Monday, 4 November 2013

nahodha wa simba aisubiri ashante




NAHODHA wa Simba, Nassor Masoud ‘Chollo’ amesema kikosi chake kipo kamili kuweza kuivaa Ashanti United katika mchezo wa Ligi Kuu ya Bara keshokutwa Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba inaingia katika mchezo huo huku ikiwa inashika nafasi ya nne ikiwa na pointi 21 baada ya mechi 12, wakati Ashanti yenyewe ina pointi 10 ikiwa katika nafasi ya 11 baada ya kucheza mechi 12 pia.
Ashanti ni miongoni mwa timu tatu zilizopanda msimu huu wa Ligi Kuu huku nyingine zikiwa ni Mbeya City na Rhino Rangers ya Tabora, imeonyesha kuzinduka katika ligi hiyo baada ya kuanza kwa kusuasua hapo awali.
Akizungumza na mtandao huu, Chollo amesema anaamini wachezaji wenzake wapo tayari kwa mchezo huo ambao ni muhimu kwao kuweza kujiongezea pointi muhimu ambazo zitaiwezesha timu hiyo kupaa kutoka nafasi ya nne wanayoshika sasa.

“Unajua ligi ni ngumu kweli kweli, kila timu tunayokutana nayo ni ngumu lakini nadhani baada ya kuyumba kwa muda kidogo sasa umefika wakati wa kufanya vizuri kwa kuhakikisha tunafanya vizuri mbele ya Ashanti katika mchezo wa wiki hii na kujiweka katika nafasi nzuri ya kwenye msimamo wa ligi.
“Lengo letu ni kuona Simba inakuwa katika nafasi nzuri kabla ya kwenda kupumzika ligi itakaposimama, lakini hilo litawezekana kama wachezaji tukipambana na kushinda mechi dhidi ya Ashanti,” anasema Chollo.

Chollo alienda mbali kwa kuwataka wachezaji wenzake kuwa wapole muda wote wa mchezo dhidi ya Ashanti na kuachana na tabia za kuanzisha vurugu hata kama watahisi kuna kitu kimeenda ndivyo sivyo.

“Vurugu haziwezi kutusaidia hata kidogo, hata kama tumeonewa bado mashabiki wa Simba wanatakiwa kutushangilia kuanzia mwanzo hadi mwisho ili tu timu ipate hamasa na kushinda,” anasema Chollo

No comments:

Post a Comment