BARCELONA, HISPANIA
KIUNGO, Deco, alicheza na Andres Iniesta na kwa matamshi yake akasema Mhispaniola huyo anastahili tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia.
KIUNGO, Deco, alicheza na Andres Iniesta na kwa matamshi yake akasema Mhispaniola huyo anastahili tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia.
Lakini haijawahi kutokea. Mara zote alizoingia kwenye king’anyang’iro hicho, aliishia tu kuwa nyuma ya ama Lionel Messi au Mhispaniola mwenzake, Xavi au Mreno Cristiano Ronaldo.
Lakini, kiungo wa zamani wa Ureno mwenye asili ya Brazil, Deco, anaamini staa huyo alistahili au anastahili kupewa tuzo hiyo la basi kutokuwa na bahati ndicho kitu kinachomponza na si kukosa uwezo.
“Unapomzungumzia Iniesta nadhani kuna mchezaji mmoja tu mwingine unayeweza kumlinganisha naye, Zinedine Zidane,”anasema Deco.
“Jamaa anajua sana. Usione kile kinachotokea uwanjani, Messi anatajwa tu na vyombo vya habari kutokana na vitu vichache anavyovifanya, lakini yule Iniesta ni hatari sana.”
Bahati mbaya ya Iniesta ni kwamba anacheza soka lake la ubora mkubwa katika kipindi ambacho wanacheza Messi na Ronaldo, wachezaji ambao tayari wamejijengea kambi ya mashabiki na wanapendwa.
Ni mapenzi tu ya watu kwa Messi na Ronaldo ndicho kitu kinachomfanya Iniesta asionekane, lakini si kwa soka la ndani ya uwanja. Staa huyo ndiye anayemfanya Messi kuwa bora pale Barcelona na Xavi kutakata kwa pasi nyingi Barcelona na La Roja.
Iniesta ana kila sababu ya kuthaminika kwa ubora wake. Mafanikio yote iliyopata Hispania kwenye michuano mikubwa kwa miaka ya hivi karibuni yametokana na ujuzi wake. Aliifanya Hispania kunyakua ubingwa wa Ulaya baada ya kuwang’arisha katika fainali za Euro 2012 na zile za 2008. Wakati La Roja inanyakua taji la ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 2010 kule Afrika Kusini, kiungo huyo ndiye aliyefunga bao la ushindi kwenye fainali dhidi ya Uholanzi. Ni watu wachache wanaotoka nyumbani kwenda kumtazama Iniesta ndani ya uwanjani, lakini utundu wake na umahiri wa kuuchezea mpira umekuwa burudani tosha kutokana na kipaji alichonacho.
Unapozungumzia ufundi wa kweli, basi kwenye Barcelona huwezi kumtaja Xavi ambaye sifa yake kubwa ni moja tu kupiga pasi, au Messi ambaye amekuwa akivunja rekodi za kufunga. Lakini ukihitaji soka lenye burudani na kiwango kikubwa, Iniesta anakata kiu.
Picha zinazungumza kuliko maneno
Ushawahi kujiuliza kwanini Barcelona au Hispania inashinda kirahisi? Kupata jibu la swali lako, subiri Iniesta anapokuwa uwanjani, halafu mfuatilie anapokuwa na mpira kitu gani kinafanyika.
Achana na uwezo wake wa kupiga chenga na pasi hatari za mwisho, staa huyo ana kitu ambacho wachezaji wengi wa Dunia ya sasa hawana. Iniesta ni kama sumaku, anapokuwa na mpira anawatamanisha wachezaji wa timu pinzani kumfuata, anawajaza wengi, wanakuwa wafuasi wake na kisha anafanya maamuzi yanayowafanya wajilaumu baadaye. Kitu hicho ndicho kinachomfanya Deco aamini katika ubora wa Iniesta. Hiyo ndiyo sifa ya Iniesta, atakutamanisha na mpira wake umfuate ukauchukue, atakuja mchezaji moja, atakuja mwingine, mwingine tena hadi akiona karibu nusu ya timu yote ipo kwake, anatoa pasi ya hatari inayowapa sifa akina Messi
Tishio la uwanjani
Kwenye El Clasico ya Jumamosi iliyopita, hakuwa na kazi kubwa katikati ya dimba. Alikuwa akitembea tu na kupika bao la kwanza lililofungwa na Mbrazili Neymar.
Lakini kuonyesha kwamba Iniesta ni hatari pengine kuliko mchezaji yeyote kwenye kikosi cha Barcelona au Hispania, tazama wachezaji wa timu pinzani wanavyohangaika kumzuia, wanaamini unapoweza kumdhibiti mchezaji huyo basi utakuwa umemaliza kazi.
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba ni nadra kumwona Iniesta akicheza chini ya kiwango na si kazi rahisi kutimiza lengo lako la kumdhibiti na ndiyo maana wachezaji wengi wa timu pinzani wamekuwa wakijaa kwake kutaka kumzuia na kutoa nafasi kubwa ya kuadhibiwa na watu wengine.
Xavi na Iniesta nani mkali
Kuna tofauti kubwa ya uchezaji wao japo wote ni viungo. Xavi ni mara chache kuona akikimbia na mpira, amekuwa na sifa ya kupiga pasi nyingi, lakini anafanya hivyo akiwa amesimama. Uchezaji wa Xavi unafanana na wa Michael Carrick. Lakini, tofauti ya Iniesta ni kwamba ukiacha uhodari wa kupiga pasi za mwisho, anapokuwana mpira anajaribu kuipangua ngome ya timu pinzani kutengeneza nafasi za mabao. Mpira unapokuwa kwenye miguu yake anauagiza anavyotaka sawa na ilivyokuwa enzi za Zidane alipokuwa ndani ya uwanja.
No comments:
Post a Comment