MSHAMBULIAJI wa kigeni wa Simba Mrundi, Amissi Tambwe, ameingia hofu ya kuendelea kuifungia mabao timu yake katika Ligi Kuu Bara baada ya kuumia misuli ya paja la kulia. Anasema ni mara yake ya kwanza kupata tatizo hilo.
Tambwe aliyejiunga na timu hiyo msimu huu, hajawahi pia kuwa majeruhi tangu atue Simba na jambo hilo limempa hofu kubwa hasa wakati huu anapotakiwa kuipandisha juu ya msimamo kutoka nafasi ya nne ilipoganda na pointi 36.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe alisema alianza kuhisi maumivu hayo wakati wa mechi dhidi ya Prisons iliyochezwa Mbeya ambayo pia ilimshuhudia akichanika usoni.
“Tangu hapo paja linaniuma sana. Ninasikia maumivu makali wakati wa kukimbia, hata mazoezi nafanya kwa shida,” alisema.
Alisema hali hiyo inamfanya acheze chini ya kiwango kutokana na hofu ya kujiumiza zaidi hasa anapovaana na mabeki ambao anasema siku hizi wanampania vilivyo.
“Ninasikitika sana kuumia misuli ya paja, ninahisi kama ndoto zangu za ufungaji bora zitafutika,” alisema.
Daktari Mkuu wa Simba, Yassin Gambe, alisema: “Kweli Tambwe ana tatizo la misuli kwenye paja lake la kulia, hata mazoezi yake anafanya mepesi tofauti na wenzake.”
Naye kocha wa Simba, Zdravko Logarusic, alikiri kukabiliwa na tishio la kumkosha Tambwe, lakini anaamini atapata nafuu mapema ili amtumie kwenye mechi walizobakiza.
No comments:
Post a Comment