Thursday, 21 November 2013

TFF yamzuia Moses Oloya kusajili Simba

Moses Oloya

KLABU ya Simba imeachana na kiungo mshambuliaji wa Uganda, Moses Oloya, kwa madai kuwa kanuni za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ndio kikwazo kikubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti jana Jumatatu, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe, alisema mpango wa kumsajili Oloya katika dirisha dogo la Januari umekufa kwa sababu kanuni za TFF zinataka kila klabu kuwa na wachezaji wasiozidi watatu wa kigeni kuanzia msimu ujao.
“Tayari tuna wachezaji wanne, bahati nzuri ni kwamba mwakani Abel Dhaira anamaliza mkataba wake, kwa hiyo mkataba wa Dhaira ukiisha tutabakiwa na wachezaji watatu wa kigeni,” alisema Hanspoppe.
“Hatuwezi kumsajili Oloya, wakati kuanzia msimu ujao tunatakiwa kuwa na wachezaji watatu tu wa kigeni. Kwa busara ni vyema tuachane na mpango huo ili wabaki waliopo, hatuwezi kumsajili Oloya kwa kipindi cha miezi sita tu.”
Wachezaji wa kigeni waliopo Simba ukimwondoa Dhaira (Uganda) ni Joseph Owino (pia Mganda), Amissi Tambwe na Gilbert Kaze (wote  Burundi).
Kwa muda mrefu, Hanspoppe alikuwa akiahidi kumsajili Oloya katika dirisha dogo ili kuimarisha nafasi ya kiungo mshambuliaji.
Oloya ambaye alikuwa akifukuziwa pia kwa udi na uvumba na Yanga, timu yake ya Saigon Xuan Thanh ilijitoa kwa hasira kwenye Ligi Kuu ya Vietnam na kushushwa hadi daraja la tatu mapema mwaka huu.
Hata hivyo habari za ndani kutoka Uganda zinasema kuwa Oloya aliondoka Ijumaa iliyopita kwenda Vietnam ambako amejiunga na klabu ya Binh doog FC inayoshiriki Ligi Kuu.
Katika hatua nyingine, Hanspoppe alisema kocha, Abdalla Kibadeni, amependekeza wasajiliwe wachezaji watatu tu katika dirisha dogo.
Alifafanua kuwa nafasi ambazo kocha anataka kuongeza wachezaji ni pamoja na kipa, beki wa kati mmoja na kiungo mshambuliaji.
“Nadhani nafasi ya kiungo mshambuliaji tumeipata, huyo Awadhi (Awadhi Juma Issa wa Mtibwa) anatutosha, kwa hiyo bado tuna nafasi mbili, ingawa binafsi nadhani hata nafasi ya beki wa kati kijana wetu Hassan (Khatibu) amekuwa akifanya vizuri sana,” alisema Hanspoppe.
Mwenyekiti huyo alikiri kuwa Ally Badru Ally waliyemsajili kutoka Suez Canal ya Misri hakuwapo kwenye mipango yao, lakini kwa sababu alikuwapo tu Dar es Salaam wanaamini kuwa atawasaidia katika ushambuliaji.

No comments:

Post a Comment