KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, ameshinda Tuzo ya Mwanasoka Bora 2012/13.
Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania 2012/13 iliandaliwa na gazeti bora la michezo Afrika Mashariki, Mwanaspoti kwa udhamini wa Vodacom na Clouds Media Group.
Niyonzima alishinda tuzo hiyo katika hafla maalumu iliyofanyika jana Ijumaa usiku katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na mgeni rasmi Naibu Waziri wa Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia, Januari Makamba.
Niyonzima aliwashinda wachezaji wengine wanne waliokuwa wameingia katika fainali ambao ni Shomari Kapombe (Simba), Amri Kiemba (Simba), Kelvin Yondani (Yanga) na Themi Felix wa Kagera Sugar.
Katika mchujo wa mwisho walioingia tatu bora walikuwa Niyonzima, Kapombe na Kiemba. Licha ya kupewa Sh5 milioni, pia Niyonzima alikabidhiwa tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi ilikwenda kwa Joseph Kimwaga wa Azam aliyewashinda Juma Luzio wa Mtibwa Sugar na Ramadhani Singano wa Simba. Kimwaga alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike ilikwenda kwa Mwanahamisi Omari ambaye aliwapiku Fatuma Mustafa na Shelda Boniface.
Mwanahamisi alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Niyonzima alipata tuzo nyingine ya Mchezaji Bora wa Kigeni na kuwashinda Kipre Tchetche wa Azam na Hamis Kiiza wa Yanga. Ushindi huu ulimpa Niyonzima tuzo maalumu.
Mbwana Samatta wa TP Mazembe ya Congo alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora Anayecheza Nje na kuwapiku Thomas Ulimwengu (TP Mazembe) na Henry Joseph aliyekuwa anachezea Kongsvinger ya Norway. Samatta pia alipewa tuzo maalumu.
Katika kipengele cha Kocha Bora, Abdalla Kibadeni alishinda kipengele hicho kwa tiketi ya Kagera Sugar na kuwapiku Ernest Brandts wa Yanga na Stewart Hall wa Azam. Kibadeni ambaye sasa anafundisha Simba alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu.
Mwamuzi mwenye beji ya Fifa, Oden Mbaga wa Dar es Salaam alichaguliwa kuwa Mwamuzi Bora na kuwapiku Martin Saanya na Ibrahim Kidiwa. Mbaga alipewa Sh500,000 na tuzo maalumu
Tuzo ya Mfungaji Bora ilikwenda kwa Kipre Tchetche wa Azam, ambaye alifunga mabao 17 msimu uliopita. Alipewa tuzo maalumu.
Tuzo ya Bao Bora la Msimu ilikwenda kwa Thomas Ulimwengu wa TP Mazembe ambaye alifunga bao hilo wakati Taifa Stars ilipocheza na Ivory Coast katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Alipata Sh500,000 na tuzo maalumu.
Tuzo ya Kipaji Maalum ilikwenda kwa Hadhara Charles Mnjeja ambaye ni msichana mwenye uwezo wa kucheza na kumiliki mpira. Alipewa Sh200,000 na tuzo maalumu.
Kikosi Bora cha Msimu ni: Juma Kaseja (Simba), Mbuyu Twite (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), David Mwantika (Azam), Amri Kiemba (Simba), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe), Haruna Niyonzima (Yanga), Themi Felix (Kagera Sugar), Mbwana Samata (TP Mazembe) na Kipre Tchetche). Kila mchezaji alipewa tuzo maalumu.
Tuzo ya Mtangazaji Mahiri ilikwenda kwa mtangazaji wa zamani wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Mshindo Mkeyenge. Mkeyenge alikuwa mtangazaji kuanzia mwaka 1963 mpaka 1975. Alipewa Shilingi milioni moja na tuzo maalumu.
Tuzo ya Uongozi wa Soka Uliotukuka ilikwenda kwa Leodegar Tenga ambaye ameongoza Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa miaka minane kwa mafanikio makubwa. Alipewa tuzo maalumu.
Tuzo ya Wakongwe ilichukuliwa na wachezaji wa zamani watano ambao kila mmoja alipewa Sh. milioni moja na tuzo maalumu. Hao ni Nicholous Akwitende, Mbwana Abushiri, Omari Zimbwe, John Lyimo na Jella Mtagwa.
Akwitende
Alichezea timu ya taifa ya Tanganyika mwaka 1952 mpaka 1964 na baadaye timu ya taifa ya Tanzania 1964 mpaka 1972.
Alichukua Kombe la Gossage miaka mitatu mfululizo.
Gavana Mwingereza aliwahi kumkodishia ndege kutoka shuleni akasaidie timu ya taifa ya Tanganyika.
Lyimo
Alichezea timu ya taifa mwaka 1960 mpaka 1969 alipolazimishwa na mwajiri wake kuacha soka. Alikuwa nahodha wa timu ya taifa Tanzania mwaka 1963 mpaka 1969.
Abushiri
Alichezea timu ya taifa mwaka 1959 mpaka 1968 na alikuwa nahodha kuanzia mwaka 1964 mpaka 1967 kabla ya kuwa Mchezaji Bora wa Afrika Mashariki mwaka 1967.
Zimbwe
Alichezea timu ya taifa mwaka 1963 mpaka 1974 na alikuwa nahodha mwaka 1969 mpaka 1974.
Mtagwa
Aliichezea timu ya taifa kuanzia mwaka 1973 mpaka 1983 na alikuwa akipokezana unahodha wa timu ya taifa na Leodegar Tenga kuanzia mwaka 1974 mpaka 1983.
Alikuwamo katika kikosi cha taifa kilichokwenda katika fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 na picha yake ilitumika katika stempu.
Washindi walipatikana kupitia utaratibu maalumu wa kupiga kura kupitia ujumbe mfupi wa maandishi chini ya Kamati huru ya Tuzo ya Mwanaspoti Bora wa Soka Tanzania iliyokuwa chini ya uenyekiti wa mwanasoka mashuhuri wa zamani nchini Zamoyoni Mogella na katibu wake, Amir Mhando ambaye ni Katibu wa Taswa.
Wajumbe wa kamati hiyo walikuwa kocha Kennedy Mwaisabula, mchambuzi wa soka Shafii Dauda, Katibu Mkuu wa chama cha makocha nchini, Michael Bundara, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura, mtangazaji wa michezo Thomas Chilala, mtangazaji wa michezo, Maulid Kitenge na mwandishi wa michezo, Doris Maliyaga.
No comments:
Post a Comment