Friday, 22 November 2013

Wafaransa wamweka Shomari Kapombe kwenye mashine




KIRAKA Mtanzania, Shomari Kapombe, alilazimika kukaa kwenye mashine maalumu nchini Ufaransa kwa muda wa nusu mwezi ili apone jeraha alilofanyiwa upasuaji.
Alilazimika kufanyiwa hivyo baada ya kugundulika ana tatizo la mzunguko mdogo wa damu kwenye miguu tofauti na sehemu nyingine za mwili.
Kapombe alifanyiwa upasuaji huo mwezi wa Agosti huko Ufaransa kutokana na jeraha kwenye kidole cha mguu wa kulia baada ya kuumia kwenye mazoezi ya klabu yake ya AS Cannes.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapombe alisema: “Nilikaa kwa kipindi kirefu nje kwa sababu baada ya upasuaji, niligundulika nina tatizo la kuwa na mzunguko mdogo wa damu kwenye miguu.
“Kutokana na tatizo hilo, ndiyo ilikuwa inafanya kidonda changu kuchelewa kupona na ikabidi itumike mashine maalumu inisaidie kupona haraka.
“Katika mashine hiyo, nilikuwa nakaa humo kila siku, nilifanya hivyo kama nusu mwezi hivi ndiyo nikaacha. Mashine hiyo ndiyo ilinisaidia kidonda kile kupona upesi na kurudi tena uwanjani kwa mara nyingine.”
Baada ya kupona, anasema ameshaichezea klabu yake mechi nne na alikuja Tanzania kwa ajili ya mechi ya kirafiki ya Taifa Stars dhidi ya Zimbabwe iliyofanyika juzi Jumanne.
Kapombe anatarajia kuondoka leo Alhamisi kurudi Ufaransa kujiunga na klabu yake iliyomchukua kwa lengo la kumtengeneza akitokea Simba ya Tanzania ili baadaye auzwe.

No comments:

Post a Comment