![]() |
Raia wa Croatia Zdravok Logarusic aliyetangazwa na Simba kuwa kocha mkuu wa timu hiyo akichukua mikoba ya Abdallar King Kibadeni. Picha na Maktaba |
Mwandishi: Ni lini umeanza kuijua Simba?
Kocha: Nilianza kufuatilia Ligi Kuu Tanzania Bara nikiwa na Gor Mahia ya Kenya. Hapo ndio nilijua kuwa Simba ni timu kubwa, yenye historia ndefu, ina mashabiki wengi, lakini pia yenye presha nyingi ndani na nje ya uwanja.
Uzuri wake ni kwamba ninafurahia kufanya kazi zenye presha.
Ninajua mashabiki wa Simba wanataka kuona klabu yao ikifanya vizuri ndani na nje ya Tanzania.
Mwandishi: Je unamfahamu mchezaji yeyote wa Simba?
Kocha: Simfahamu mchezaji yeyote wa Simba, na hiyo ni nzuri kwangu. Kama mchezaji anataka nimfahamu au nimkumbuke jina lake anapaswa kufanya vitu uwanjani (azungumze kwa vitendo uwanjani), sitaki kumjua mchezaji kupitia vyombo vya habari, nataka nimjue mchezaji kutokana na kazi yake uwanjani.
Simba ina wachezaji 36, kwa hiyo kila mchezaji anatakiwa kufanya bidii kubwa uwanjani ili nimfahamu jina lake, majina hayachezi uwanjani, wanaocheza ni wachezaji.
Mwandishi: Nini kitakuwa kipaumbele chako Simba?
Kocha: Rahisi sana. Ni kuleta mataji na vikombe Simba. Haitakuwa kazi rahisi, lakini mashabiki wetu wanataka hivyo na sisi tutajitahidi kuwafanya mashabiki wafurahi.
Mwandishi: Una ahadi gani kwa mashabiki wa Simba?
Kocha: Ahadi yangu kwa mashabiki wa Simba ni kwamba benchi la ufundi pamoja na wachezaji tutajituma na kujitolea kwa nguvu zetu zote mazoezini na katika mechi kwa asilimia 150. Kujituma kwa nguvu ndio kutatupa matokeo mazuri, hakutakuwa na masihara.
Mwandishi: Mashabiki watarajie nini kutoka kwako?
Kocha: Inabidi nionyeshe vitendo uwanjani, na matokeo ya uwanjani yatazungumza kwa niaba yangu.
Mwandishi: Umewahi kusikia lolote kuhusu wapinzani wa Simba wanaitwa Yanga?
Kocha: Katika mechi za watani wa jadi kwa Afrika, Simba na Yanga zipo katika tatu bora katika mechi za wapinzani wa jadi. Hizo ni mechi spesho na zina hisia za kipekee. Ninataka kuwa sehemu ya watu waliomo kwenye mechi hizo, nitafurahi sana.
Mwandishi: Umekuwapo Afrika kwa muda mrefu, una maoni gani kuhusu soka la Afrika?
Kocha: Soka la Afrika linapiga hatua kila saa, kila siku, kila wiki, na ninafurahi kwa sababu na mimi ni sehemu ya maendeleo hayo. Lakini Afrika inaweza kufanya vizuri zaidi ya hapo.
Kama nchi yangu ya Croatia ina watu milioni nne tu, katika fainali tano za Kombe la Dunia zilizopita imeshiriki mara nne na tangu mwaka 1998 mpaka 2012 imekuwa katika kumi bora katika viwango vya Fifa duniani, ni kwanini Afrika isifanye hivyo?
Kwa maoni yangu katika viwango vya Fifa vya dunia, Afrika ilipaswa kuwa na nchi mbili katika kumi bora, na katika 20 bora kungekuwa na angalau nchi tano za Afrika, lakini sasa ni Ivory Coast tu ambayo ipo katika 20 bora (wapo nafasi ya 17).
Sisi sote lazima tufanye kazi pamoja kwa lengo la kuendeleza soka la Afrika.
No comments:
Post a Comment