Hapines Watimanywa |
WAKATI mshindi wa jumla wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka 2011 wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (Taswa) Shomari Kapombe akizaliwa mwaka 1994, katika kijiji cha Kishozi, Kagera alizaliwa mtoto wa kike ambaye hakudhaniwa iwapo siku moja angefika mbali kimtazamo, kiakili, kifikra na katika masuala ya ulimbwende.
Mtoto huyu alipewa jina la Biera lenye uhalisia wa kabila la Wahaya na baba yake ambaye alifariki baada ya yeye kutimiza umri wa mwaka mmoja. Alianza kulelewa na mama yake Amina Bukoko katika mji wa Tabora wakati huo mama yake akiwa na umri wa miaka 21 tu.
Huyu ni Happiness Watimanywa aliyetawazwa kuwa Miss Tanzania Septemba 21, mwaka huu akiwa na umri wa miaka 19.
Mwanaspoti lilimtafuta mrembo huyu na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo...
Mwanaspoti lilimtafuta mrembo huyu na kufanya mahojiano naye kama ifuatavyo...
Mwanaspoti: Wewe ni msomi na mrembo, unadhani urembo hasa ni nini?
Happiness: Kama unataka kuwa mrembo si lazima uvutie tu machoni mwa watu, kuna vitu vingi. Kwanza unapaswa kuwa mrembo wa umbo na sura hata hivyo uwe na vigezo vyote kwa kuitwa mrembo. Pili ni tabia, unapaswa kuwa mrembo wa roho na nafsi (inner beauty) huwezi kuwa mrembo kisha ukafanya vitu vilivyo tofauti na urembo wako. Pia vilevile uweze kutambua udhaifu ulionao na kuurekebisha.
Mwanaspoti: Ni makosa gani ambayo unahisi yalifanywa na warembo waliowahi kutwaa taji la Miss Tanzania na umejipanga vipi kuyarekebisha na matarajio yako ni nini katika kuibadili sekta ya urembo nchini?
Happiness: Sidhani kama kuna makosa yaliyofanywa na warembo waliopita, ila kuna baadhi ya vitu ambavyo Watanzania wanasahau kwamba mrembo naye ni binadamu. Kuna vitu atavifanya ambavyo huenda vinaweza kuonekana kuwa na utofauti, ni kama binadamu wa aina nyingine. Lakini kikubwa ni kutekeleza masuala ya kijamii na yeye mwenyewe anavyoishi katika jamii. Kujijengea uwezo wa kufikiri ni nini utaifanyia jamii, si kuishia kuvaa taji ila ni zaidi ya ulimbwende.
Mwanaspoti: Umewahi kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini na je umejipanga vipi katika kuhamasisha utalii wa ndani?
Happiness: Nina mipango mingi na mizuri kuhusu hilo. Kwanza mimi nimekuwa mtalii mzuri na nilianza utalii wa ndani nikiwa mdogo kabla sijaingia katika masuala ya ulimbwende. Nimewahi kutembelea Mikumi, Serengeti, Manyara na nimewahi kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro. Nilikwea mlima huo mwaka 2011 na kufanikiwa kufika katika kilele cha Uhuru, nikiwa huko nilishuhudia mambo mengi sana na nilipata uzoefu mkubwa. Nimewahi kushuhudia mengi na Tanzania imebarikiwa vitu vingi. Nimeshawahi kuona simba anapanda mti nadhani ni uzoefu tosha, nimepanga kuhamasisha utalii wa ndani na kukaribisha wageni kutembelea nchi yetu.
Mwanaspoti: Ukiwa Miss Tanzania 2013, pia ulililetea sifa taifa kwa kuongoza katika somo la Uhasibu kati ya nchi 150, hebu tuambie ilikuwaje na vipi bado unaendelea na somo hilo?
Happiness: Nilikuwa nikilipenda somo la Uhasibu tangu nikiwa kidato cha kwanza licha ya kufanya vizuri katika somo la hisabati tangu shule ya msingi. Kwanza tulikuwa na mitihani ya IGCSE; mitihani hii tuliifanya kawaida sana ila kwa kuwa nilikuwa mdadisi sana hasa nisipomwelewa mwalimu wangu ilinisaidia kuweza kufanya vizuri. Hata hivyo alama zangu darasani zilikuwa ni kuanzia 90 mpaka 100 sikushuka chini ya hapo.
Nakumbuka niliitwa katika shule niliyokuwa nikisoma St Costantine International School, Arusha wakati wa mahafali ya kidato cha nne na kupewa habari hiyo njema, nilifurahi sana. Mtihani niliufanya mwaka 2009 na majibu nilipewa 2010. Lakini kidato cha tano na sita nilisoma masomo yaliyo nje ya mchepuo yaani Jiografia, Historia na Uhasibu, sikuhitaji masomo ya mchepuo.
Mwanaspoti: Kwa nini hukuhitaji mchepuo na je kwa sasa unasoma wapi na unaendeleaje kimasomo?
Happiness: Kama sipendi kitu sikiweki moyoni na siwezi kulazimishwa nifanye kitu ambacho naona kwangu hakina manufaa. Hata nikifanya hakitakuwa na matokeo mazuri, niliwaambia wazazi na walimu na nashukuru walinielewa. Masomo haya niliyasoma pale Chuo Kikuu cha London na sasa ninasoma Chuo Kikuu cha Strathelyde kilichopo Glasgow huko Scotland, Uingereza. Nikisomea shahada ya biashara na sasa nipo likizo, nitaendelea na masomo siku za hivi karibuni.
Mwanaspoti: Licha ya kwamba upo Uingereza kimasomo nasikia wewe pia ni mwalimu, imekuwaje ukaamua kuacha fani ya ualimu na kuwa mlimbwende, nini hatima yako kimasomo?
Happiness: Ha ha ha ha ndiyo! Mimi ni mwalimu na kwa miezi kadhaa nikiwa likizo nimekuwa nikifundisha katika shule za Morogoro International School na Forest Secondary School. Masomo nitaendelea nayo na nitaweza kufanya vyote kwa wakati mmoja, ni mipango tu. Kuhusu suala la ulimbwende napenda kuwa mrembo, nilijua ipo siku nitashiriki. Nilifikia uamuzi huu nikiwa likizo Dodoma kwa bibi mzaa mama, niliamua kushiriki ngazi za vitongoji, nashukuru Mungu nilifanikiwa mpaka kufika katika kambi ya Miss Tanzania pale Girrafe Hoteli. Dar es Salaam.
Mwanaspoti: Ukiwa kambini uliishije na wenzako, pia ilikuwaje baada ya ushindi hawakuonekana kuwa na kinyongo na hata kukuzungumzia vibaya kwenye vyombo vya habari?
Happiness: Upendo ndiyo silaha yangu daima. Niliishi vizuri na wenzangu na hata waandaaji walikuwa wakisema warembo wa mwaka huu walikuwa tofauti na wa miaka iliyopita. Tulikuwa kama marafiki, tuliungana na kushikamana na kusaidiana. Nikiwa kambini nilijitahidi kut afuta marafiki na nilikuwa na mipango sahihi, niliweza kuwasaidia wengine na hata pale walipohisi nimewazidi kitu fulani niliwapa moyo na kuwasaidia katika vitu mbalimbali. Wapo walionizidi pia katika mambo mengine nilijitahidi kuwa nao karibu ili kuelekezwa zaidi na hivi ndivyo ilivyokuwa kila mmoja aliondoka na mengi kutoka kwa wenzake.
Mwanaspoti: Ulikuwa mwiba kwa wenzio unadhani sababu ni upeo mkubwa ulionao?
Happiness: Nadhani kwa kuwa nilikuwa mshiriki wa kwanza kuingia nusu fainali ya mashindano hayo kwa kutwaa taji la Redds Miss Photogenic 2013. Nikiwa kambini wenzangu wote 29 walinikubali licha ya kwamba nilionyesha uwezo wa hali ya juu kuanzia kwenye kipaji hata michezo.
Mwanaspoti: Kuna tetesi kwamba wewe si Mtanzania halisi bali ni Mnyarwanda kuna ukweli katika hili?
Happiness: Naweza kusema kwamba mimi ni Mtanzania halisi. Hata hivyo, katika historia, marehemu baba yangu alikuwa Mhaya wa huko Kishozi, Bukoba na familia yote ya Watimanywa ni Watanzania halisi. Ila upande wa bibi yangu mzaa mama, babu yake ndiyo alikuwa Mkongo na bibi yake alikuwa Mnyarwanda.
Mwanaspoti: Mama yako Amina Bukoko anaonekana ni mdogo kiumri vipi mnaishije na je, mmezaliwa wangapi?
Happiness: Mama yangu alinizaa akiwa na umri wa miaka 21, hivyo hatujapishana sana. Tunaelewana na ananielekeza katika mambo mengi tu. Lakini nililelewa zaidi na bibi yangu hivyo wote naona ni kama mama zangu. Nina wadogo zangu wawili Romeo na Angel ambao wote wanaishi na baba na mama huko Morogoro na kwa sasa wanasoma katika Shule ya St Costantine niliyosoma mimi hapo awali.
Mwanaspoti: Je, una rafiki wa kiume?
Happiness: Aah (Anatabasamu) ndiyo ninaye lakini siko tayari kumtaja kwa jina na nina sababu nyingi za kufanya uhusiano wetu kuwa siri.
Mwanaspoti: Ni kitu gani kibaya ambacho hutoweza kukisahau?
Happiness: Sitosahau nikiwa darasa la nne bibi yangu alivamiwa na majambazi na walimuumiza sana kiasi cha kulazwa hospitalini. Niliporudi nyumbani likizo niliambiwa kuwa bibi alikuwa anaumwa lakini sasa anaendele vizuri. Nilijisikia vibaya sana baada ya kugundua kuwa ugonjwa wake ulitokana na majeraha aliyoyapata baada ya kuvamiwa.
Mwanaspoti: Kitu gani kizuri ambacho huwezi kukisahau katika maisha yako?
Happiness: Kufika katika kilele cha Uhuru, Mlima Kilimanjaro, kwa kweli ni kumbukumbu nzuri ambayo sitoisahau hasa nilipodhani kuwa nikifika pale juu nitaiona Moshi, lakini nilichoambulia kuona ni mawingu na mawe pekee kutoka juu kwenda chini, yaani haielezeki.
No comments:
Post a Comment