Winga wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe |
WINGA wa zamani wa Simba, Ulimboka Mwakingwe amevunja ukimya na kusema kwamba tatizo Simba si kocha bali ni wachezaji wa bei chee ambao wanahitaji muda mrefu
.
Mchezaji huyo alienda mbali zaidi na kusisitiza kwamba uongozi unahitaji kuunda kamati kwa kuzingatia uwezo wa mhusika kiufundi kuliko kuangalia utajiri wake au uswahiba.
Ulimboka alisema kama wasipofanya usajili mzuri kwenye dirisha dogo basi ubingwa watausikia hewani kwani wachezaji wengi waliopo si wa ushindani bali wa kawaida sana jambo ambalo linawagharimu na hawaendani na hadhi ya Simba ambayo yeye ni mwanachama.
“Makocha sioni kama wana tatizo ila aina ya wachezaji walionao, wao wanawatumia sana vijana wale lakini kwa levo yao bado sana kucheza kiwango cha ushindani kwenye ligi, wale vijana uwezo wanao lakini hawajafikia levo ya kushindana kuonyesha kuwa timu inataka kweli pointi tatu na hawajafikia kiwango cha kukabidhiwa dhamana ya Simba ninayoijua mimi,” alisema.
“Haiwezekani mchezaji anatoka timu B moja kwa moja anapangwa kucheza nafasi ngumu kama beki wa kati au straika, si unatafuta majanga tena? Wapewe nafasi lakini walipaswa kuwa na sapoti ya wakubwa wengi ambao walipaswa kusajili kwa klabu kuingia mfukoni si kukusanya wa bei rahisi kutimiza idadi.
“Dirisha dogo linakuja waangalie wachezaji wazoefu kwenye timu nyingine za ligi kama vile wanavyosajili wachezaji wa nje na watoe fedha wasajili wazoefu wa ndani ili timu ipate mafanikio kama ilivyokuwa zamani,”alisisitiza.
Mchezaji huyo pia aliwataka viongozi kuheshimu michango na mawazo ya wachezaji wa zamani katika usajili ili kuisaidia timu hiyo kupata wachezaji wa kiwango cha juu badala ya kusajili kishabiki au kwa kubebana
No comments:
Post a Comment