Friday 17 January 2014

Yanga yang’ara Uturuki, kocha atoa onyo kali



KOCHA Mkuu wa Yanga Johannes Van Der Pluijm ametua Uturuki na kupokewa vizuri na vijana wake ambao jana Jumatano waliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fafanga Inc, mechi yake ya kwanza Yanga iliilaza mabao 3-0 timu ya Ankara Sekerspor.
Katika mechi ya jana mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu na Emmanuel Okwi.
Sambamba na hilo, Kocha Msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa aliliambia Mwanaspoti kutoka Uturuki kuwa bosi wake alikutana na viongozi na baadaye wachezaji ambao aliwatahadharisha kuhusu nidhamu na kuwaambia hatakuwa na mzaha katika hilo.
Mkwasa alisema kocha huyo amewataka wachezaji kuwa makini ndani ya uwanja kwa kutekeleza majukumu yao na nje ya uwanja hataki kusikia tatizo lolote kutoka kwao.
Kocha huyo kutoka Uholanzi pia amewaambia wachezaji hao kwamba ndani ya miezi sita ya ajira yake anataka kuona kikosi hicho kinafanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuhakikisha wanashinda michezo yote ya mbele yao.
Mkwasa alisema: “Kocha alivyofika alikutana na wachezaji wote na kufanya nao kikao kifupi cha kumtambulisha kwenye timu na katika kikao hicho alisisitiza nidhamu kuwa hatakuwa na masihara.’’
“Aliweka wazi kwamba katika kipindi cha zaidi ya miaka 14 aliyofanya kazi Afrika hajawahi kupata matatizo ya nidhamu kwa wachezaji wake na anataka iwe hivyo hivyo na Yanga.’’
Wakati Mkwasa akiyasema hayo, Makamu Mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga ameliambia Mwanaspoti jijini Dar kwamba, katika kumkabidhi kazi kocha huyo pia wamempa vyeo vingine viwili mbali na kuwa kocha wa timu hiyo.
Sanga alisema kocha huyo pia ametakiwa kutekeleza majukumu ya mkurugenzi wa ufundi kwani baada ya kuangalia vyeti uongozi uliona kufanya kazi hiyo sambamba na ile ya ukocha.
“Tuliangalia vyeti vyake tukaona tumpe majukumu hayo kwamba mbali na ukocha pia atakuwa na kazi ya kutekeleza majukumu ya mkurugenzi wa ufundi kwa wakati mmoja,” alisema Sanga.

No comments:

Post a Comment