Friday, 15 November 2013

NANI KUPELEKA KADI YA SALAMU KWENDA BRAZIL KATI YA RONALDO NA IBRAHIMOVICH

Debate: Ronaldo v Ibrahimovic - Who does the World Cup need more?



Vita vya kupigania nafasi nne za mwisho za bara Ulaya katika Kombe la Dunia 2014 vitaanza Ijumaa huku Ufaransa na Ureno zikipigania kujiunga na miamba wenzao barani kama vile mabingwa watetezi Uhispania na Ujerumani nchini Brazil.

Ureno, wakiongozwa na nyota Cristiano Ronaldo, ndio wenye mechi ngumu zaidi watakapokutana na Sweden, ambao wana nyota wao Zlatan Ibrahimovic atakayekuwa akiwaongoza.
Mabingwa wa zamani Ufaransa wataenda Kiev kucheza dhidi ya Ukraine wakitumai kuwa ikiwa watafuzu, haitakuwa kwa njia tata kama walivyofanya walipofuzu kwa fainali za 2010 ambapo bao la uamuzi dhidi ya Ireland lilifungwa baada ya kuandaliwa na Thierry Henry kwa kutumia mkono.
Mechi hizo nyingine mbili zitahusisha Ugiriki ambao wamekuwa hawafungi mabao mengi na ambao watakutana na Romania. Mechi ya kuhadithiwa huenda ikawa ya Iceland watakaokuwa wenyeji wa Croatia ambao walifika nusufainali 1998. Iceland wanataka kuwa taifa ndogo zaidi kuwahi kufuzu kwa fainali hizo.
Kocha wa Ureno Paulo Bento, aliyeongoza timu hiyo kufika nusufainali za Euro mwaka uliopita, anafahamu kuwa matarajio ni makuu.
“Ninaelewa ni kwa nini kunaweza kuwa na matarajio makuu kwa sababu litakuwa (Kombe la Dunia) Brazil, ingawa lengo letu lingekuwa tu sawa kama fainali zingekuwa kwingine,” mkufunzi huyo wa umri wa miaka 44 aliambia Fifa.com.
"Kiwango cha azma yetu hakingebadilika. Lakini ukweli ni ukweli. Nje ya kambi, kuna matarajio makuu kuhusu kufika kwetu huko, kwa sababu fainali zitachezewa Brazil na kwa sababu wao huzungumza Kireno. “Tulipoweka malengo yetu ya muda mrefu, lengo kuu lilikuwa kufika Brazil, na bado tunaweza kulifikia.
“Dhidi ya Sweden, tutakuwa tukikabiliana na mechi hiyo inavyostahiki: kwa kujiamini, kuheshimu wapinzani wetu na, zaidi ya yote, kuwa na imani kuu kwamba tunaweza kufika Brazil 2014."
Wengi wa mashabiki wasioegemea upande wowote wanavunjwa moyo kwamba mmoja kati ya Ronaldo na Ibrahimovic atakosa kivumbi cha Brazil, lakini straika huyo wa PSG anasema timu yake inastahili nafasi kwenye kikapu droo ya Kombe la Dunia itakapokuwa ikifanywa Desemba 6 Mata de Sao Joao.
"Tulikuwa na mechi ngumu wakati wa michuano ya kufuzu kwenye makundi lakini hili hata lilitusisimua zaidi,” alisema Ibrahimovic.
"Ureno huenda ndio wanaopigiwa upatu zaidi ukizingatia timu yao na wachezaji wao, lakini sisi tulimaliza wa pili katika kundi lililokuwa na Ujerumani na tunastahili kwenda Brazil zaidi,” alisema nahodha huyo wa Sweden.
Ukraine itakuwa mwenyeji wa timu ya Ufaransa ambayo imo hatarini ya kukosa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 1994 na ambayo bila shaka imepanga kuondoa kumbukumbu mbaya za makala ya 2010 uwanjani na hata nne ya uwanja ambapo wachezaji wa Ufaransa waliishia kususia mazoezi.
Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps – ambaye mwaka 1998 aliibuka nahodha wa kwanza wa Ufaransa kuinua Kombe la Dunia baada yao kulaza Brazil mjini Paris – alisema wachezaji wake wamo katika hali nzuri tayari kushinda Ukraine.
“Mechi huchezwa uwanjani lakini kichwa ndicho huongoza miguu,” alisema kocha huyo wa zamani wa Juventus na Monaco.
“Tuko katika hali ya kiakili ya ‘kukabili’, na ‘kupigana’. Hakuna nafasi ya shaka, kusita au kuuliza maswali,” akaongeza.
Kocha wa Ukraine Mikhail Fomenko ameongoza timu yake katika mkimbio wa kutoshindwa wa mechi sita tangu achukue hatamu Desemba 2012 na anasema timu hiyo ina msukumo wa kutosha kushinda mechi hiyo.
“Ufaransa wana ujuzi na uzoefu na ni wapinzani hatari lakini hatuogopi mechi zijazo,” Fomenko aliambia AFP.
"Ninafikiri wachezaji wote wanaelewa vyema lile ambalo sharti tutimize katika mechi dhidi ya Ufaransa.”
Romania watajaribu kufuzu kwa fainali kwa mara ya kwanza tangu 1998 watakapotembelea Ugiriki ambao walifunga tu mabao 12 katika mechi 10 za makundi, kwenye mechi inayoonekana kuhusisha timu zinazotoshana nguvu.
Kufika kwa Iceland hadi mechi hizi za muondoano za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia kwa kiasi kikubwa kumefanikishwa na utulivu na ujuzi wa kocha mzoefu kutoka Sweden Lars Lagerback, aliyekuwa mkufunzi wa Sweden katika fainali mbili za Kombe la Dunia zilizopita.
Lagerback, ambaye pia aliongoza Sweden katika fainali tatu za ubingwa Ulaya, alisema wako tayari kwa lolote.
“Bila shaka tutavunjwa moyo sana ikiwa hatutafika Brazil ikizingatiwa kwamba tumekaribia sana, lakini ukiniuliza mimi tutakuwa tu tumeshinda,” alisema.
“Hakukuwa na watu wengi nje ya Iceland, na hata Iceland kwenyewe, waliotarajia tufiko hapa, ingawa matarajio ya watu yamekua kadiri tulivyosonga katika kinyang’anyiro hiki cha kufuzu.”

No comments:

Post a Comment