![]() |
KIKOSI kamili cha Yanga kipo kambini mjini Bagamayo, Pwani kikijiweka sawa kabla ya kushuka Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam keshokutwa Jumamosi kuumana na Komorozine ya Comoro kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Miongoni mwa nyota walioko katika maandalizi hayo ni straika, Emmanuel Okwi aliyeleta utata mkubwa.
Yanga imemweka mchezaji huyo kwenye mipango yake kwa madai kuwa ina uhakika wa kumtumia katika mechi hiyo endapo leseni yake itakuja kutoka makao makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ambalo ndilo husimamia michuano ya Afrika. Lakini kwa mujibu wa kanuni za CAF mchezaji anayecheza mashindano yake lazima awe anacheza kwenye ligi ya ndani ya nchi husika ambayo husimamiwa na shirikisho la nchi husika.
Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limemzuia Okwi kuichezea Yanga kwenye Ligi Kuu Bara mpaka itakapopata ufafanuzi wa kina wa kisheria kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambalo awali lilimuidhinisha kuichezea SC Villa ya Uganda, lakini klabu hiyo ikamuuza kwenda Yanga ndani ya muda mfupi.
Kigogo mmoja wa Yanga aliyeko kwenye jopo la kamati inayoiongoza Yanga kwenye michuano ya kimataifa, alisema wamefanya utafiti wao CAF na kubaini kwamba Okwi atapata leseni na atacheza ndio maana wanamwandaa.
Alidai kwamba siku moja kabla ya mchezo, CAF itatuma kivuli cha leseni za wachezaji wote watakaoruhusiwa kucheza katika mchezo huo kwa timu zote mbili za Yanga na Komorozine na wanaamini ya Okwi itakuwemo.
Mwanasheria mkongwe kwenye michezo nchini, Alex Mgongolwa, alithibitisha kwamba endapo CAF itatuma leseni ya Okwi kabla ya mchezo huo ambayo ndiyo inatakiwa kwa kamisaa wa mchezo, nyota huyo atakuwa huru kuichezea Yanga katika mechi hiyo na nyingine zote zitakazofuata.
“Nikweli kwamba CAF kabla ya mchezo huo itatuma leseni hizo za wachezaji wa timu zote mbili ambazo wanatakiwa kuzitumia katika kujiridhisha kama wachezaji watakaocheza ni halali au vinginevyo,” alisema.
“Katika leseni hizo kama ya Okwi ikifika basi hakuna shaka kwamba atakuwa huru kuichezea Yanga kwenye mechi hiyo na zingine zozote zitakazokuwa chini ya CAF.”
Okwi ambaye alikuwa mchezaji wa Simba, aliuzwa kwenda Etoile du Sahel ya Tunisia, hata hivyo timu hiyo haikuilipa Simba wala mchezaji huyo ambaye aliamua kugoma kucheza. Jambo hilo liliifanya Fifa kumruhusu aichezee Villa kwa muda wakati suala lake likifanyiwa kazi.
No comments:
Post a Comment