Friday, 21 March 2014
Usajili mpya waanza Simba
SIMBA ambayo inapigana usiku na mchana
kusaka nafasi tatu za juu kwenye msimamo wa
Ligi Kuu Bara, imekifanyia tathmini kikosi
chake na kugundua matatizo mengi.
Kutokana na matatizo hayo, Simba sasa
imeamua kuanza usajili wake mapema ingawa
baadhi ya wachunguzi wa mambo wamehusisha
usajili huo na kampeni za uchaguzi wa klabu
hiyo uliopangwa kufanyika Mei 4, Dar es
Salaam.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka
ndani ya Simba, zimeeleza kuwa tayari uongozi
wa timu hiyo umekata tamaa ya kupata nafasi
mbili za juu lakini wameamua kuifanya siri yao
na kufa na tai shingoni kwa kutengeneza
mikakati mipya ya kusuka kikosi cha mwakani.
Katika kukamilisha mipango hiyo, Simba
imemuagiza Mkurugenzi wao wa Ufundi,
Mosses Basena raia wa Uganda, kuzunguka nchi
mbalimbali Afrika kutafuta wachezaji wapya wa
kigeni ili kurudisha nguvu mpya ndani ya Simba
na kupata wachezaji makini tofauti na misimu
iliyopita ambayo wamekuwa wakiingia mkenge
kwa kuletewa magarasa.
Tayari Basena alishaondoka nchini wiki moja
iliyopita kuanza mchakato huo kwenye nchi
ambazo ligi zinaendelea.
Alianzia Uganda ambako alikuwa anatafuta
mabeki wa pembeni, kiungo namba nane na
kiungo mshambuliaji atakayesaidiana na
mfungaji wao mahiri Mrundi Amissi Tambwe.
Basena anatarajiwa kurejea nchini leo Alhamisi
baada ya kuwasilisha ripoti atageuzia rada zake
Afrika Magharibi.
Mwanaspoti lilimtafuta Kocha Mkuu wa Simba,
Zdravko Logarusic ambaye alikiri kuwepo kwa
mpango huo ambapo alisema wanalenga
mipango ya baadaye ya timu hiyo ingawa bado
hajajua kama ataendelea kuwepo katika kikosi
hicho kwa kuwa mkataba wake unaishia Juni
Mosi.
“Hilo lipo, tunafanya kazi kwa karibu na
Basena, tunataka kuanza kufikiri kuhusu
baadaye hasa kwa nafasi ambazo tunaona
zilitupa shida katika msimu huu, tunatakiwa
kuanza sasa maandalizi ya msimu ujao,
nimeshiriki katika mchakato huo ingawa sina
uhakika mpaka sasa kama nitakuwa hapa kwa
wakati huo kwani mkataba wangu unafika
mwisho Juni Mosi,” alisema Logarusic.
Hata hivyo Logarusic alipoulizwa nyota gani
wanaweza kuachwa katika kikosi hicho alisema
kazi hiyo bado haijafanyika kwani wanasubiri
msimu umalizike waone timu itaishia nafasi
gani.
Katibu Mkuu wa Simba, Ezekiel Kamwaga
alisema: “Kuhusu Basena ni kweli nimemtuma
kikazi Uganda kuna kazi amekwenda kutufanyia
lakini kwa sasa siwezi kusema majukumu
tuliyomuagiza kwenda kuyatekeleza, wakati
ukifika tutaweka wazi.”
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment