Saturday, 5 April 2014
FAGIO: Mourinho kuwatimua mastaa Chelsea
KICHAPO kimechafua hewa Stamford Bridge.
Jose Mourinho amecharuka, hashikiki na
kufichua wazi lazima apitishe panga mwishoni
mwa msimu.
Kocha huyo baada ya kushuhudia kikosi chake
kikichapwa na Paris Saint-Germain mabao 3-1
kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumatano
iliyopita, alimshukia straika Fernando Torres na
kufichua kwamba hatakuwa na chake tena
klabuni hapo.
Ripoti zinabainisha kwamba Torres ametajwa
mwanzo tu na kocha huyo amepanga kupitisha
panga kwa mastaa watano.
Kwenye orodha hiyo, Ashley Cole, straika
Romelu Lukaku, Mbrazili David Luiz na kiungo
mkabaji wa Nigeria, John Obi Mikel
wataonyeshwa mlango wa kutokea Stamford
Bridge.
Kutokana na bilionea mmiliki wa klabu hiyo,
Roman Abramovich kuwa kwenye presha
kubwa ya kuendana na sera ya usawa wa
matumizi ya pesa kwenye usajili, Mourinho ni
lazima awatimue wachezaji waliopo klabuni ili
kufungua njia ya kusajili nyota wapya.
Wachezaji wengine ambao wanatajwa kuwa
kwenye hatihati ya kuendelea kubaki kwenye
klabu hiyo hadi msimu ujao ni beki John Terry
na kiungo Frank Lampard ambao watamaliza
mikataba yao mwishoni mwa msimu na
hawajapewa ofa ya mikataba mipya.
Mchezaji mwingine atakayeingia kwenye orodha
hiyo ni straika Samuel Eto’o, ambapo kama
wote wataondoka basi klabu itakuwa imenusuru
Pauni 22 milioni kwa mwaka na hivyo
watakuwa huru kufanya usajili wa nyota wapya.
Kipa, Petr Cech, naye yupo kwenye wakati
mgumu baada ya Mourinho kufichua wazi
kwamba Thibaut Courtois, anayecheza kwa
mkopo Atletico Madrid atarejea Stamford
Bridge mwishoni mwa msimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment