Friday, 15 November 2013

Kwanini Hall amefukuzwa Azam FC?

Stewart Hall

NI ukweli unaoumiza kuwa mwanafunzi wa shule fulani aliyepata alama 34 za somo la Hisabati bado aliongoza darasani. Alipopelekwa shule nyingine, kiongozi wa somo hilo hilo alikuwa na alama 98. Haishangazi kwa nini Azam imeachana na Stewart Hall.
Azam inashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini imegoma kukubali kuwa kwa uwekezaji wao mkubwa wanaoufanya hii ni nafasi halali kwao kuwepo. Hata kama wako pazuri, lakini kuna imani imejengeka Chamazi kuwa wanastahili kuwa mbali zaidi ya walipo sasa.
Hata kama wangekuwa wanaongoza ligi, lakini Azam ingejiuliza inaongoza Ligi kwa pointi ngapi? Dhidi ya timu ambazo zimewekeza kwa kiasi gani? Zinacheza katika viwanja gani? Katika huduma gani?
Kuwa na pointi sawa na Mbeya City hakuitendei haki Azam yenyewe, wala kupitwa pointi moja na Yanga hakuitendei haki Azam. Walipaswa kuwa juu ya hapo kwa vipimo walivyojiwekea wenyewe, lakini chini ya Stewart Hall haikuwa inaelekea huko.
Ashanti ilianza kukoleza safari ya Stewart
Wakati Yanga na Simba zikichota pointi sita na mabao tisa dhidi ya Ashanti, Azam iliambulia pointi moja tu dhidi ya timu hiyo na hii ilikuwa mechi ya kwanza kwa Ashanti kupata pointi yake ya kwanza baada ya kuburuzwa tangu msimu uanze.
Si tu kwamba Ashanti ilichukua pointi moja, lakini pia iliiburuza Azam uwanjani kwa kadiri ilivyojisikia. Azam ilikuwa katika uwanja wake wa nyumbani iliouzoea, nyasi ilizozizoea na timu ambayo gharama yake uwanjani ni zaidi ya Sh300 milioni.
Kutokana na mbio hizo za akina Said Maulid na wenzake, Aggrey Morris aliishia kulamba kadi nyekundu, nusura Ashanti iondoke na ushindi.
Bado zilikuwepo mechi ambazo Azam ilishinda angali wapinzani wakiwa timu bora uwanjani. Mechi ya Yanga, wababe hawa wa Jangwani walikuwa bora kuliko Azam na tofauti pekee ilikuwa bao la dakika za majeruhi la Joseph Kimwaga.
Katika mechi dhidi ya Simba, ni Kipre Tchetche pekee ndiye aliyekuwa tofauti kati ya Simba na Azam kutokana na juhudi zake binafsi na ubora wa bao lake la pili alipopokea mpira mrefu kutoka langoni mwake.
Stewart na wababe wanaojilinda
Nimetazama mechi nyingi za Azam msimu huu. Inatumia viungo wawili wakabaji. Kipre Balou anacheza kama mkabaji. Sure Boy ni kiungo asiyekuwa na madhara eneo la mbele. Kiungo wa mbele ni Humphrey Mieno. Hana kasi wala pasi za mwisho za hatari.
Matokeo yake, kwa muda mwingi Azam inacheza pasi ndefu kwa Kipre, John Bocco au kinda Kimwaga ambaye ameanza kupata nafasi katika siku za karibuni. Swali linakuja, ukiwa na wachezaji kama wa Azam kwa nini usicheze soka la kushambulia (attacking game) bila ya hofu?
Kama Mbeya City na kikosi chao chenye gharama ya Sh10 milioni hakiogopi kushambulia, vipi kwa Azam yenye kikosi kilichowagharimu zaidi ya Sh300 milioni? Tangu lini kikosi chenye gharama hizi kikacheza mashambulizi ya kushitukiza?
Waliotazama mechi dhidi ya Ruvu Shooting wangeshangaa zaidi. Eneo la katikati lilitawaliwa zaidi na kijana Hassan Dilunga. Aliingia katika shimo kubwa linalotengenezwa katikati ya Kipre Balou, Himid Mao na kiungo wa mbele, Mieno.
Azam ikafa katikati na ikafanikiwa kufunga mabao kwa mashambulizi ya kushitukiza. Kitu hiki kinawakera wenye timu. Kwanini timu yao haichezi? Kwa nini inanyatia kushambulia? Mbona Yanga na Simba haziogopi kucheza? Tangu lini timu kubwa ikatawaliwa katika mechi kwa kuogopa kucheza?
Unaweza kukubali fomesheni ya Hall katika mechi dhidi ya TP Mazembe, Al Alhy, Esperance au Orlando Pirates, lakini sio dhidi ya Rhino Rangers au JKT Oljoro.
Aligoma kusajili mastaa wapya
Tunalaumu timu zetu kwa kusajili wachezaji wengi na kuacha wengi. Lakini kwa Hall, hadithi ilikuwa tofauti. Hata hao wachache hakuwataka. Aliamini Azam ingefanya vema zaidi bila ya mchezaji mpya kikosini, kweli aliendelea na wale wale wa msimu uliopita akiahidi angepandisha vijana.
Hata hivyo hakufanya hivyo. Alichezesha wachezaji wale wale wa zamani bila ya kutumbukiza vijana. Usiku wa sare ya Azam, wenye timu walikasirika. Wakamwambia katika mechi ijayo ya Yanga, lazima apange vijana.
Wakamuingizia majina, mojawapo likiwa la Kimwaga ambaye alimuumbua kwa kuifunga Yanga bao la tatu.
Tangu lini timu ikapitisha pazia bila ya kusajili? Barcelona ina kikosi maridhawa cha kwanza, pamoja na chuo cha soka, lakini bado iliwanunua akina Alexis Sanchez na wengineo. Vipi Azam?
Matokeo yake, sasa Azam ina washambuliaji wawili tu walio tayari kupambana kikamilifu, Kipre Tchetche na Bocco ambaye muda mwingi ni majeruhi. Maeneo mengi ya ndani ya uwanja hayana ushindani kwa sababu hayajapata changamoto msimu huu.
Vijana waliopandishwa msimu huu tena kwa shinikizo ni Kimwaga na Farid Maliki, lakini Azam ina timu ya vijana iliyo bora na ambayo ina wachezaji wengi bora pengine kuliko wa kikosi cha kwanza lakini hawatumiki.
Stewart alikuwa chini ya alama
Nilichogundua wanaoimiliki Azam hawajipimi kwa pointi walizonazo sasa. Hawataki kuongoza ligi au kuchukua ubingwa kwa pointi chache. Wanajipima kwa uwekezaji wao wenyewe. Kama ilivyo TP Mazembe.
 Tangu wawekeze zaidi hawataki kuzungumzia ubingwa wa ndani kwa sababu wanahisi ni mali yao halali kutokana na uwekezaji wao.
Ni kama Roberto Mancini na Manchester City. Nafasi ya pili Ligi Kuu England haikutosha kutokana na uwekezaji wao wenyewe. Hili ndio tatizo la mpira wa pesa.
 Timu yenye viwanja viwili vya mazoezi, gym ya kisasa, bwawa la kuogelea, haitaki kujipima kwa ushindi mwembamba na soka la kujihami dhidi ya Rhino Rangers.

No comments:

Post a Comment