Wednesday, 30 October 2013

WENGER KADHAMIRIA KWENDA NA WAKATI

Mageuzi ya soka ni jambo muhimu katika kila klabu inayotaka kwenda na wakati.
Lazima pawepo tafakari nyingi, ubunifu wa hali ya juu ya uingizaji mitaji kwa ajili ya kupata kikosi bora zaidi na pia kukipa nguvu siku hadi siku.
Falsafa hiyo bado haiingii akilini mwa baadhi ya watu wa soka, lakini ni wazi hao wataachwa nyuma kwani uhafidhina kwenye soka haukubaliki tena. Nikiwa mmoja wa wakazi wa London Kaskazini kitambo sasa, nimekuwa kwa namna ya pekee nafuatilia klabu ya Arsenal, ambayo tangu mwaka 1996 imekuwa chini ya kocha Mfaransa, Arsene Wenger.
Kocha huyu mwenye shahada ya uchumi aliyetangulia kuzifundisha timu za AS Nancy, AS Monaco na Nagoya Grampus kwa muda mrefu, amekuwa akipinga matumizi ya fedha nyingi kwenye usajili.
Anaungana na dhana ya kwamba klabu nzuri hujengwa kwa timu yake kukusanya wachezaji tangu wakiwa vijana na kuwapika vilivyo ili kuepusha matumizi ya fedha nyingi, pia wachezaji kuzoeana kwa muda mrefu.
Hata hivyo, siku hizi mambo mengi yamebadilika; utandawazi umeingia kwenye soka ambapo matajiri waliokuwa kwenye biashara nyingine wamejitumbukiza katika mchezo huo.
Hawa wamebadili kwa kiasi kikubwa mwelekeo ambapo wenyewe au kwa kutumia mawakala huweza kuchomoa wachezaji wazuri kwenye timu kwa kitita wanachoamua, hata kiwe kikubwa kiasi gani.
Ndiyo maana lsiku hizi kuna mjadala mkali juu ya uhalali wa bei ya Gareth Bale ya zaidi ya Pauni milioni 83.
Wenger alikuwa muumini wa siasa za mpira za kugawana ‘kisungura’ kidogo kwenye ada za uhamisho.
Pengine alichota mawazo hayo kwenye masomo yake ya uchumi na menejimenti na kwa kiasi kikubwa ameifanikishia makubwa Arsenal, ikiwa ni pamoja na kuizalishia faida kubwa na kujenga uwanja wa pili kwa ukubwa Uingereza.
Hata hivyo, falsafa yake imesababisha ‘ukame’ wa vikombe katika miaka saba iliyopita, japokuwa ukiwianisha jumla ya vikombe alivyowapatia Arsenal na muda aliokaa (ubingwa mara 13 na Kombe la FA mara 10), amewapandisha sana. Lakini kuna usemi  ‘Mla ni mla leo, mla jana kala nini?’ mashabiki wanataka mataji sasa, wala huwaambii kitu kwa idadi ya makombe aliyoleta Highbury na sasa Emirates tangu 1996 wala kwa uwanja aliojenga na gawio la faida alilopeleka kwa wamiliki.
Kidogo kidogo Wenger anaonekana kuondoka kwenye makucha ya nadharia yake ya kihafidhina hivyo kwamba ukiwaona Arsenal wanacheza sasa unafurahi.
Japokuwa msimu wa jana hawakuvuka sana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya na majuzi wamefungwa na Borussia Dortmund, lakini wanaonyesha soka ya uhakika.
Labda matajiri wale waliomvurugia mpango wa kukuza vijana na kuwatumia kuleta mataji Arsenal, ndio wamemfanya abadilike, lakini pia yawezekana kutimiza kipaumbele chake kama uwanja na faida nono kwa wamiliki kumechangia.
Baada ya nyota wake, wakiwamo manahodha kuondoka kila majira ya kiangazi, anaonekana limemfika kooni na anabadili mbinu zake.
Aliumia mno kuondokewa na manahodha wake, Cesc Fabregas na Robin van Persie, waliokuwa bora dimbani pia, lakini wengine walioikimbia Arsenal ni akina Mathieu Flamini aliyerejea sasa, Gael Clichy, Samir Nasri, Emmanuel Adebayor, Kolo Toure, Ashley Cole na wengineo.  Wanapoondoka halafu wanatesa waliko, wanakuja Emirates na kuwafunga Arsenal au kuwatesa, inaumiza sana kwa kocha na wadau.
Nilitazama kwa makini mechi kati ya Arsenal na Napoli na hungeweza kuamini wale ni Napoli waliochezewa kama watoto, wakabandikwa bao mbili bila majibu na kukoswakoswa mengine zaidi.
Lakini hata kabla mechi ya mwisho dhidi ya Bayern Munich msimu uliopita kule Allinz Arena, Ujerumani, Arsenal ilishinda hivyo hivyo, wakionesha soka safi, lakini walishachelewa na ilikuwa kasoro bao moja tu wavuke.
Hadi naandika makala haya, Arsenal inaongoza Ligi Kuu  England na iko pointi sawa na Dortmund pia katika Ligi ya Mabingwa Ulaya wakiongoza kundi lao.
Hiyo si bahati mbaya, inabadilika, ilianza kujengwa zaidi kwa kuvunja benki na kuwasajili akina Lukas Podolski, Olivier Giroud, Santi Cazorla na labda tumtaje pia Per Metersacker.
Katika kipindi kama hiki cha msimu, Arsenal huwa nafasi ya tatu au ya nne katika misimu saba iliyopita.
Siku ya mwisho ya dirisha la usajili msimu huu, Wenger alimnunua Mesut Ozil wa Real Madrid kwa Pauni milioni 43 ambazo hazikupata kununua mchezaji mmoja hapo Arsenal. Alitaka pia kuwachukua akina Angel Di Maria na Karim Benzema akitenga kitita cha jumla ya Pauni milioni 70. Amerudisha chenji kwa wenyewe.
Hiyo ilikuwa baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Aston Villa katika mechi ya kwanza ya ligi msimu huu iliyotaka kusababisha msambaratiko Emirates.
Wenger aliweka jitihada hadi kumsajili, akionekana kubadilika kutoka mtu anayetaka kuendelea kuisaidia klabu isiwe na madeni mengi akasahau kwamba mashabiki hawangemwelewa (japo wamebaki naye miaka saba bila kikombe).
Sasa Wenger anaonekana shujaa tena. Nakumbuka alivyowanunua Clichy na Van Persie kwa fedha isiyozidi dola milioni tano, amewauza ghali kama wengine na fedha ziliwekezwa badala ya kununua wachezaji nyota. Hakuamini katika dhana hiyo, falsafa yake ilikataa.
Nilizungumza na majeruhi, Aboud Diaby majuzi, akaniambia maisha ya ‘kufunga mkanda’ yanaelekea kuwa historia Arsenal baada ya Wenger kukubali mageuzi ya soka na ukweli wa mambo ‘sokoni’.
Fedha za mauzo ya wachezaji sasa zitatumiwa kununua wengine, sio kama zile dola milioni 35 za Van Persie, $26 milioni za Toure na nyinginezo zilivyotupwa kabatini.
Sasa Wenger anaonekana kwenda kinyume kabisa cha yale aliyoyajenga miaka 17  bila shaka kutokana na kujifunza, maana soka nao ni mpira wa makosa.
Kutumia dola milioni 84 kuwasajili Podolski, Giroud na wengine wawili kulifanya watu kupandisha kope, wakasema pundamilia anafutwa miraba yake na juzi amesema anachotaka ni kuwafurahisha washabiki wa Arsenal.

No comments:

Post a Comment