Thursday, 21 November 2013

Kapombe: Nakwambia Ulaya si mchezo

Mwili wake una mabadiliko, umeongezeka, amejengeka zaidi kimazoezi na kwenye mechi kati
ya Stars na Zimbabwe iliyochezwa juzi Jumanne na kumalizika kwa suluhu, Kapombe
 alicheza vizuri nafasi ya beki wa kulia kipindi cha kwanza na baadaye kuhamia beki wa kushoto.

KIRAKA Shomari Kapombe anayechezea Klabu ya AS Cannes ya Ufaransa ametamka kwamba amekutana na maisha tofauti sana Ulaya na sasa ni kama amezaliwa upya.
Kapombe bado hajafanikiwa, ndiyo ameanza kutafuta lakini ameonyesha dalili kwamba anaweza kufika mbali.
Ukimtazama au kuzungumza naye, utagundua kuna vitu vingi vipya kwake ambavyo ni tofauti na zamani.
Mbali na nidhamu akiwa ndani au nje ya uwanja ambayo kwake si kitu kipya, lakini anajitambua, ameimarika na anajua nini cha kufanya kwa ajili ya mafanikio yake. Ni profesheno.
Mwili wake una mabadiliko, umeongezeka, amejengeka zaidi kimazoezi na kwenye mechi kati ya Stars na Zimbabwe iliyochezwa juzi Jumanne na kumalizika kwa suluhu, Kapombe alicheza vizuri nafasi ya beki wa kulia kipindi cha kwanza na baadaye kuhamia beki wa kushoto.
Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongala alisema kwamba kiwango cha Kapombe kilikuwa juu, alionyesha mbinu na alijua kutumia nguvu.
Ongala alisema kuwa kucheza Ulaya ni zaidi ya mpira kwani mbali na kipaji ulichonacho, wanaangalia vingi na zaidi ni nidhamu.
Mwanaspoti lilizungumza kwa kina na Kapombe ambaye  alieleza kwa undani maisha aliyokutana nayo kwa kipindi chote tangu alipotua Ufaransa Agosti mwaka huu.
Anasema: “Kama unavyojua wenzetu wako mbele, wanatuzidi kila kitu, kwa hiyo unapofika huko kila kitu kinakuwa kipya. Maisha ni magumu kwa sababu kila kitu kipo juu na maisha yao ni ya kisasa tofauti na hapa kwetu.”
“Mwanzoni mazingira niliyaona magumu, kama unavyojua mambo ya ugeni, kila unachokutana nacho ni kipya. Wako makini kwa kila kitu, hakuna mzaha. Kila mtu yupo makini na jambo alilokusudia na hasa mnapokuwa mazoezini au mahali popote kulingana na wakati,” anasema Kapombe.
“Unaona mtu ana uchungu na hamu ya kutaka kujua jambo fulani na anafanya kwa umakini ili asikosee na afanikiwe, unapolegea unajiharibia mwenyewe. Ufaransa mpira ni kama  kazi nyingine, wafanyakazi wa sehemu mbalimbali wanapoamka kwenda kazini na nyinyi mnaamka kwenda mazoezini, ni kazi,” anasema Kapombe na kuweka wazi kuwa wanafanya mazoezi asubuhi tu.
Anaeleza kuwa mbali na mafunzo ya mpira, wanafundishwa na vitu vingine vingi vya nje ya soka ili kuishi kiprofesheno.

No comments:

Post a Comment