Wednesday, 27 November 2013

Tunarudi kutazama movie za Schwarzenegger

SchwarzeneggerJan2010.jpg


SIJUI kwa nini mpaka leo Mwenyekiti wa Simba hana jina la utani la kipiganaji? Nadhani muda si mrefu atapewa jina hili la utani. Kama alinusurika katika siku za nyuma kupewa jina hili, basi huu ni wakati mwafaka kwake.
Soka letu linarudi katika vurugu zetu za zamani. Ni vurugu hizi hizi ambazo zilitupatia viongozi wenye majina mengi ya mapambano kuliko ya soka. Walikuja watu wanaoitwa Tyson, Mpiganaji, Yeltsin, Komandoo na wengineo.
Tayari Mwenyekiti wa Simba amemwambia bosi wa TFF bwana Jamal Malinzi kuwa haifahamu katiba. Na kwa sababu bwana Malinzi alikuwa kiongozi wa mpira wa zamani, hapana shaka na yeye atajibu mapigo.
Muda si mrefu tutaangalia filamu hii kwa mvuto zaidi na mwishowe, kwa sababu wote ni viongozi wa zamani katika soka letu watajipatia majina ya kipiganaji ambayo Rais aliyepita, Leodeger Tenga hakuwahi kuyapata.
Ukitazama Kamati za bwana Malinzi, zimejaza viongozi wa Simba na Yanga ambao ni wataalamu wa fitina na majina yaliyozoeleka katika soka. Sijui alikuwa anafikiria nini? Lakini wengi wanaonekana wako tayari kwa mapambano ya fitina pengine kuliko kuendeleza soka letu.
Wachache sana kati yao wana upeo na dhamira, lakini wengine akili yao itakuwa kuangalia kama masilahi ya Simba au Yanga yamelindwa. Ni hawa hawa ndio wamekaa kimapambano zaidi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Simba naye anajipanga. Amemwingiza katika kundi lake mpambanaji wa muda mrefu, Michael Wambura ambaye mfumo wa watawala waliomaliza muda wao ulimuweka kando.
Huyu hajaingia katika kumsaidia Mwenyekiti wa Simba kwa maadui wa nje ya Simba tu, bali pia wale wa ndani ambao waliwahi kumfukuza Wambura pale alipowaambia watu wa Friends of Simba kuwa kundi lao ni kama Kamati ya Harusi. Ni kitu kilekile ambacho mwenyekiti amekisema majuzi kwa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliojaribu kumwondoa.
Na sasa tunaachana na soka la uwanjani taratibu. Tulianza kuzoea zaidi soka la uwanjani, lakini muda si mrefu tutarudi katika zama zetu za kucheza soka la nje ya uwanja. Hivi Kilimanjaro Stars ikiambulia patupu michuano ya Cecafa pale Nairobi?
Hakuna anayesisimka kwamba tumepeleka vijana wadogo Nairobi na tunaweza kushinda kitu. Watu wanasisimka kutaka kujua Malinzi atamjibu nini Mwenyekiti wa Simba baada ya kukataa kufuata amri yake ya kuitisha mkutano ndani ya siku 14.
Habari ya kocha mpya wa Simba si habari tena. Hakuna anayetaka kujua uwezo wake. Klabu imegawanyika katika pande mbili. Kuna watu wanamtaka Mwenyekiti wengine hawamtaki. Habari ya kocha pembeni kwa sasa.
Tunakokwenda hakuna tofauti sana na mtu anayerudi kutazama ile filamu maarufu ya Commando ambayo ilimpatia umaarufu Arnold Schwarzenegger enzi zake. Tunarudi katika zama za viongozi wapiganaji ambao hata ‘First eleven’ za timu zao hawazifahamu.
Bahati nzuri katika zama hizi watu hawataki usumbufu. Wanaotaka kuangalia filamu za Schwarzenegger wataangalia, lakini wengine kama kawaida yao watakuwa wakiwaangalia akina Lionel Messi, Cristiano Ronaldo, Mesut Ozil, Coutinho, Wayne Rooney na wengineo katika dunia halisi ya soka.
Unang’ang’ania nini kuongoza timu ambayo haina uwanja wa mazoezi tangu kuanzishwa kwake mwaka 1936? Yetu macho!

No comments:

Post a Comment