Saturday, 1 March 2014

SOMA NYUMA YA PAZIA YA JANA;Wazza na maneno ya hekima ya Mignon


WOTE tunazaliwa mashujaa, waaminifu na walafi, lakini mwisho wa yote wengi wetu tunabakia kuwa walafi tu.”
Maneno haya aliwahi kuyasema mwandishi maarufu wa kike wa Marekani, Mignon McLaughlin.
Yeye mwenyewe alifariki siku tano kabla ya sikukuu ya Krismasi mwaka 1983. Sijui kama alikufa akiwa bado mlafi. Kama kuna maisha mengine baada ya haya, nitamuuliza Mignon aniambie anajihisi alikufa akiwa mlafi, mwaminifu au shujaa?
Wayne Rooney, maarufu kwa jina la Wazza, aliposhika peni wiki iliyopita kusaini mkataba mpya Manchester United huku akiondoka na dau la Pauni 300,000 kwa wiki, nilijiuliza, Rooney ni mwaminifu, shujaa au mlafi?
Tabasamu usoni, kalamu mkononi, Pauni 70 milioni katika akaunti. Wazza alihitaji nini zaidi? Alihitaji pesa tu. Mwondoe Wazza katika kundi la watu waaminifu. Hata Sir Alex Ferguson anajua kuwa Rooney si mwaminifu. Ni mlafi. Hakuna cha kushangilia sana katika mkataba wake mpya.
Muda mwingi wakala wake, Paul Stretford na yeye mwenyewe wametumia katika kuichezea akili Manchester United kwa kujifanya kama anataka kuhama hili United ilazimike kulipa pesa nono kwake.
Ndiyo maana hakuwahi kutaka kukanusha kwenda Chelsea wakati jina lake likivumishwa kwenda huko. Wala hakuwahi kukanusha kutaka kuchezea nje ya England. Wala hakuwahi kukanusha kwamba hataki kucheza Real Madrid .
Lakini moyoni alijua kwamba anataka kubaki Old Trafford. Alichotaka ni kuhakikisha Manchester United inambakiza kwa gharama yoyote hasa wakati huu ambapo maisha ya klabu yake yanayumba.
Pengine kuliko muda mwingine wowote, Manchester United ina asilimia nyingi za kukosa nafasi nne za juu. Lakini unadhani Wazza anajali sana kucheza Ligi ya Mabingwa UIaya? Ametwaa ubingwa wa Ulaya, ametwaa mataji matano Ligi Kuu England, mawili ya FA, moja la Klabu Bingwa ya Dunia. Unadhani anajali sana kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao? Anachojali ni kile kilicho katika akaunti yake.
Anachojali zaidi ni namna anavyoweza kumtunza Coleen McLoughlin na watoto wake Kai na Klay. Anachojali ni jinsi gani atakavyomudu kununua jumba la kifahari Florida muda wowote atakaojisikia.
Huu ndiyo ulikuwa wakati mwafaka wa Wazza kuhama Manchester United kwa kisingizio cha ubovu wa timu. kama ni mapenzi, Rooney ni shabiki wa Everton na Celtic. Lakini kitu kikubwa maishani kwake ni pesa.
Wazza ni mwaminifu kwa Everton na ndio maana aliwahi kusema ‘Once blue always blue’ akimaanisha kuwa ukiwa Everton siku zote utakuwa Everton. Wazza pia ni shujaa. Ndiye mwanasoka ambaye ukiweka mguu yeye ataweka kichwa. Lakini hapa mwishoni katika ulafi, naye yumo sana.
Oktoba mwaka huu atatimiza umri wa miaka 29. Hiki ndicho anachoangalia zaidi. Na atapokea pauni 300,000 kwa wiki mpaka atakapotimiza miaka 33, wakati huo Marekani ikiwa na Rais mwingine baada ya Barrack Obama.
Pesa ndio kila kitu katika maisha ya wanasoka wa kisasa. Unadhani Rooney ni mjinga? Basi mfuatilie Cristiano Ronaldo alichofanya katika kipindi cha majira ya joto kilichopita. Alitumia mbinu hii hii.
Muda wa dirisha lililopita la majira ya joto, Ronaldo alikuwa hakanushi lolote kuhusu uvumi kwamba alikuwa anataka kurudi Old Trafford kujiunga na kikosi cha Sir Alex Ferguson. Nyuma yake alikuwepo wakala wake Jorge Mendes ambaye ndiye alikuwa anauchezesha mchezo wote.
Miezi michache baadaye, Ronaldo alikuwa akisaini mkataba wa mamilioni ya pesa Santiago Bernabeu. Unadhani anajali sana mafanikio ya Madrid? Unadhani anatamani zaidi kuchukua Ligi ya Mabingwa kuliko kuwa mchezaji tajiri zaidi duniani?
Kwa upande wa Manchester United, katika suala hili la Wazza hawakuwa na kitu cha kufanya zaidi. Aliwabana pazuri zaidi lakini na wao wamepiga hesabu nzuri.
Ukimsajili Radamel Falcao au Edinson Cavani kwa sasa utalipa kwa klabu yake Pauni 45 milioni na zaidi. Baada ya hapo utampa mkataba wa miaka mitano wenye thamani ya Pauni 250,000 ka wiki. Hesabu zake kwa ujumla utapata kiasi cha Pauni 80 milioni na zaidi.
Kwa staili hii ilikuwa ni bora kwa David Moyes kumbakiza Wazza kwa gharama yoyote ile. Kwanza ni kwa sababu ilikuwa ni kucheza bahati nasibu kumleta mshambuliaji mwingine ambaye si ajabu angeweza kuwa kama Fernando Torres alipohamia Stamford Bridge kutoka Anfield.
Chaguo pekee lilikuwa kumbakisha Wazza. Wazza mwenyewe hakuwa na shida sana licha ya kuzuga kwamba alikuwa anataka kuondoka zake Old Trafford. Angeondoka vipi wakati yeye alikuwa ameamua kuwa chaguo la tatu la Mignon kwa maneno yake matatu ya ushujaa, uaminifu na ulafi?
Aliamua kwenda katika chaguo la tatu. Na wala simlaumu yeye. Wanasoka wote wako hivyo hivyo. Hata Samuel Eto’o alienda Russia kwa kuchagua hilo neno la tatu la Mignon. Alifuata pesa tu.

No comments:

Post a Comment