BAADA ya timu ya soka ya Taifa ya vijana ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ya Tanzania, Tanzanite kuitoa Msumbiji sasa inacheza na Afrika Kusini kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia.
Tanzanite itapambana na Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, keshokutwa Jumamosi katika mechi ya awali kabla ya kurudiana ugenini wiki mbili zijazo.
Mechi hii ni muhimu sana kwa vijana wa Tanzania kwani ndiyo itakayoweka msingi wa kupata nafasi ya kwenda Canada mwakani katika fainali za michuano hiyo zitakazofanyika nchini humo.
Iwapo Tanzanite itapata ushindi mzuri katika mechi hiyo ya nyumbani itakuwa rahisi kwao kwenda kuulinda ushindi huo katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Afrika Kusini.
Kwa hiyo, mechi ya Jumamosi ni ya muhimu kwa vijana wa Tanzania kwani wanapaswa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani na kutoka na ushindi mkubwa kwa timu hiyo ngumu ya Afrika Kusini.
Bila shaka yoyote kazi hiyo haitakuwa rahisi kama ilivyokuwa kwa Msumbiji waliyoichapa 10-0 kwenye uwanja huo kwani Afrika Kusini si timu ya kubeza hata kidogo.
Lakini, pamoja na hilo sitazamii kuwa Tanzanite watabweteka na kuiruhusu Afrika Kusini kutamba nchini bali watajikaza na kujitoa mhanga ili kuhakikisha kwamba wanapata ushindi tena mkubwa.
Ni wajibu kwa wachezaji wa Tanzanite kujituma na kuweka sifa ya Taifa lao mbele kwa kuhakikisha kwamba wanapata ushindi ambao utakuwa chachu katika mechi ya marudiano itakayochezwa Afrika Kusini.
Wachezaji, kocha na viongozi wa timu hiyo wana wajibu wao kwa Watanzania wa kuhakikisha kwamba wanafanya vizuri katika mechi hiyo na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania.
Lakini, Watanzania kwa upande wao nao wana wajibu wao wa kutimiza kwa timu hiyo kwa kuisaidia kwa hali na mali ili iweze kushiriki vyema katika mashindano hayo.
Watanzania wanatakiwa kuipa misaada timu hiyo ili iweze kufanya maandalizi mazuri kwani mzigo huo ukiachiwa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) unaweza kuwa mkubwa na mgumu.
Ieleweke kwamba timu hii ya Tanzanite haina mdhamini kwa hiyo ni wajibu kwa kila mdau wa mpira wa miguu mwenye uwezo kuisaidia ili iweze kutimiza malengo yake kwa ufanisi.
Tanzanite inahitaji kila aina ya msaada ili iweze kumudu gharama za kuiweka kambini na usafiri wa kwenda Afrika Kusini kwa mechi ya marudiano wiki mbili zijazo.
Lakini, msaada mkubwa zaidi ambao Tanzanite inauhitaji ambao upo kwenye uwezo wa kila mmoja wetu hasa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo ya jirani ni kwenda Uwanja wa Taifa kuwapa nguvu.
Watanzania wanatakiwa kufurika kwa wingi Uwanja wa Taifa, Jumamosi ili kuwapa nguvu vijana hao wa Tanzanite kwa kuwashangilia kwa nguvu kubwa jambo ambalo litawaongezea ari ya kuwashinda wapinzani wao.
Ni dhahiri kwamba iwapo vijana wa Tanzanite watashangiliwa kwa nguvu kubwa na mashabiki watakaofurika uwanjani watawazidi nguvu Afrika Kusini na kutoka uwanjani na ushindi.
Jambo jema ni kwamba TFF imeona umuhimu wa Watanzania kwenda uwanjani kwa kuweka viingilio vidogo katika mechi hiyo hali ambayo inampa nafasi kila Mtanzania kumudu kwenda uwanjani.
Kiingilio cha chini katika mchezo huo ni Sh. 1,000 ambayo kila Mtanzania ana uwezo wa kuipata kwa hiyo ni matarajio yangu kwamba Uwanja wa Taifa utajaa mashabiki siku ya Jumamosi.
Ni muhimu kwenda uwanjani lakini la muhimu zaidi ni kuishangilia kwa nguvu timu hiyo ya Taifa ya vijana tangu dakika ya kwanza ya mchezo hadi dakika 90 zitakapomalizika.
Umoja na mshikamano wetu ni nguvu kubwa itakayowafanya Tanzanite watoke uwanjani na ushindi mnono na kujiwekea akiba nzuri kabla ya mechi ya marudiano. Mungu ibariki Tanzanite, Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment