Alex Ferguson |
MANCHESTER, ENGLAND
MANCHESTER United hali imekuwa mbaya. Lakini, kocha wa zamani wa kikosi hicho, Sir Alex Ferguson bado hajaondoa turufu yake kwa David Moyes kwamba ataiweka sawa timu hiyo, huku akisisitiza kwamba hafikirii kurejea kuinoa timu hiyo ya Old Trafford.
Wataalamu wa masuala ya soka walikuwa wakimpigia upatu mkongwe huyo arejee kunusuru mambo Manchester United baada ya sasa kupoteza mechi tatu kati ya sita za mwanzo kwenye Ligi Kuu England na kushika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi hiyo.
Katika mahojiano na televisheni moja ya nchini Marekani, Mskochi Ferguson alisema suala la kurejea kwenye kiti cha ukocha wa Manchester United hilo haliwezi kutokea.
“Sivutiwi na kuwa kocha tena au kujihusisha na matokeo ya Manchester United kwa sasa,” alisema Ferguson.
“Manchester United ipo kwenye mikono salama ya David Moyes. Atakuwa salama tu, yeye ni kocha mahiri. Utapoteza pesa zako tu kwa kupiga kampeni za kutaka nirudi kuwa kocha.
Ferguson aliongeza: “Nimefanya uamuzi. Muda huu ndiyo sahihi. Haiwezekani kwangu mimi kurejea kwenye ukocha. Nimeanza maisha mapya kwa sasa.
Nataka kwenda kutazama Kentucky Derby na US Masters, Melbourne Cup. Nataka kutembelea Tuscany na Ufaransa.”
Kwenye mahojiano hayo na Charlie Rose, Ferguson alibainisha kwamba alifuatwa na bilionea mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich kumwomba aende akainoa timu hiyo ya Stamford Bridge.
“Walituma wakala wao aje kuzungumza na mimi pindi Abramovich alipoinunua Chelsea kwa mara ya kwanza,” alisema Ferguson na kuongoza:
“Niliwajibu hakuna kitu kama hicho.” Ferguson pia aliibua upya sakata la straika Wayne Rooney baada ya kusisitiza kwamba fowadi huyo alimfuata na kuomba kuhama Manchester United siku moja baada ya klabu hiyo kunyakua ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Hata hivyo, alisema amefurahishwa na namna straika huyo alivyobadili msimamo wake na kucheza kwa kiwango kikubwa katika kikosi hicho cha Manchester United kwa sasa.
No comments:
Post a Comment