LICHA ya kuambulia sare ya mabao 3-3 na kutumia gharama nyingi, kambi ya siku chache waliyopiga Yanga mjini Pemba kujiandaa na mechi dhidi ya Simba imewapa hasara.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ametamka kwamba tatizo la kuwepo majeruhi wengi kikosi hicho kwa sasa kumetokana na uchakavu wa Uwanja wa Gombani, Pemba walioutumia kwa mazoezi makali kuhakikisha mnyama anateketea kabisa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Brandts, ambaye anapinga utaratibu wa timu kukaa kambini wiki nzima kama baadhi ya viongozi wanavyodai aliweka wazi kwamba: “Unajua tulipokuwa kambini kule Pemba uwanja wa mazoezi ulikuwa na nyasi ndefu, hali hiyo ndiyo imesababisha kuwepo kwa majeruhi wengi, wachezaji wengi walipata majeraha.”
Kocha huyo alisema kwamba hali ya uwanja huo ilifanya wachezaji wengi kuwa na majeruhi ya aina mbalimbali na mengine yalikuja kujitokeza baadaye.
Alisema kwamba walilazimika kuutumia uwanja huo unaotumika pia kwa Ligi Kuu Zanzibar kwa vile walikuwa hawana jinsi na ndio uliokuwa karibu na kambi na wenye afadhali.
Yanga inakabiliwa na majeruhi ambao wamekuwa wakiathiri utendaji wa kikosi cha kwanza ingawa kwenye msimamo ipo pazuri.
Majeruhi wa muda mrefu wa Yanga ambao hawajaanza mazoezi ni David Luhende, Nizar Khalfan, Juma Abdul, Bakari Masoud na Salum Telela.
Mbuyu Twite, Athuman Idd ‘Chuji’ na Hussein Javu jana Jumatatu walishindwa kufanya mazoezi na wenzao. Mbuyu anaugulia majeraha ya paja la mguu wa kulia, tangu alipoumia katika mechi yao na JKT Ruvu akatolewa na nafasi yake ya beki wa kulia ilichezwa na Ibrahim Job.
Javu anaumwa sawa na Chuji, lakini tatizo la Chuji hakutoa taarifa zozote kwa kocha wake, Brandts wala daktari wa timu, Nassor Matuzya kama inavyotakiwa na hawana taarifa zake.
“Twite hali yake bado tangu alipoumia siku ile ya mechi, naendelea kufuatilia afya yake kujua kama anaweza kuanza mazoezi kesho (leo Jumanne) au bado, Javu pia anaumwa,” alisema Matuzya huku akikataa kufafanua nini hasa kinachowasumbua Javu na Chuji.
No comments:
Post a Comment