J,OHANNES Chrysostomus Wolfgangus Theophilus Mozart. Je unamfahamu mtu huyo? Wachache wanamfahamu. Wachache waliwahi kumsikia. Pamoja na majina hayo matano, alifahamika zaidi kwa jina moja, Mozart.
Alikuwa mfalme wa kupiga kinanda, ni mzaliwa wa Austria. Desemba mwaka jana, wakati tukikaribia kusherehekea sikukuu ya Krismasi, Mozart alitimiza miaka 222 tangu afariki dunia. Alikuwa mtaalamu hasa. Hakuna aliyekaribia kipaji cha Mozart. Kipaji chake kiliingia kaburini akiwa na umri wa miaka 35. Kutokana na kupendwa kwake kulikopindukia, kifo chake katika umri mdogo kiliwashtua wengi.
Madaktari walitoa sababu 118 za kifo chake kwa ajili ya kuwaridhisha mashabiki wake. Mpaka sasa kaburi lake lipo katika makaburi ya St. Marx, jijini Vienna, Austria.
Mpaka sasa kuna wafuasi wake ambao huwa wanaliinamia kaburi lake na kutega sikio wakiamini kuwa kuna sauti tamu ya kinanda inatoka katika kaburi la Mozart. Kutokana na kipaji chake maalumu wanaamini kuwa Mozart anaendelea kupiga kinanda chake kaburini.
Desemba mwaka uliopita wakati Mozart akitimiza miaka 222 tangu afariki, mwanasoka mmoja mwenye kipaji alionekana kuwa katika fomu sana katika Ligi Kuu England. Bahati iliyoje? Mtu huyu anaitwa Tomas Rosicky. Tangu Desemba, Rosicky yupo katika ubora wake. Anapiga chenga za madaha, anageuka haraka, anapandisha timu kwa haraka. Anaifanya Arsenal icheze kwa haraka katika eneo la adui.
Unalijua jina la utani la Rosicky? Wakati akikipiga katika klabu ya Borussia Dortmund mashabiki wa Ujerumani walimpachika jina la Little Mozart wakimaanisha kuwa ni Mozart mdogo. Unajua kwa nini alipewa jina hilo? Kwa sababu uwezo wake mkubwa wa kumiliki mpira huku wakati mwingine nyayo zake zikiwa hazigusi ardhini sawa sawa.
Wajerumani wakafananisha nyayo hizo na vidole vya Mozart wakati anachezea kinanda na vifaa vingine vya muziki.
Hapo hapo pia wakaamini kuwa Rosicky alikuwa kiunganishi wa timu kutokana na muono wake mkubwa wa soka, mbinu na pasi zake za haraka. Wakaamini hakuwa na tofauti sana jinsi Mozart halisi alivyokuwa anafanya katika nyimbo zake.
Katika pambano la hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu kati ya Arsenal dhidi ya Dortmund nchini Ujerumani, mashabiki wa Dortmund walishangilia sana wakati Rosicky alipoingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya kinda, Serge Gnabry.
Mashabiki wa Arsenal kwa sasa wanapagawa na kipaji cha Rosicky, lakini ukweli ni kwamba wamechelewa sana kugundua thamani ya kipaji cha Rosicky kutokana na majeruhi yake ya mara kwa mara.
Binafsi naamini, kama Rosicky angekuwa hasumbuliwi na majeruhi, basi kiwango chake kingekuwa katika anga za kina Andrea Pirlo, Andres Iniesta, Clarence Seedorf na wengineo. Tatizo ni majeruhi yake.
Hawa ni aina ya wachezaji ambao wameishia njiani. Tangu akiwa na miaka 28, kila wiki anakuwa majeruhi.
Kuna wachezaji wanaoishia njiani kwa staili tofauti. Javier Hernandez Chicharito naye ni aina ya wachezaji wanaoishia njiani.
Chicharito ni aina ya mchezaji ambaye ukimpanga kila mwisho wa wiki na ukamfanya awe staa wa timu basi angefikia anga za kina Ruud Van Nisterlooy au Fillipo Inzaghi. Aibu iliyoje kuwa makocha wanaomsimamia wanamwacha katika benchi kama shabiki.
Javier Saviola au Jose Antonio Reyes. Unawakumbuka hawa? Walikuwa na vipaji vikubwa wakati wanakuwa lakini vikatoweka taratibu. Tofauti yao na Little Mozart ni kwamba huyu ameathiriwa na majeraha ya muda mrefu, tena ya mara kwa mara.
Hata hivyo maisha ndivyo yalivyo, wakati mwingine hayatendi haki. Kuna wanasoka wengi wenye vipaji vya kawaida na wako uwanjani kila mwisho wa wiki. Lakini kwa Rosicky hadithi imekuwa tofauti.
Msimu huu Arsenal imemwambia kuwa atalazimika kufikisha idadi ya mechi 25 uwanjani ili aweze kupatiwa mkataba mpya klabuni hapo. Lakini katika ubora wake, kama miguu yake ingetumia kipaji chake sawasawa, Arsenal wangekuwa wanahaha kumbakiza Rosicky asiende Real Madrid au PSG.
Viggo Mortensen, mwigizaji maarufu wa Marekani mwenye asili ya Denmark, aliwahi kusema: “Haijalishi ni kiasi gani cha kipaji umepewa, unahitaji kuwa na bahati”.
Kila ninapomtazama Rosicky nakumbuka kauli hii. Hivi Zinedine Zidane na Ronaldinho wangekuwa wamekumbwa na majeruhi kila wiki, nani angejua ubora wao? Nani amewahi kumsikia Mjerumani Sebastian Desler? Wachache wamewahi kumsikia. Wengi wangemjua zaidi Desler kama angekutana na mdudu anayeitwa bahati.
Hata Little Mozart angeweza kujulikana zaidi kama angekutana na mdudu huyu. Wakati huu mashabiki wa Arsenal wanapopagwa na kipaji cha Little Mozart huwa nawashangaa sana.
Wengi hawakujua kwa nini Wajerumani wa Dortmund walimuita Little Mozart. Umechelewa kumsikia Little Mozart.
No comments:
Post a Comment