Saturday, 23 November 2013

SAMATTA,ULIMWENGU RUKSA KUTESA CHALLENGE




KLABU ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, imewaruhusu Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta kuichezea Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Chalenji.
Wakati kukiwa na uhakika wa kuwatumia wachezaji hao, Kocha wa Kili Stars, Kim Poulsen amesema anataka kufika mapema Kenya ili kuzoea hali ya uwanja.
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Boniface Wambura ameliambia Mwanaspoti kuwa, walikubaliana na Mazembe kuwatumia Samatta na Ulimwengu baada ya kucheza mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia.
“Tumekubaliana na Mazembe kwamba watawaruhusu Samatta na Ulimwengu waje kucheza Chalenji baada ya mechi yao ya fainali Novemba 30, hivyo ndivyo tulivyokubaliana kama kuna mabadiliko tutajua baadaye,” alisema Wambura.
Kwa upande wake, Poulsen alisema keshokutwa Jumatatu timu yake itaondoka kwenda Kenya ili kuzoea hali ya hewa na uwanja.
“Tunaondoka Jumatatu, unajua hapa tunafanya mazoezi katika nyasi bandia na kule tunaweza kucheza mechi zetu katika nyasi za asili, kwa hali hiyo tunapaswa kuwahi na kufanya mazoezi katika uwanja wa aina hiyo ili tuendane na mazingira,” alisema Poulsen raia wa Denmark.
Katika michuano hiyo mwaka jana nchini Uganda, Mazembe iliwazuia wachezaji hao kuichezea Kili Stars licha ya kuahidi kwamba ingewapa ruhusa.
Kilimanjaro Stars ipo katika Kundi B la michuano hiyo lenye timu za Zambia, Burundi na Somalia, itacheza mechi yake ya kwanza dhidi ya Zambia, Novemba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa Machakos.
Mechi nyingine za Kilimanjaro Stars ni dhidi ya Somalia Desemba Mosi (Nyayo) na ile ya mwisho dhidi ya Burundi itachezwa Desemba 4 kwenye Uwanja wa Nyayo

No comments:

Post a Comment