Ashley Young akilalamika apewe penalti kwenye mechi ya Ligi Kuu England kati ya Manchester United na Aston Villa kwenye Uwanja wa Old Trafford. |
MADRID, HISPANIA
MWINGEREZA Ashley Young alipoanguka na kuisaidia Manchester United kupata penalti kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Sociedad usiku wa juzi Jumanne, hakuna aliyeshangazwa.
Staa huyo ana historia ya kujiangusha na alishawahi kukanywa na kocha wake wa sasa David Moyes na hata yule wa zamani Sir Alex Ferguson kuhusiana na tabia hiyo mbaya mchezoni. Kitendo cha kujiangusha mara kwa mara kinawakera wengi, wanachukizwa na Young kwasababu amekuwa akiwadanganya waamuzi na kutoa penalti ambazo kiuhalisia hazina ukweli wowote.
Kwenye Ligi Kuu England, Young amesababisha penalti zaidi ya nne ambazo zinatokana na kujiangusha kwake, kwenye timu ya taifa amesababisha penalti moja.
Penalti yake katika mechi na Sociedad imewachefua wengi na kuanza kuorodhesha idadi ya penalti zote zenye utata ilizopata Manchester United na England zilizosababishwa na winga huyo wa zamani wa Aston Villa.
Novemba 5, 2013: Man United 0-0 Real Sociedad
Sawa haukuwa usiku mzuri kwa Robin van Persie na Javier Hernandez baada ya kuikosesha Manchester United ushindi, huku Marouane Fellaini naye akishuhudia kadi nyekundu. Lakini, aliyetibua zaidi usiku huo mtamu wa Ligi ya Mabingwa ni winga Ashley Young, ambaye aliendelea na utamaduni wake wa kujiangusha na kutengeneza penalti.
Baada ya kuwadanganya marefa wengi England, safari hii Young aliweza kumrubuni mwamuzi Mtaliano Nicola Rizzoli mbele ya mashabiki wapatao 28,000 kwa kujiangusha na kusababisha penalti kwa Manchester United.
Young alikwenda chini kirahisi sana baada ya kupokea pasi ya kisigino kutoka kwa Shinji Kagawa, lakini kilichowakera wengi ni jinsi alivyojiangusha utadhani amefanyiwa faulo kubwa. Hata hivyo, Manchester United ilishindwa kufunga mkwaju huo wa penalti baada ya Mdachi van Persie kukosa.
Septemba 14, 2013: Man United 2-0 Crystal Palace
Kwenye mchezo huu, Young alishitukiwa na mwamuzi Jon Moss na kuonyeshwa kadi ya njano kutokana na kujiangusha baada ya kuguswa na Kagisho Dikgacoi. Lakini, kwenye mchezo huo huo, baadaye alijilegeza tena na kwenda chini kirahisi na kusababisha penalti huku akimsababishia Dikgacoi kutolewa kwa kadi nyekundu.
Baada ya tukio hilo, Moyes alisema: “Sitaki wachezaji wangu wajiangushe. Nitamweleza Ashley kitu kama kile sitaki kukiona.” Kwa tukio la mechi na Sociedad inaonekana ni ngumu kwa staa huyo kuacha tabia yake hiyo mbaya ya kuuchafua mchezo mzuri wa soka.
Aprili 15, 2012: Man United 4-0 Aston Villa
Dhidi ya klabu yake ya zamani, Young alikwenda chini kama kawaida yake na kusababisha penalti iliyoifanya Manchester United kufunga bao la pili. Kocha wa zamani wa kikosi hicho, Sir Alex Ferguson alisema Young alijiangusha kirahisi sana.
Aprili 8, 2012: Man United 2-0 QPR
Young alijiangusha bila ya kusumbuliwa kitu baada ya kukabwa na beki wa QPR, Shaun Derry kwenye eneo la hatari. Beki huyo alitolewa kwa kadi nyekundu na straika Wayne Rooney alifunga mkwaju huo wa penalti.
Baada ya mechi, Bosi wa QPR, Phil Beard aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter: “Ni ngumu sana kuelewa kilichotokea baada ya kurudia kulitazama tukio lile, lakini Ashley Young anapaswa kuungana na Tom Daley kwenye Olimpiki.”
Oktoba 23, 2011: Man United 1-6 Man City
Kwenye mechi ya kichapo cha mabao 6-1 kutoka kwa mahasimu wao Manchester City, Young alijiangusha baada ya kunyoosha mguu wake kumfikia James Milner na kisha akajiangusha akilalamikia penalti. Kwa bahati mbaya kwake, mwamuzi aliitoa nje na kuwa adhabu ya kawaida.
Oktoba 12, 2010: England 0-0 Montenegro
Young alionyeshwa kadi ya njano baada ya kujiangusha na kugalagala kwenye sare ya bila kufungana dhidi ya Montenegro katika Uwanja wa Wembley.
Baada ya mechi, Young alisisitiza kwamba alitendewa madhambi. Kwa matukio hayo, waamuzi sasa wanaanza kumsoma Young na kwamba atakuwa kwenye hatari kubwa ya kuadhibiwa hata kama amechezewa rafu ya kweli.
Keane amkosoa
Kiungo na nahodha wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amemkosoa vikali Ashley Young kutokana na tabia yake ya udanganyifu dhidi ya waamuzi kwa kujiangusha na kusababisha penalti zenye utata
Keane amemshutumu winga huyo baada ya tukio lake la juzi alipojibwaga chini kufuatiwa kuguswa kidogo na beki wa Sociedad, Markel Bergara na kusababisha penalti iliyopigwa na Van Persie na kugonga mwamba.
Moyes, ambaye mwanzoni aliwahi kumkosoa Young kwa vitendo hivyo, kwenye mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa hakusema kitu cha kumkandamiza nyota wake baada ya kusema mwamuzi amefanya uamuzi wake.
No comments:
Post a Comment