Thursday, 21 November 2013

Mzungu Gor Mahia ashika kiuno

Kocha wa Gor Mahia, Bobby Williamson

KWELI Wahenga walisema ‘Muosha Huoshwa’. Kocha wa Gor Mahia, Bobby Williamson, amekiri kuzidiwa maarifa na mpinzani wake wa AFC Leopards, James Nandwa, ambaye juzi Jumapili aliiongoza Ingwe kuibuka na ushindi wa bao 1-0 katika fainali ya Gotv Shield akifuta uteja wake dhidi ya mzungu huyo.
Fainali hiyo ilikuwa mechi ya tatu kuwakutanisha makocha hao baada ya mwaka jana kuvaana mara mbili wakiwa na timu za taifa. Nandwa akiingoza Harambee Stars katika michuano ya Cecafa Challenge Cup alifungwa mara mbili ikiwamo mechi fainali mbele ya Williamson aliyekuwa akiinoa Uganda. Michuano hiyo ilifanyika Kampala.
Lakini hiyo juzi Jumapili, Nandwa kama mtu mwenye hasira kali, alikipanga vyema kikosi chake mpaka mzungu akakubali na sasa amenyoosha mikono akisema kipigo hicho ni saizi yake.
“Leopards walikuja juu sana, katika mechi nzima hawakutupa nafasi japo nasi tulijitahidi. Kwa ujumla walikuwa timu tofauti kabisa na hakika viwango vyao vilimaliza,” anasema kocha huyo raia wa Scotland.
Mchezaji wa zamani wa Gor, Peter Pinchez Opiyo, anayewania tuzo ya Kiungo Bora wa mwaka, ndiye aliyewaletea mkosi mabingwa hao wa Ligi Kuu Kenya kwa bao lake la dakika ya 53.
Kabla ya mechi hiyo, Williamson alielezea hofu yake akisema alitarajia mchuano mgumu kutoka kwa Nandwa ambaye alimtaja kuwa kocha mwenye uwezo wa kupevusha timu kwa muda mfupi.
Hofu ya mzungu huyo ilionekana wazi katika mechi kwani Williamson aliamua kumpanga mshambuliaji mmoja tu, Mganda Dan Sserunkuma, huku akiwajaza wachezaji katika safu ya kati.
Japo Sserunkuma alihangaisha sana wapinzani, kukosa sapoti kwa straika wa pili ndio kuliimaliza Gor. Hali hiyo ilibadilika punde straika Patrick Kiongera alipombadilisha kiungo Antony Akumu dakika ya 60, ila ushirikiano wao mwema na Sserunkuma kwenye dakika hizo chache ulikuja kwa kuchelewa.
Kwa upande wake Nandwa aliamua kuanza na mastraika wawili Allan Wanga na Noah Wafula huku Wafula akicheza kama straika wa pili  karibu na viungo na wakati mwingine akiwa winga.
Wafula ndiye aliyechangia bao hilo kutoka kulia mwa uwanja baada ya kumlemea beki Moussa Mohamed na kuachia krosi safi iliyounganishwa na Opiyo.
Aidha Nandwa alimwanzisha kiungo mkongwe, Charles Okwemba, ambaye mara nyingi ametumiwa kama mchezaji wa akiba. Ushirikiano wake mzuri na Opiyo pamoja na usambazaji wa mpira pamoja na usukaji wa pasi uliridhisha.
Kwa ushindi wake, Leopards imenyakua kitita cha Sh2 milioni na tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho barani Afrika mwakani.

No comments:

Post a Comment