DENIS Kadito, wakala wa mchezaji kiraka Mtanzania, Shomari Kapombe, ameandika waraka mzito kwa Simba akitoa ufafanuzi wa mambo mbalimbali ya mchezaji huyo, hatima yake pamoja na soka la Tanzania.
Ndani ya waraka huo wakala huyo hajazitaja kwa majina lakini Mwanaspoti linajua kwamba anazisema Yanga na Azam ambazo inadaiwa zinatumia nguvu kubwa kumshawishi Kapombe. Waraka huo unasomeka kama ifuatavyo;
Onyo kwa timu kuhusu Kapombe
Naomba nitoe ujumbe huu kwa Watanzania wapenda michezo, hususani mchezo wa mpira wa miguu. Kwa masikitiko makubwa sana, nimepata taarifa kwamba timu mbili maarufu hapo nchini Tanzania, zimekuwa zikiongea na Shomari Kapombe huku zikimpatia vishawishi na shinikizo ili avunje mkataba wake na timu ya AS Cannes ya Ufaransa.
Hii imenisikitisha sana, kwani kazi kubwa niliyofanya na ninayozidi kuifanya kila siku inaonekana kuharibiwa na watu wachache wasiopenda kuangalia maendeleo ya nchi yetu na malengo yangu katika kusaidia kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu.
Mimi nimechagua kuja Tanzania kujaribu kufungua milango katika nchi za Ulaya ili Watanzania tuweze kuendelea katika mchezo wa mpira wa miguu.
Naamini inaeleweka kwa kila mtu kwamba Shomari Kapombe ana mkataba wa miaka miwili na timu ya AS Cannes ya Ufaransa.
Kitendo cha timu hizi kuongea na mchezaji aliye ndani ya mkataba na timu nyingine bila kunishirikisha mimi kama wakala au timu ya AS Cannes ni kitu ambacho hakikubaliki chini ya sheria za Fifa.
Kitendo kinachofanywa na timu hizi kinajulikana kwa lugha ya Kiingereza kama “tapping-up a player”, kitu ambacho kinapingwa kwa nguvu zote na wanafamilia wote waungwana walio chini ya Fifa.
Adhabu yake inaweza kusababisha timu hizi zipigwe faini kubwa na kufungiwa kufanya usajili kwa kipindi fulani. Pia kumshinikiza mchezaji avunje mkataba bila sababu maalumu kunaweza kusababisha mchezaji apigwe faini kali sana na kufungiwa kucheza mpira kwa kipindi fulani.
Nimesikikitishwa sana na timu moja kongwe kufanya vitendo hivi. Lakini vitendo hivi havinishangazi sana. Timu hii imekuwa ikitumia nguvu ya pesa kufanya mambo watakavyo na itafika muda watu tuseme inatosha sasa na sheria ifuate mkondo wake.
Huko nyuma, timu hii kongwe iliwasajili wachezaji wangu wawili bila kunishirikisha mimi kama wakala wao. Wachezaji hao ambao wana mkataba na mimi ni wachezaji wa timu ya Taifa za Tanzania na ya nchi jirani. Mpaka leo hii, nimekuwa muungwana sana na wala sijataka kuisumbua hii timu kongwe.
Kitendo cha kuongea na Shomari Kapombe bila kunishirikisha ni kwamba wamedhamiria kuzidi kunichokonoa na kuonyesha dharau ya hali ya juu.
Naomba nitoe onyo kwamba, sitasita kuwafikisha Fifa na kuwashitaki ipasavyo. Kama sheria za Fifa zinaweza kuishughulikia timu kubwa na yenye utajiri mkubwa kama Chelsea, basi sina wasiwasi kwamba mkono wa sheria utafika Tanzania.
Timu nyingine changa, ambayo imekuwa ikionekana kama timu iliyojipanga na kufanya mambo kisasa zaidi hapo nchini, imenisikitisha sana kuingia katika mkumbo huu.
Ninaiomba timu hii chini ya uongozi wake waendelee kufanya mambo kwa kisasa na wazidi kuonyesha kwa vitendo maendeleo ambayo kila mtu angependa ayaone nchini kwetu Tanzania.
Kwa hapo Tanzania, nimeanza kwa kushirikiana na Simba SC, lakini napenda nitoe changamoto kwa timu nyingine kama za Yanga, Azam FC, Mtibwa kwamba mimi niko tayari kushirikiana nao katika shughuli mbalimbali za kuendeleza soka hapo nchini kwetu.
Ninaomba tufuate na tuheshimu sheria za Fifa ambazo sisi kama wanafamilia wa mpira wa miguu, tumekubali zituongoze.
Kwa wachezaji mpira wa Kitanzania, hususani ambao wangependa kushirikiana nami, kabla ya kitu chochote kile, ninaomba tu nitoe ushauri kwamba ni muhimu sana wewe kama mchezaji ujitambue.
Mchezaji inabidi ujitambue wewe ni nani, malengo yako ni yapi na uko tayari kupitia changamoto gani ili ufanikishe malengo yako.
Mwisho, naomba niahidi kwamba, nikipata ushirikiano mzuri kutoka kwa Watanzania wenzangu wenye nia nzuri, basi sina wasiwasi Tanzania tutapiga hatua kubwa miaka michache ijayo.
Asanteni sana,
Denis Kadito
Wakala chini ya Chama cha Mpira wa Miguu Uholanzi, KNVB
No comments:
Post a Comment