Thursday, 13 February 2014

MOYES AKIRI HALI NI MBAYA

MANCHESTER, ENGLAND
HALI ni mbaya zaidi. Mtu anayesakamwa zaidi
katika mchezo wa soka kwa sasa, kocha David
Moyes wa Manchester United, amekiri kuwa
hali ni mbaya sana Old Trafford kuliko wakati
mwingine wowote.
Wakati mashabiki wa timu hiyo wakiamini
kuwa timu yao ilikuwa imeshinda 2-1 katika
pambano dhidi ya Fulham juzi Jumapili, katika
sekunde za majeruhi, mshambuliaji wa Fulham,
Darren Bent, alifunga bao lililoipatia sare ya
2-2 timu yake katika dimba la Old Trafford.
Bao hilo limeiacha Manchester United ikiwa
pointi tisa nyuma ya timu inayoshika nafasi ya
nne, Liverpool, ambayo saa 24 kabla ya mechi
hiyo ilikuwa imeiburuta Arsenal mabao 5-1
katika Uwanja wa Anfield.
Alipoulizwa kama alijua kuwa mambo
yangekuwa kama yalivyo sasa, Moyes alijibu:
“Hapana kwa kweli. Imekuwa kama hivi msimu
huu, lakini leo (juzi Jumapili) imekuwa mbaya
mno. Unaweza kusema kwamba tulikuwa laini
sana akilini na hatukumaliza kazi yetu.
Nakubali.
“Tulitawala mchezo. Kufungwa bao moja
lilikuwa jambo baya. Kiasi cha nafasi
tulizotengeneza, tulizojaribu na jinsi
tulivyocheza ilishangaza sana kwa nini
hatukushinda, yaani sielewi.
“Tulimiliki mpira kadiri tulivyoweza. Tungeweza
kufunga zaidi. Wachezaji walijaribu na mabao
yalikuja, hata wakati walipofungwa 2-1  na
dakika tano kuongezwa Fulham bado
hawakucheza vizuri, walituacha sana na mpira
kwa hiyo lilikuwa suala la kupoteza muda,
lakini ghafla tukawapa bao la kijinga sana.
“Wachezaji wameumia sana. Naona kila siku
jinsi wanavyoumizwa kwa sababu matokeo
hayaji kama wanavyotaka. Lakini tuna timu
nzuri na kuna timu chache sana zinazotamani
kucheza na sisi, nina uhakika.”
Kwa mara ya kwanza baada ya miaka mingi,
Manchester United sasa iko katika hatari ya
kukosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa
Ulaya na Moyes alipoulizwa kuhusu suala hilo,
alijibu kwa kifupi: “Tutajaribu kadiri
tuwezavyo.”
Beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher,
ambaye kwa sasa ni mchambuzi mahiri wa soka
England, alikiri kwamba hajawahi kuona timu
inajihami kwa kiasi kile kama ambavyo Fulham
ilifanya katika mechi dhidi ya Manchester
United.

No comments:

Post a Comment