Kocha wa ArsenalArsene Wenger. |
NI miaka 17 imepita Arsenal tangu Arsene Wenger alipotua jijini London akitokea Japan na kuanza maisha mapya ya soka na Ligi Kuu England.
Hadi sasa, Mfaransa huyo amebakia wa pekee kati ya makocha wengine 19 wa ligi hiyo akiwa ameishi na kufanya kazi kwenye klabu moja pekee kwa kipindi kirefu.
Jumamosi, Septemba 28, alitimiza miaka 17 kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Swansea City. Ni mambo gani ya kukumbukwa kwake?
1- Wasioshindika ‘The Invincibles’. Kikosi chake cha msimu wa 2003-04 ni kumbukumbu ambayo wacheza sinema wa Disney wameamua kukitengenezea filamu. Ni kikosi ambacho kilimaliza msimu bila kupoteza mechi, pia kutwaa ubingwa.
2- Henry. Aliyemtengeneza Thierry Henry kutoka winga asiye na sifa hadi kuwa mshambuliaji mahiri. Wenger alimwokoa Henry kutoka benchi la Juventus na kumbadili uchezaji wake, alimfanya shujaa wa klabu kwa mabao 228. Henry ameingia kwenye orodha ya washambuliaji mahiri duniani
3- Msimamo. Huwezi kumlaumu Wenger kwa woga mbele ya vyombo vya habari. Ni mtu ambaye wakati mwingine amekuwa akichekesha. Alipoulizwa kuhusu kupoteza wachezaji wengi nyota alijibu: “Jiulize, kama umeamua kuwa na uhusiano na msichana, ghafla unabaini anaye mwanamume mwingine unafanyaje. Huwezi kujinyoga.”
4- Umoja. Aliweza kuunda safu imara ya kiungo ya Emmanuel Petit na Patrick Vieira. Wawili hao walimlipa kwa kumpa mataji.
5- Koti lake refu. Ni kitambulisho chake kwa wengi hasa nyakati za baridi ambako koti hilo refu linalofikia magotini halikosi daima. Wakati fulani kamera za wapigapicha zilimwonyesha akishindana nalo lilipoharibika zipu, Desemba mwaka jana.
6- Jicho lake. Kwa muda mrefu, Wenger alikana kukosa mtazamo. Amekuwa mwepesi wa kuwatetea nyota wake kama alivyofanya wakati ule Patrick Vieira alipomwangusha adui uwanjani.
7- Mara kadhaa amegoma kuingia katika mzozo wa kununua wachezaji wa bei mbaya wakati wa usajili na badala yake amewekeza kwenye vijana. Msimu huu, kwa miaka 17,Wenger ametoa Pauni 42.5 kumsajili Mesut Ozil!
8- Hasira. Alionyesha kukasirika baada ya kutolewa nje na mwamuzi Mike Dean katika mchezo dhidi ya Man United kwenye Uwanja wa Old Trafford mwaka 2009 baada ya kupiga teke chupa ya maji. Alisimama kwenye ukuta na kushika kiuno mbele ya mashabiki.
9- Robert Pires. Ni mtu aliyekuwa na miguu ya ajabu. Kiungo ambaye hata hivyo alipiga penalti ya ajabu ambayo imeacha simulizi iliyofunika mafanikio yake Arsenal.
10- Ugomvi. Tukio la kukwaruzana na aliyekuwa kocha wa Man United, Sir Alex Ferguson. Ni upinzani mkubwa baina ya wawili hao. Upinzani wao ulitosha kukoleza utamu wa Ligi Kuu: Wawili hao wanakumbukwa kwa upinzani wa muda mrefu.
11- Bei poa. Ni kwenye ununuzi wa Nicolas Anelka, Patrick Vieira na Freddie Ljungberg ambao waliipa mafanikio klabu yake licha ya kununuliwa kwa bei karibu na bure.
12- Wageni pekee. Ni kocha aliyewahi kuchezesha wageni pekee kwenye Ligi Kuu England, ambaye baadaye aligeukia wazawa, Jack Wilshere, Alex Oxlaide-Chamberlain na Theo Walcott ambao amewakuza.
13- Furaha. Tukio la furaha kwake ni safari wakati wa likizo yake ambako aliwahi kuteleza na kuanguka kwenye boti.
14- Mlezi. Alifanikiwa kumlea na kumtengeneza kiungo Cesc Fabregas kuwa mmoja wa viungo bora duniani, ambaye alimshuhudia akihamia Barcelona.
15- Usajili wa Robin Van Persie. Ni ajabu kuona kwamba alimnasa kwa bei ndogo, akaishi naye akiwa majeruhi, akarejea na kuipa ubingwa Man United mwaka jana.
16- Mavazi. Siku zote ni suti, lakini yenye tai nyekundu. Siku zote akiwa benchi hakosi vazi lile ambalo unaweza kudhani halibadiliki.
17- Daima. Unaweza kusema ni mtaalamu wa 1-0 kwa Arsenal. Amefanikiwa kuingiza staili kwenye klabu hiyo ambayo ni vigumu kwa klabu nyingine kuiga.
No comments:
Post a Comment