UKIACHANA na wazee wenye rekodi za aina yake kwenye dansi la Tanzania kama Maalim Gurumo, Hassan Bitchuka, Shabaan Dede na wengineo, kizazi cha miaka ya karibuni kuna watu watatu ambao wamesumbua sana.
Hao ni Ali Choki, Banza Stone na Mwinjuma Muumini. Ubunifu wa wasanii hao ndio umewafanya kuwa juu lakini ni Choki ndiye anayeendelea kufanya vizuri zaidi kwa sasa akiiongoza Extra Bongo kama Mkurugenzi.
Choki amezungumzia mustakabali wa muziki nchini pamoja na mambo mbalimbali lakini amekiri kwamba muziki wa dansi bado haujashuka kama watu wanavyodhani bali mabadiliko yaliyopo ndiyo yanafanya muziki huo uonekane kushuka kwani wengi wa mashabiki wa muziki kwa sasa wanasikiliza muziki wa Bongo Fleva.
Anasema kwamba muziki huo wa vijana umewaibia mashabiki kwani unapewa nafasi kubwa sana kila sehemu ikifuatiwa na dansi na Taarab ambazo nazo zina watu wake.
“Ukiwa msanii unatakiwa kuwa mbunifu na kazi yako, hutakiwi kuwa na mfumo mmoja tu kwa mashabiki wako, wape mashabiki burudani tofauti yenye vionjo mbalimbali, hivyo ndivyo ninavyofanya mimi sina mfumo mmoja.
“Mfano kila ninapotaka kuzindua albamu mpya ni lazima nifikirie upya jinsi ya kuingia ukumbuni ili mashabiki wanione ni wa tofauti na nimekuja na kitu kipya,’’ anasema Choki.
Choki ambaye amewahi kutamba na bendi mbalimbali ikiwemo Twanga Pepeta, Mchinga G8, Double Extra, TOT Plus na nyinginezo, anasema kuwa muziki wa sasa haulipi bali hufanywa kimazoea kutokana na utandawazi ulioingia.
“Kazi zetu zinaharibiwa na mitandao, kwa sasa hakuna mtu anayepokea kazi zetu kwa ajili ya kuuza, hii ni kwa sababu kabla kazi haijafika kwa wadosi tayari mtaani inakuwa imeanza kusikika.
“Yote haya yanafanywa na wanamuziki wenyewe, kazi zao zinapomalizika huwa wanaomba kuzisikiliza lakini cha ajabu wanaziingiza kwenye mitandao na watu wanaanza kuzisikia.
“Kwa mfumo huu sanaa yetu ya muziki itakufa au kama haitakufa basi itakuwa haisikiki kama miaka ya nyuma ingawa pia kwa kiasi fulani huchangiwa na vyombo vya habari hasa redio ambazo siku hizi hazipigi sana nyimbo zetu,” anasema.
Faida
“Kwa sasa hakuna faida kubwa kwenye muziki, kwanza tunauza wenyewe mkononi hivyo hata gharama ya matengenezo ya albamu huwa hayarudi, tunatumia gharama kubwa lakini fedha tunayoingiza ni ndogo.
“Tangu nianze muziki kila albamu inakuwa na faida yake kutokana na mauzo yanavyokuwa lakini albamu ambazo ziliniingizia faida kubwa ni ile ya Special Remix tuliyoshirikiana na Mzee Gurumo na Respect kwa kweli zilifanya vizuri sana.
“Mbali na hiyo kuna albamu niliifanya nikiwa Twanga iliyokuwa na nyimbo za Fainali Uzeeni na Umbea Hauna Posho, Mhindi alinunua nyimbo hizo mbili tu ingawa alituambia tujazie nyingine.
Akiwa Mchinga mwaka 2005 pia alifanikiwa kutengeneza albamu iliyoitwa Mwaka wa Tabu ingawa katika bendi hiyo alikaa kwa miezi sita tu na kurudi Twanga ambako walimpa mkataba wa miaka miwili na baada ya mkataba huo alisaini mkataba mpya TOT wa mwaka mmoja na nusu.
Akiwa TOT alipewa rungu la kuajiri wanamuziki na kufunga safari hadi Jamhuri ya Congo ambao walifanya vizuri na bendi hiyo iling’ara.
“Extra Bongo ilikuwepo tangu 2003 lakini niliipumzisha tu, mwaka 2009 niliirudisha upya napo haikuweza kudumu kwa sababu fitina za muziki ziliingia, nilichukuliwa wanamuziki wote na kujikuta nabaki na wanamuziki wachache ambao haikuwa rahisi kufanya nao kazi.
“Mwaka 2010 niliamua kuanza upya na kuchukuwa wanamuziki sehemu mbalimbali ikiwemo Twanga ambapo nilimchukuwa Rogert Hega, Ferguson na wengine ambao waliisaidia kuisimamisha bendi kwa nguvu moja,” anaeleza Choki.
Mafahari Watatu
Wana mpango wa kufufua kundi lao hilo linaloundwa na wanamuziki watatu mahiri, Choki, Muumini na Banza, ila wanahitaji mtu wa kuwawezesha kifedha ili watengeneze albamu yao.
“Ushirikiano wetu Mafahari Watatu tunashirikiana vizuri tu, ingawa kila mtu ana shughuli zake lakini binafsi ninapokuwa na kazi zangu huwa nawashirikisha na ndiyo maana hata uzinduzi wangu mwezi uliopita nilimwalika Muumini.
“Hiyo yote ni kutaka kuwaonyesha watu kuwa sisi ni wa moja na tumefanya kazi kwa muda mrefu na tunapoona mmoja hana kazi basi humshirikisha ili naye aweze kufanya kazi yake.
“Tumekubaliana kurudi kutengeneza albamu ya pamoja lakini tatizo lipo kwenye fedha, tukipata mtu anayeweza kutudhamini basi mashabiki watatuona tena pamoja,’’ anasema Choki.
Hivi karibuni Choki alifanya uzinduzi wa albamu yake mpya ya Mtenda Akitendewa n amepanga kuifanyia uzinduzi mikoani huku akidai kuanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa.
“Huwa nachukuwa muda mrefu kutoa albamu kwa sababu napenda kuanza na utengenezaji wa video ndipo nizindue albamu, hii albamu nilianza kuitengeneza 2010 na kuizundua mwaka huu.
Anasema kuwa kamwe hawezi kuwatupa wanamuziki wenzake Banza Stone na Muumini kwani wameanza muda mrefu kufanya kazi ya muziki pamoja: “Banza amebadilika kwa sasa hata kazi anafanya vizuri, siwezi kuwatupa,”.
Ushindani wa bendi
“Kwa sasa hakuna ushindani katika bendi tofauti na miaka kadhaa iliyopita, siku hizi mashabiki wetu wamejua utamu wa nyimbo za nyumbani ndiyo maana hata zile bendi zilizokuwa zikitamba sana huko nyuma zikiongozwa na wanamuziki wengi kutoka DR Congo zimepoa,” anasema Choki.
Choki kwa sasa anaendelea na ratiba yake ya uzinduzi wa albamu yao mpya ambapo anajiandaa kwenda mikoa ya Kanda ya Ziwa katika kipindi cha Pasaka.
No comments:
Post a Comment