Harona Niyonzima |
WAKATI watu kama, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu, Amis Tambwe, Abel Dhaira na Kipre Tchetche wanalipwa mishahara ya zaidi ya Sh 2 milioni kwa mwezi kila mmoja, mchezaji ghali wa Ashanti United analipwa Sh.200,000.
Hiyo ina maana kwamba mshahara wa Niyonzima pekee yake, unaweza kulipa wachezaji 11 wa kikosi cha kwanza cha Ashanti United ambacho kinaanza mechi yoyote.
Mshahara wa Sh 200,000 ambao analipwa mchezaji wa juu wa Ashanti ni sawa ya bei ya kiatu ambacho anavaa uwanjani Ngassa, Kavumbagu, Niyonzima, Amis Tambwe au John Bocco.
Si hilo tu, Ashanti inatumia Sh 8.5 milioni kulipa mishahara ya wachezaji na viongozi kila mwezi.
Katibu wa Ashanti United, Aboubakary Silas alilifahamisha Mwanaspoti kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi anapata Sh. 200,000 za Kitanzania na posho ya Sh.5,000 kila siku mara baada ya mazoezi.
“Hatuna fedha za kulipa mishahara mikubwa, tunajitahidi angalau kuwapa posho kila baada ya mazoezi pamoja na kuwagharimia huduma za afya, maji na hata kulipia kambi siku moja au mbili kabla ya kucheza mechi,” alisema Silas na kufafanua kuwa wana wachezaji sita wanaosoma elimu ya juu kwa sasa kwenye kikosi hicho.
Wachezaji hao ni Roland Nasis, Ibrahim Himid, Shabani, Wambong Mkongo (wote Chuo cha Elimu ya Biashara ‘CBE’), Imam Ali (Chuo cha Usimamizi wa Fedha ‘IFM’) na Hussein Mohamed (anayesoma Chuo cha Uhasibu Dar es Salaam ‘DSA’).
“Unapokuwa na wachezaji wasomi inasaidia wachezaji wengine kujua ni mambo gani mazuri na yapi mabaya kwa kuwa mfano mzuri kwa wenzao.”
Naye mchezaji wa zamani wa Simba Boniface Pawasa ambaye ana elimu ya diploma ya masoko alisema: “Bila elimu maisha yangu yangekuwa magumu hasa baada ya soka. Niliamua kurudi darasani ili niishi vizuri kwenye dunia ya sasa yenye kuendeshwa na wasomi.”
Pawasa pia alizitaka timu kubadili programu zao ili kutoa fursa kwa wachezaji kusoma na kujiendeleza kwenye mambo yao binafsi huku akiwasisitizia wachezaji nao kutambua kuwa soka lina mwisho.
No comments:
Post a Comment