Tuesday, 5 November 2013

Kumbe Yaya hakumwonea Kaseja






WAKATI mashabiki wa soka nchini Tanzania wakiamini kwamba, Juma Kaseja, alikosea kufungwa bao la faulo na kiungo wa kimataifa wa Ivory Coast, Yaya Toure, katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia, rekodi zinaonyesha kwamba Toure amekuwa akifunga mabao ya aina ile kila kukicha.
Toure vs Gambia
Katika Uwanja wa Bakau jijini Banjui nchini Gambia wiki moja kabla ya Toure hajamtungua Kaseja, Toure alifunga bao kama lile katika dakika ya 89 mnamo Juni 8, 2013.
Ivory Coast ilikuwa inaongoza kwa mabao mawili yaliyofungwa na mkali wake anayekipiga katika klabu ya Anzhi Makhachkala, Lacina Traore na jingine likifungwa na Wilfried Bony.
Toure vs Juma Kaseja
Wiki moja baadaye yaani Juni 14, 2013, timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, ilikuwa wahanga wa faulo ya Toure. Awali Stars ilipata bao la kuongoza kupitia Amri Kiemba, lakini Lacina Traore akasawazisha. Dakika ya 23, Toure akamtungua Kaseja kwa staili ile ile aliyotunguliwa kipa wa Gambia.
Ukuta wa Stars ulionekana mfupi kwa Toure na hata Kaseja akalaumiwa kwa ufupi dhidi ya shuti la Toure, lakini kumbe ilikuwa ni moja kati ya mashuti ya kawaida ya Toure dhidi ya ukuta wa wapinzani na kipa wao. Thomas Ulimwengu alisawazisha, lakini Toure akafunga tena kwa penalti. Baadaye Ivory Coast wakafunga bao la nne.
Toure vs Newcastle
Kama ilivyokuwa kwa Kaseja basi ndivyo ilivyokuwa kwa kipa wa Newcastle United, Ruud Krul. Hii ilikuwa ni katika mechi ya kwanza ya ufunguzi wa Ligi Kuu England msimu huu. Mechi hiyo ilipigwa Agosti 19, 2013 Jumatatu usiku. Faulo ilifanyika nje ya eneo la hatari la Newcastle katika eneo lile lile ambalo Taifa Stars walifanya madhambi dhidi ya Ivory Coast.
Safari hii Toure alikumbana na ukuta wa wachezaji warefu wa Newcastle kama vile Steven Taylor, Mapou Yanga-Mbiwa, Fabio Coloccini na wengineo, lakini Toure aliunyanyua mpira kwa staili ileile ya dhidi ya Stars na ulipotua, mpira ulikwenda nyavuni na kumwacha Krul akiwa hana la kufanya.
City waliikandamiza Newcastle mabao 4-0 ambapo wafungaji walikuwa David Silva, Sergio Aguero na Samir Nasri. Ilithibitisha kwamba Toure hakumwonea Kaseja

Katika pambano la pili la nyumbani la ligi dhidi ya Hull City Agosti 31, 2013, Toure alifunga kwa staili ile ile aliyotumia kumfunga Kaseja. Kulikuwa hakuna kitu ambacho kipa wa Hull City, Allan McGregor angeweza kufanya.
Samir Nasri alikuwa amefanyiwa madhambi katika kona ya nje ya eneo la hatari la Hull City. McGregor aliupanga ukuta wake wenye wachezaji warefu kwa umaridadi mkubwa, lakini Toure alifanya kile kile ambacho alimfanyia Kaseja pale Uwanja wa Taifa.
Aliunyanyua mpira kwa umaridadi mkubwa na ulipotua ulikwenda moja kwa moja katika nyavu za Hull City. 
Kiungo wa Hull City ambaye pia ni kiungo wa timu ya taifa ya Misri, Ahmed Elmohamady, alijaribu kukimbilia katika lango lake kwa ajili ya kuzuia mpira huo lakini hakufanikiwa. Bao la kwanza la Manchester City lilifungwa na Alvaro Negredo kwa kichwa.
Toure vs Wigan Atheltic
Katika pambano la Kombe la Ligi dhidi ya Wigan Athletic uwanjani  Etihad Septemba 24, 2013, kipa wa Wigan, Lee Nicholls, naye aliendelea kuwa mhanga wa mashuti ya Toure kama ilivyokuwa kwa Kaseja.
Baada ya City kupata faida ya mpira wa adhabu nje ya lango la Wigan, Nichollas aliupanga ukuta wake kwa umaridadi mkubwa, lakini bado Toure alifanikiwa kuuvusha mpira kwa umaridadi na kuuingiza wavuni.
Mwisho wa pambano City iliibamiza Wigan mabao 5-0 mengine yakifungwa na Edin Dzeko, Stevan Jovetic na kiungo wa pembeni kutoka Hispania, Jesus Navas.
Toure vs Norwich City
Katika ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Norwich City Jumamosi lisingeweza kukosekana bao la Toure, hasa la namna ileile ambayo alimtungua Juma Kaseja.
Dakika ya 59, beki Bradley Johnson alimchezea rafu mbaya mshambuliaji, Edin Dzeko, nje ya eneo la hatari la Norwich. Toure kama kawaida aliuchukua mpira na kuuweka mbele ya ukuta kabla ya kupiga faulo maridadi katika upande wa nyavu zile zile alizomfunga Kaseja.
Kipa John Ruddy asingeweza kufanya lolote kuzuia bao hilo. Mabao mengine ya City yalifungwa na Bradley Johnson (aliyejifunga mwenyewe), David Silva (20), Matija Nastasic (25), Alvaro Negredo (36), Sergio Aguero (71) na Edin Dzeko (86).

Hii ni kwa mara ya kwanza Manchester City imefunga mabao saba tangu ilipofanya hivyo, Desemba 1968 katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Burnley.

No comments:

Post a Comment