Tuesday, 5 November 2013

CHELSEA INAVYOTESA NA DAKTARI MREMBO


 
 Chelsea inatesa na daktari wake mrembo, Eva Carneiro. Wenye kejeli wanadai kwamba uwepo wa daktari Eva ndio chanzo cha Ashley Cole na John Terry kuugua mara kwa mara. Lakini, hayo ni masihara tu.


LONDON, ENGLAND
ITALIA kumeibuka mjadala mzito kwamba AC Milan imemwajiri mrembo kwenye jopo la madaktari wa timu hiyo ili kuwa kama Chelsea. Kwenye mitandao ya kijamii kunasambazwa picha ya mrembo, akitajwa kuwa ni daktari mpya wa AC Milan, licha ya mabosi wake kuwa hawajathibitisha bado.
Wakati jina la mrembo huyo likisakwa, mjadala huo ulivuka mipaka hadi kwenye Ligi Kuu England, Stamford Bridge ambako kuna daktari wa kike anayetesa kwenye ligi hiyo.
Chelsea inatesa na daktari wake mrembo, Eva Carneiro. Wenye kejeli wanadai kwamba uwepo wa daktari Eva ndio chanzo cha Ashley Cole na John Terry kuugua mara kwa mara. Lakini, hayo ni masihara tu.
Tangu alipotua Stamford Bridge, Eva amekuwa maarufu kwa kuwa daktari wa kike kufanya huduma kwenye klabu kubwa kama Chelsea na kuweza kuhimili mikikimikiki ndani ya klabu hiyo.
 AVB ampandisha Stamford Bridge
Hakikuwa kitu kinachotarajiwa kufanywa na Chelsea au na mmiliki wake bilionea wa Kirusi, Roman Abramovich, lakini mara baada ya kuchaguliwa kuinoa timu hiyo mwaka 2011, Andre Villas-Boas alifanya usajili wa nguvu kwa kumnasa Eva ili kuwa daktari wa kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Uwepo wa Eva kwenye benchi la Chelsea kulianza kuwavuta wengi na kuifanya timu hiyo kutikisa England kwa kuwa daktari wa kike, ambaye amekuwa akiwapa burudani mashabiki pia wakati anapokimbia kuingia ndani ya uwanja kutoa huduma endapo kama kuna mchezaji wa Chelsea aliyeumia.
Kwa mujibu wa wasifu wake kwenye tovuti ya Chelsea, Eva aliwahi pia kufanya kazi katika kikosi timu ya Olimpiki ya Uingereza kama daktari wa timu ya wanawake.
Cole asahau Chelsea imefungwa
Uwanja wa Hawthorns kwenye mechi ya Ligi Kuu, dakika 90+4, Chelsea ikiwa nyuma 1-0 nyumbani kwa West Bromwich Albion, Machi 3, 2012, Cole alianguka chini kuugulia kwamba ameumia.
Lakini, beki huyo wa kushoto baada ya Eva kuingia uwanjani kumpatia huduma, alipoinama kumuuliza tatizo linalomsumbua huku mikono yake ikiwa imemshika mgongoni mchezaji huyo, Cole alizubaa chini na kushindwa kutambua kwamba alipaswa kunyanyuka haraka kwa kuwa tayari timu yake ilikuwa nyuma kwa bao 1-0.

Imedaiwa huduma ya mrembo huyo ilimzubaisha Cole na kushindwa kutambua kwamba Chelsea ilipaswa kupambana walau kusawazisha bao hilo ili kunusuru kibarua cha aliyekuwa kocha wao kwa kipindi hicho, Villas-Boas.
Aanzia kikosi cha akiba
Daktari Eva anayeripotiwa kuwa na uzoefu mkubwa kutokana na kufanya kazi katika taasisi kubwa tofauti, alianzia kwenye kuwatibu wachezaji wa kikosi cha akiba kabla ya kupandishwa kwenye kikosi cha kwanza katika msimu wa 2011-2012 na kocha AVB.
Haijafahamika sababu ya AVB kumpandisha mrembo huyo na kumtaka awe daktari wa wachezaji wake wa kikosi cha kwanza na watangulizi wake hawakuwa wakifikiria mpango huo.
Moja ya wachezaji wa kikosi cha kwanza waliowahi kufurahia huduma ya mchezaji huyo ni Terry wakati alipokuwa akisumbuliwa na maumivu ya goti.
Ashabikia Chelsea
Japo kumekuwa na ugumu kidogo wa kufahamu mambo yake binafsi, lakini taarifa zilizopatika Septemba 2009 ni kwamba mrembo huyo ni shabiki mkubwa wa Real Madrid. Lakini, hivi karibuni alidaiwa kuwa ni shabiki mkubwa wa Chelsea na hilo lilijionyesha dhahiri wakati timu hiyo iliponyakua ubingwa wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Anachodai mwenyewe ni kwamba alianza kujihusisha na mambo ya soka katika fainali za Kombe la Dunia 1998 na hasa alipotazama mechi ya Brazil na Mexico. Wazazi wa Eva wana asili ya Uingereza na Hispania, lakini anaonekana kuwahusudu sana Wabrazili.
Kazi nyingine ya mrembo huyo kwenye kikosi cha Chelsea ni kuhakikisha anawasaidia wachezaji kupata usingizi hasa wanapokuwa kwenye nchi ambayo majira yake yana tofauti kubwa na England.
Nesta alipata mke
Kwenye fainali za Kombe la Dunia 1998 zilizofanyika Ufaransa, beki wa kati wa zamani wa Italia, Alessandro Nesta ndiko alipompata mkewe Gabriela Pagnozzi.
Nesta, ambaye alifunga ndoa na Gabriela, Mei 7, 2007, alisema mapenzi na mrembo huyo yalianza baada ya kuumia kwenye fainali hizo na kisha huduma zote alikuwa akizipata kutoka kwake


Gabriela alikuwa mfanyakazi tu katika kambi ya Italia katika fainali hizo na alipewa jukumu la kumhudumia Nesta alipopata majeruhi kwenye mechi dhidi ya Austria.
“Ninachoweza kusema, niliumia kule Ufaransa na kisha yeye akawepo jirani yangu kwa ajili ya kunihudumia.
Maumivu yangu yamekwisha na yeye ameendelea kubaki na mimi,” alisema Nesta ambaye amezaa watoto Sofia na Tommaso katika uhusiano huo

No comments:

Post a Comment