenye kumfukuzia Raul haitakuwa na pointi za kupigiwa kura, bali ni idadi ya mabao watakayofunga katika michuano hiyo mikubwa ili kumpiku Mhispaniola huyo.
Msimamo wa mabao ulivyo
Messi ameshika usukani kwa kufikisha mabao 65, sita tu kuifikia rekodi hiyo ya Raul wakati Ronaldo anafuatia kwenye nafasi ya pili na mabao yake 59.
Kwenye 10 bora ya wenye mabao mengi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ni Ronaldo na Messi tu ndio pekee wanaoendelea kucheza michuano hiyo hadi sasa.
Wakali wengine wenye mabao mengi ni Mdachi Ruud van Nistelrooy (56), Thierry Henry (50), Alfredo Di Stefano (49), Andriy Shevchenko (48), Eusebio (46), Philippo Inzaghi (46) na Didier Drogba (42).

Vita yao inavyokwenda
Ronaldo amefikisha mabao 59 katika mechi 96, wakati Messi mabao yake amefunga baada ya kucheza mechi 82. Kama Ronaldo ataendeleza rekodi yake ya wastani wa mabao anaofunga kwenye kikosi cha Real Madrid na akicheza kila mechi hadi fainali, atakuwa na mabao tisa zaidi.
Rekodi za sasa zinaonyesha amefunga mabao manane katika mechi nne, sawa na wastani wa mabao mawili kwa kila mechi. Akiendelea kufanya hivyo anaweza kufunga mabao 18 zaidi na jambo hilo litamfanya kufikisha mabao 77.
Ni jambo linaloonekana gumu kiuhalisia, lakini kwa Ronaldo kitu kama hicho kinawezekana. Akifanikiwa hilo atakuwa amefunga mabao 222 katika mechi 215 kwenye kikosi hicho cha Real Madrid.
Lakini, kwa Ronaldo kumfikia Raul ni lazima ampiku kwanza Messi. Staa huyo wa Barcelona alifunga mabao mawili Jumatano iliyopita kwenye mechi dhidi ya AC Milan na rekodi yake ni kwamba amefunga mabao sita katika mechi tatu msimu huu.
Kwa kuendelea na rekodi hiyo na akioongoza Barcelona hadi fainali, Muargentina huyo atakuwa amefikisha mabao 83.
Wawili hao wote wanayo nafasi ya kuivunja rekodi ya mabao ya Raul ambaye bao lake la mwisho la Ligi ya Mabingwa Ulaya alilifunga kwenye robo fainali miaka miwili iliyopita akiwa na kikosi cha Schalke 04.
Kwa hali ilivyo kwa sasa, kama rekodi hiyo ya Raul itashindwa kuvunjwa msimu huu, basi mwakani atakuwa Messi au Ronaldo watakaoandika majina yao katika kurasa za kihistoria, lakini jambo hilo haliwezi kufika mwakani mechi bado nyingi msimu huu na wakali hao wanatarajiwa kuendelea kutikisa nyavu.

No comments:

Post a Comment