Saturday, 8 February 2014

Mwamuzi aliyemtoa Ronaldo afungiwa




MADRID, HISPANIA
MWAMUZI aliyemtoa kwa kadi nyekundu supastaa, Cristiano Ronaldo kwenye mchezo wa sare ya bao 1-1 kati ya Real Madrid na Athletic Bilbao kwenye Ligi Kuu Hispania wikiendi iliyopita amefungiwa mwezi mmoja kutokana na utata wa tukio hilo.
Mwamuzi huyo, Miguel Angel Ayza Gomez ameadhibiwa na Kamati ya Ufundi ya Chama cha Waamuzi wa Ligi Kuu Hispania (CTA) na kwamba haruhusiwi tena kucheza mechi za Real Madrid msimu huu.
Ayza Gomez alitoa taarifa mbili zenye utata kuhusu kadi nyekundu ya Ronaldo, kwanza alidai amefanya hivyo baada ya staa huyo kumpiga kibao nahodha wa Bilbao, Carlos Gurpegi, kabla ya baadaye kudai amemtoa nje mwanasoka huyo bora duniani kwa sababu alizozana na kiungo Ander Iturraspe kwenye purukushani za tukio hilo.
Utata wa ripoti yake ulimponza Ayza Gamez, huku mwamuzi wa zamani wa Ligi Kuu England, Graham Poll akidai kwamba Ayza ametolewa kafara kutokana na nguvu ya Real Madrid.

No comments:

Post a Comment