AFANDE Sele, mwanamuziki maarufu wa kizazi kipya nchini, aliwahi kuimba katika wimbo wake fulani hivi akisema; ‘Aliwazalo mjinga ndilo litakalomtokea.’
Leo, miaka kadhaa baada ya mstari ule, Yanga kimewatokea walichokuwa wanawaza kwa muda mrefu, lakini wakaonekana wajinga.
Tangu Emmanuel Okwi apate makali katika miguu yake miaka minne iliyopita Mtaa wa Msimbazi, jijini Dar es Salaam, Yanga walikuwa wanawaza kumpata, na kweli wamempata.
Maswali mengi kuliko majibu
Kabla Okwi hajavaa jezi za njano na kijani, kuna maswali mengi yanayopaswa kujibiwa ingawa majibu yake hayaonekani hewani. Tatizo si Yanga imempataje Okwi. Tunajua kuwa fitina maridadi za usajili kwa sasa zimehamia Yanga baada ya kufifia kwa kundi la Friends of Simba la klabu ya Simba ambao ndio walikuwa hodari zaidi kwa fitina hizi kabla ya kuibuka kwa watu wanaoitwa akina Bin Kleb, Seif Magari, Mussa Katabaro na wengineo pale Jangwani.
Lakini maswali yanakuja. Ni kweli Simba haijalipwa pesa za Okwi? Kama wamelipwa, nani alipokea? Kwa nini SC Villa wameruhusiwa kumuuza mchezaji ambaye alitajwa kuwa yupo kwa mkopo tu klabuni kwao kwa ruhusa maalumu kutoka Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa)?
Nani hasa alikuwa anammiliki Okwi kati ya SC Villa ya Uganda na Etoile du Sahel ya Tunisia? Lakini pia kwa sasa kuna mfumo wa Transfer Matching System (TMS) ambapo jina la mchezaji mwenye matatizo lisingeweza kukubali kuingia katika orodha ya wachezaji wa Yanga. Mbona Yanga wamefanikiwa kuliingiza jina la Okwi? Kwa nini wamepata ITC kama kweli Okwi alikuwa ana matatizo?
Kitanzi katika shingo ya Simba
Alfajiri ambayo kiungo Patrick Mafisango alifariki, ilidaiwa kwamba dakika chache kabla hajakutana na ajali alikuwa anakwepa kusaini mkataba mpya na klabu ya Simba huku viongozi wao wakidaiwa kutembea na dola kadhaa za kumpa Mcongo huyo.
Hata hivyo, inadaiwa kuwa Mafisango alikuwa na mpango wa kwenda kucheza nje ya nchi, au kusaini Yanga. Kama kweli angesaini Yanga, leo Yanga ingekuwa na wachezaji wanne muhimu zaidi katika kikosi cha Simba kilichotamba miaka mitatu iliyopita wakiunda ‘uti wa mgongo’ wa timu.
Ili timu iwe imara inahitaji kuwa na wachezaji wanne ambao ukiwapanga uwanjani unapata ‘uti wa mgongo’, yaani kipa, beki wa kati, kiungo na mshambuliaji.
Kikosi hicho kiliundwa kwa msingi wa kipa, Juma Kaseja, katika ulinzi, nguzo alikuwa Kelvin Yondani, katika kiungo msingi alikuwa Mafisango, katika ushambuliaji nguzo alikuwa Okwi
Ina maana kasoro Mafisango, nguzo yote imekwenda Yanga. Hakuna ubishi kwamba Yanga wanaibuka na kikosi imara zaidi kwa sasa hapa nchini kama utawajumuisha Kaseja, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Okwi, Yondani, Mbuyu Twitte, Didier Kavumbagu, Frank Domayo na Hassan Dilunga. Nani hataki kuwa na wachezaji hawa?
Kwa nini Simba wameondokana na nguzo hizi kuimarisha nyumba ya wapinzani wao? Ukweli ni kwamba wakati wenzao Yanga wakijadili soka la uwanjani, Simba wanaendeshwa na mwanasiasa na wamekubali kwenda kisiasasiasa zaidi.
Timu ambayo Simba walikuwepo nayo miaka mitatu iliyopita, wakitamba katika mechi za kimataifa dhidi ya Kiyovu ya Rwanda na Setif ya Algeria huku wakitolewa kwa shida na Shandy ya Sudan robo ya wachezaji leo wapo Yanga.
Kama nilivyosema, ujanja ujanja ambao ulikuwepo Simba katika kundi la Friends of Simba kama vile kumpora Victor Costa katika mikono ya Yanga na kumvalisha jezi iliyoandikwa Jamal Malinzi, yote haya yamehamia Yanga.
Wajanja wote wa Simba wamesusa na wamemuachia timu Mbunge kwa sababu wanaamini amekuwa na mdomo mwingi kuliko vitendo. Wanataka maneno yake yafike mwisho na aadhirike mbele ya wanachama. Nina uhakika wa asilimia 100 wengi kati yao wamefurahi uhamisho wa Okwi kwenda Yanga kwa sababu wanajua huu ni wakati ambapo Mbunge atawekwa pabaya na wanachama.
Yanga itabakia chui wa karatasi?
Nimesema hapo juu. Yanga inaonekana kutimia katika maandishi. Wana Kaseja, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima, Okwi, Yondani, Mbuyu Twitte, Hamis Kiiza ‘Diego’, Didier Kavumbagu, Frank Domayo na Hassan Dilunga. Nani hataki kuwa na wachezaji hawa?
Bado siku 13 kengele za mwaka mpya zigonge. Na zikigonga Yanga watakuwa wamekaribia kushiriki michuano ya kimataifa. Wanaamini wana kikosi kabambe. Mioyoni wanaweza kuwa wanasema ‘Huku Okwi, huku Ngassa, katikati Kiiza na Kavumbagu’. Lakini watafanya kweli?
Kama wachezaji walionao sasa wakicheza asilimia 80 ya uwezo wao, Yanga inaweza kushindana katika anga za juu na kuwafurahisha mashabiki wao. Tatizo kubwa ni kwamba mastaa hawa wanaweza kuwepo na bado Yanga wakabakia kuwa chui wa karatasi tu. Chui asiyeuma.
Mpira wetu bado hauna nidhamu. Utasikia Okwi kaenda kwao miezi miwili, Niyonzima kaenda kwao wiki sita, na mastaa waliopo wanashindana kuingia klabu za usiku kuliko kwenda mazoezini asubuhi.
Haijalishi ni kiasi gani cha mastaa unao klabuni, kama hawajitumi kama wachezaji wa Mbeya City wanavyofanya, basi hakuna unachoweza kufanya katika soka. Unaishia kuogopwa kwa majina ya gazetini tu.
Matokeo yake, licha ya usajili huu sioni kama Yanga wanaweza kukomesha ubabe wa Waarabu na TP Mazembe. Labda kama wakiamua kufa uwanjani na kufanya mazoezi ambayo wachezaji watakojoa damu.
Maisha yanataka nini Okwi?
Desemba kama hii mwaka jana, Okwi alipokea kiasi cha zaidi ya dola 40,000 (Sh 64 milioni) katika Hoteli ya Sheratoni jijini Kampala kutoka kwa matajiri wa Simba ili asaini mkataba wa miaka miwili wakihofia kuwa Yanga na Azam zingemchukua.
Siku chache baadaye Simba hao hao walimuuza kwenda Tunisia ambapo alipewa dola 45,000 za utangulizi na kisha akaambiwa adai nyingine. Hicho ndio kilikuwa chanzo cha ugomvi wa klabu hiyo na Okwi mpaka staa huyo akaamua kurudi nyumbani Uganda kwani alilalamika kuwa alikuwa hajalipwa mshahara wa miezi mitatu.
Lakini kweli pesa zinamfuata Okwi. Juzi ametia tena kibindoni zaidi ya dola 60,000 kusaini Yanga kwa miezi 30 ijayo. Hii inamaanisha amevuna Sh200 milioni za Kitanzania kwa kipindi cha miezi 12 tu. Unataka nini zaidi? Nani anamlaumu?
Kilicho wazi ni kwamba anavunja mizizi yote ya urafiki na watu wa Simba ambao walimlea nchini tangu mtu anayeitwa Geofrey Nyange Kaburu amlete nchini akiwa na umri wa miaka 16.
Watu wachache ndani ya klabu wanaweza wakafurahi kwa sababu uhamisho wa Okwi unamaanisha kuwa sasa wanachama watakuwa wamemchoka mwanasiasa na wao watapata nafasi ya kuheshimiwa tena klabuni. Hata Kaburu mwenyewe anaweza kuwa katika kundi hili.
Lakini kwa vyovyote vile hii ni sinema, ndio imeanza ngoja tusubiri itakavyokwisha
No comments:
Post a Comment