Friday, 8 November 2013

TANZANITE YATUA SALAMA MAPUTO

Tanzanite Stars


Kikosi cha timu ya Taifa ya wanawake chini ya miaka 20 (Tanzanite) kimewasili salama jijini Maputo, Msumbiji tayari kwa mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza ya Kombe la Dunia itakayochezwa kesho (Novemba 9 mwaka huu).

Kwa mujibu wa kiongozi wa msafara wa Tanzanite, Kidao Wilfred ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), timu hiyo chini ya Kocha wake Rogasian Kaijage ilifanya mazoezi yake ya kwanza jana asubuhi.

Tanzanite itafanya mazoezi yake ya mwisho leo (Novemba 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Zimpeto ambao ndiyo utakaotumika kwa mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni kwa saa za Msumbiji.

Nao wachezaji waliobaki kumalizia mtihani yao ya kidato cha nne wameondoka leo saa 11 jioni kwa ndege ya LAM wakiongozwa na naibu kiongozi wa msafara, Khadija Abdallah Nuhu ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA).

KESSY KUSIMAMIA MECHI YA KOMBE LA DUNIA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Lina Kessy kuwa kamishna wa mechi ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kwa wanawake chini ya umri wa miaka 20 kati ya Afrika Kusini na Botswana.

Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza itachezwa nchini Afrika Kusini, Novemba 9 mwaka huu. Waamuzi kutoka Zambia ndiyo watakaochezesha mechi hiyo namba kumi.

Waamuzi hao wataongozwa na Glads lengwe atakayepuliza filimbi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bernadette Kwimbira kutoka Malawi, namba mbili ni Mercy Zulu na mezani atakuwepo Sarah Ramadhani, wote wa Zambia.

Afrika Kusini ilishinda mechi ya kwanza ugenini mabao 5-2. Mshindi wa mechi hiyo atacheza raundi ya pili na mshindi wa mechi kati ya Tanzania na Msumbiji.

No comments:

Post a Comment