Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kuchaguliwa kwake |
Dar es Salaam. Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amempongeza na kumuafiki Jamal Malinzi kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 27 mwaka huu.
Malinzi alitwaa nafasi hiyo baada ya kumbwaga mpinzini wake, Athuman Nyamlani kwa jumla ya kura 73 dhidi ya 52 za mpinzani katika uchaguzi uliofanyika Dar es Salaam.
Katika salamu zake kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya CAF na familia ya soka Afrika, Rais Hayatou alisema uchaguzi huo unampa Rais Malinzi fursa ya kuupeleka mbele mpira wa miguu nchini Tanzania.
Alisema CAF ina imani na uwezo wake katika uongozi, uzoefu na ujuzi katika soka havitalisaidia soka la Tanzania pekee bali Afrika kwa ujumla.
Tayari Malinzi ameshatangaza kuvunja kamati zote zilizoundwa chini ya uongozi wa Tenga zikiwa zile za kudumu na zile ndogo ndogo za kisheria huku akitoa msamaha kwa wote waliofungiwa katika masuala ya soka isipokuwa wale waliohukumiwa kwa rushwa au kupanga matokeo.
Habari za uhakika ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa Malinzi anatarajia kutangaza Kamati ya Ufundi ambayo itaongozwa na Wilfred Kidau huku Ally Mayai ‘Tembele’ atakuwa miongoni mwa wajumbe.
Pia atamrejesha kundini Ramadhan Nassib kwa kumpa Kamati ya Fedha na Masoko. Nassib aliangushwa kwenye uchaguzi huo na Wallace Karia. Mwingine atakayeneemeka na utawala huo wa Malinzi ni Pelegrinius Rutayuga ambaye atapewa Kamati ya Vijana.
Katika kuhakikisha mabadiliko hayo ndani ya TFF, tayari Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo umemteuwa Said Hamad El Maamry kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ili kulinda mali za shirikisho hilo.
Wajumbe wa bodi hiyo ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye anakuwa Makamu Mwenyekiti, Dk Ramadhan Dau, Mohamed Abdulaziz na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Stephen Mashishanga.
Rais huyo mpya wa TFF, Jamal Malinzi anatarajiwa kukabidhiwa ofisi Jumamosi na Rais aliyemaliza muda wake, Leodegar Tenga ambaye ameiongoza taasisi hiyo kwa miaka minane baada ya kuiongoza kwa vipindi viwili vya miaka minne minne tangu alipochukua ofisi hiyo mwaka 2005
No comments:
Post a Comment