Saturday, 1 March 2014
VAN PERSIE AWAOMBA MSAMAHA WENZAKE
MANCHESTER, ENGLAND
ROBIN van Persie ameinamisha kichwa chake
chini na kusema ‘samahani’. Ndiyo, alikosea.
Hata yeye mwenyewe amejua kuwa alikosea
kuwashutumu wachezaji wenzake kuwa
hawampi nafasi uwanjani.
Hata hivyo, nyota huyo wa kimataifa wa
Uholanzi, amedai kwamba hakuwakosoa mastaa
hao katika mahojiano aliyoyafanya mapema
mwanzoni mwa wiki.
Kwa mujibu wa kituo kimoja cha televisheni
cha kwao Uholanzi, inadaiwa kuwa Van Persie
aliwashambulia wachezaji wa Manchester
United kwa kushindwa kujipanga uwanjani na
kumnyima nafasi yake ya kucheza vyema.
Tukio hilo lilitokea mara baada ya pambano
dhidi ya Olympiakos ambalo Manchester
United walipigwa 2-0 ugenini na kuiweka
matatani ndoto yao ya kufika robo fainali ya
Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Hata hivyo imedaiwa kuwa Van Persie aliwaita
wachezaji wa timu hiyo mmoja mmoja wakiwa
mazoezini katika Uwanja wa Carlington na
kufafanua kauli yake huku akidai kwamba
ililenga katika kuzungumzia kiwango chake
binafsi na si kuwazungumzia wao.
Kauli hiyo ya Van Persie ambaye alinunuliwa na
Sir Alex Ferguson kutoka Arsenal kwa dau la
Pauni 25 milioni misimu miwili iliyopita,
imesababisha kizaazaa katika vyumba vya
kubadilishia nguo Manchester United.
Imedaiwa kuwa staa wa kimataifa wa Mexico,
Javier Hernandez ‘Chicharito’ ni miongoni mwa
mastaa waliokerwa na kauli hiyo huku akimjibu
Van Persie kimafumbo kwa kusema mchezaji
hawezi kufanikiwa bila ya kushirikiana na
wachezaji wenzake.
Chicharito alituma picha akiwa anashangilia
bao la Patrice Evra katika moja ya mechi za
Manchester United huku akiandika ‘Bila ya
wachezaji wenzako hauwezi kuwa lolote katika
soka. Siku zote kuwa na shukrani’.
Hata hivyo, baadaye siku hiyo hiyo Chicharito
alisema hakuwa anamshambulia Van Persie.
Alisema: “Kauli yangu katika Instagram
haikumlenga RVP. Sisi ni marafiki wazuri katika
timu moja na tuna lengo moja.”
Wakati huohuo, beki mkongwe wa Manchester
United, Patrice Evra, amedai kwamba kustaafu
kwa Sir Alex Ferguson bado kunaleta wingu zito
Old Trafford na kila mtu anapaswa kusahau
suala hilo mapema.
“Kulikuwa na mabadiliko makubwa na kila mtu
lazima asahau. Hakuna anayependa mabadiliko.
Timu ilicheza kwa miaka 27 na Alex Ferguson.
Tuko nyuma ya kocha mpya. Tutafanya kila
tunaloweza kufuzu katika Ligi ya Mabingwa.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment