![]() |
Ronaldo |
WAKATI mwingine kila shujaa anaishi na hukumu yake ya maisha yote aliyoishi. Yupo askari aliyerusha risasi ya mwisho kwa dikteta fulani. Daima Dunia itamkumbuka kwa risasi hiyo kwa maisha yake yote.
Wengine wanaonekana wazembe na wanakumbukwa kwa uzembe wao kwa maisha yao yote duniani. Kipa wa Brazil katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1950 zilizofanyika Brazil, Moacir Barbosa, mpaka sasa hajasamehewa na wananchi wa Brazil.
Anatajwa kufungisha bao la pili la Uruguay katika mechi ya fainali. Mpaka sasa Wabrazili hawajamsamehe. Hata kaburi lake lililopo Campinas, Brazil nalo halijasamehewa. Majuzi kipa wa zamani wa Brazil, Dida, alikuwa anamuombea msamaha. Sioni kama watamsikiliza. Lakini wengine ni mashujaa na wanakumbukwa kwa ushujaa wao kwa maisha yao yote.
Zinedine Zidane wa Kombe la Dunia mwaka 1998 atakumbuka na Wafaransa kwa maisha yake yote. Ni kama Pele wa 1958 au Diego Maradona wa Mexico ya mwaka 1986.
Ni kama Cristiano Ronaldo wa Jumanne usiku jijini Stockholm kule Sweden atakavyokumbukwa maisha yake yote na Wareno. Hata kaburi lake litakumbukwa kwa miaka mingi ijayo. Popote atakapolazwa, iwe Santo Antonio au Funchal pale Madeira.
Wareno walihitaji sana kwenda Brazil. Nililiandika hili wiki chache kabla ya mechi. Unajua kwa nini? Hawa ndiyo watoto zao wakubwa miongoni mwa mataifa waliyoyatawala. Achana na Angola, Cape Verde na Msumbiji, Brazil ndiyo taifa kubwa zaidi lililotawaliwa na Ureno.
Kwa bahati mbaya, Ureno na makoloni yao yote kasoro Brazil hawajawahi kuandaa Kombe la Dunia. Wakati Brazil ilipoandaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 1950 na Barbosa kufanya kosa lisilosameheka, Ureno haikushiriki mashindano hayo.
Jumanne usiku, ilikuwa fursa yao ya mwisho kwenda Kombe la Dunia katika koloni lao. Nani anajua ni lini Kombe la Dunia litarudia tena Brazil? Hasa ukizingatia nafasi ya mwisho waliipata miaka 63 iliyopita. Walihitaji timu yao iende. Lakini zaidi walimhitaji Ronaldo kuwapeleka katika fukwe za Copacabana pengine kuliko mchezaji yeyote yule katika kikosi chao. Shujaa hapimwi katika klabu. Anapimwa katika timu ya taifa.
Ushujaa wa klabu ni rahisi kuupata kwa sababu unautumikia mshahara wako. Ushujaa wa timu ya taifa ni mgumu kwa sababu hauna malipo. Unaitumikia damu yako na ya watu wako. Unaitumikia bendera yako, unaitumikia historia yako, unaitumikia nchi yako.
Kwa Wareno, kama ilivyo duniani kote, Ronaldo anaonekana kijana mwenye kipaji, mpenda magari mazuri, malaya, anayekesha katika kioo, tajiri. Lakini ushujaa kwa watu wake ulikuwa mbali.
Jumanne usiku ameibadili historia yake. Kaburi lake halitachapwa viboko kama lile la Barbosa. Ameliingiza jina lake katika historia kama Zidane alipofanya usiku ule wa Julai 12, 1998 katika Uwanja wa Stade de France jijini Paris, Ufaransa.
Ameliingiza jina lake katika historia kama vile Maradona alivyofanya Juni 29, 1986 katika Uwanja wa Azteca. Ni kama Pele alivyofanya katika Uwanja wa Rasunda jijini Stockholm Juni 29, 1958
Ronaldo alihitajika afanye alichofanya usiku ule wa Jumanne jijini Stockholm. Kweli hakuwaangusha. Alifunga la kwanza, akafunga la pili, akafunga la tatu. Aliwaweka Waswedeni mfukoni kwake. Akawafanya alichojisikia.
Kombe la Dunia bado. Sioni kama Ureno watafanya vizuri licha ya kuwa na Ronaldo. Lakini katika historia yao, Wareno walihitaji jeshi la mtu mmoja kuwafikisha fukwe za Copacabana. Ndani ya siku nne, Ronaldo alifunga mabao manne ya kuwapeleka Copacabana.
Ronaldo na Messi hawaingizwi katika kundi la Pele, Maradona, Ronaldo de Lima, Gerd Muller na Zidane kwa sababu heshima yao ndani ya taifa iko chini. Messi anampita Maradona katika idadi ya mabao, lakini sasa anahitaji kuwa jeshi la mtu mmoja ndani ya Brazil miezi saba ijayo.
Kama Ronaldo anaweza kufanya kitu zaidi katika fainali za Maracana msimu ujao atakuwa zaidi ya Maradona. Kikosi chake hakina mastaa wa kumwezesha kufanya jambo la maana Brazil. Amezungukwa na mastaa wa kawaida.
Ni kama ilivyokuwa kwa Maradona. Lakini Maradona alitoa maajabu. Hata hivyo hadi alipofika inatosha kumwingiza Ronaldo katika kundi la Luis Figo na Eusebio ambao katika mitaa ya Lisbon, Ureno wanaonekana kama miungu watu.
Ronaldo alikuwa anaonekana kama mvaa hereni mwenye maringo anayetisha Santiago Bernabeu. Amefanikiwa kuvuka mtihani huu akiwa na kitambaa chao begani. Kwa lolote atakalofanya ataonekana shujaa. Hata kama akifanya ujinga, kaburi lake litasamehewa.
Ni kama unavyomwona Maradona. Anavuta bangi, anakula unga, anafanya vurugu za kila aina, lakini Waargentina walishamsamehe kwa mambo aliyowafanyia. Hata akifa, kaburi lake lilishasamehewa kutokana na usiku ule wa Azteca Mexico.
Ni kama usiku wa Stockholm ulivyosababisha Wareno wamsamehe Ronaldo. Kwa lolote baya litakalotokea mbele, tayari ameshaingia katika vitabu vyao.
No comments:
Post a Comment