Friday, 22 November 2013

Mcroatia wa Simba ana rekodi safi Afrika



KOCHA kutoka Croatia, Zdravko Logarusic ametajwa kuwa ndiye atakayeketi kwenye benchi la klabu ya Simba wakati itakaporejea kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara hapo mwakani.
Hiyo ni baada ya Simba kuwaonyesha milango ya kutoka makocha wake wa sasa Abdallah ‘King’ Kibadeni na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’.
Logarusic atarithi klabu hiyo ikiwa kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kukusanya pointi 24 katika mechi 13, huku sare za mfululizo na kichapo kutoka Azam FC kwenye mechi zake nne za mwisho za kuhitimisha duru la kwanza ni moja ya sababu iliyowatoa Kibadeni na msaidizi wake Julio.
Lakini, sasa Simba imepanga kuwa na maisha mapya kuanzisha mwaka mpya na wanaamini kocha huyo  atawafikisha kwenye hatua nzuri mwisho wa msimu kama alivyofanya kwenye klabu nyingine za Afrika alizowahi kuzinoa ikiwamo Gor Mahia ya Kenya.
Logarusic ni nani?
Ni kocha mwenye uzoefu mkubwa wa mchezo wa soka, kwani alicheza kwa mafanikio makubwa kabla ya kuanza kuwa kocha wa mchezo huo. Ni kocha mwenye stashahada tatu tofauti za ukocha na leseni ya Croatia, Australia na ya Uefa PRO.
Kwa umahiri wake, kocha huyo anayetazamiwa kung’ara kwenye benchi la Simba alifanya kazi kwenye mabara manne tofauti, Ulaya, Amerika, Australia na Afrika huku akiwa na uzoefu wa miaka 20 kwenye mchezo wa soka. 
Tangu aanze kujihusisha na ukocha, Logarusic amekaa kwenye benchi na kuziongoza timu zake kwa zaidi ya mechi 1000. Nje ya soka Logarusic ni baba wa familia ya watoto wawili, Lora na Rafael. Mkewe anaitwa Senada.
Atua Gor Mahia, afanya mambo
Logarusic alitua Gor Mahia inayoshiriki Ligi Kuu Kenya msimu wa 2011-2012. Wakati alipotua kwenye timu hiyo aliikuta ikiwa nafasi ya 14 kwenye ligi baada ya wiki saba.
Baada ya kutua hapo alibadili mambo kwa muda mfupi na kuisaidia timu hiyo kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na kufanikiwa kutwaa Kombe la Kenya na hivyo kuifanya Gor Mahia kufuzu kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (Caf).
Alishinda taji la Top 8 na kuchaguliwa na kushinda tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka nchini Kenya baada ya mafanikio yake hayo kwenye klabu hiyo huku akiongoza timu hiyo kuweka rekodi ya kucheza mechi 22 bila ya kupoteza.

Kilichomwondoa kwenye timu hiyo ni uongozi ulioamua kumfuta kazi baada ya kuchoka kuendelea kumsubiri alipochukua muda mrefu nchini kwao Croatia wakati wa likizo.
Jambo hilo liliwafanya viongozi wa Gor Mahia kumchagua aliyekuwa msaidizi wake, John ‘Bobby’ Ogolla kuchukua mikoba yake kwa muda kabla ya kumnasa Bobby Williamson ambaye hapo kabla alikuwa akiinoa timu ya Taifa ya Uganda.
Yapo madai kwamba mafanikio ya Williamson hadi kutwa ataji la Ligi Kuu Kenya msimu huu yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kazi nzuri iliyofanywa na Logarusic hapo kabla.
Atesa Afrika
Tangu msimu wa 2009-2010, Logarusic anatesa kwenye ardhi ya bara la Afrika baada ya kuibukia nchini Ghana katika klabu ya FC King Faisal.
Alianza kazi kwenye timu hiyo ikiwa nafasi ya 16 baada ya kucheza kwa wiki 13, lakini kwa muda mfupi aliokuwa na timu hiyo aliisaidia kushika nafasi ya saba kwenye ligi mwishoni mwa msimu.
Kutokana na hilo, Logarusic alichaguliwa kwenye orodha ya makocha watatu bora nchini Ghana.
Msimu uliofuata, kocha huyo alijiunga na FC Ashgold ya Ghana, ambao aliwakuta wakiwa nafasi ya tisa, lakini hadi mwisho wa msimu wa ligi aliwapandisha na kumaliza wakiwa nafasi ya pili.
Kwa mara nyingine alichaguliwa kwenye orodha ya makocha watatu bora wa Ghana na timu yake ilifuzu kucheza Kombe la Shirikisho Afrika.
Aomba kazi kwa mtandao
Baada kuondoka Gor Mahia, Logarusic aliamua kuandika barua ya maombi ya kazi na kisha kuiweka kwenye tovuti yake binafsi, akielezea ujuzi wake na uzoefu wa kazi ya ukocha.
Akielezea kuwa na uzoefu wa miaka 20 kwenye soka, kocha huyo alisema ana uzoefu mkubwa wa mawasiliano na wachezaji na vyombo vya habari na kwamba anafahamu vyema lugha ya Kingereza na haitakuwa ngumu kwake kuwasiliana na wachezaji wake na benchi la ufundi kwa ujumla
Logarusic akiwa mchezaji aling’ara katika klabu kadha za nchi za Croatia, Sweden, Ujerumani na Australia kabla ya kuwa kocha

No comments:

Post a Comment