Real Madrid kumsajili Bale kwa mapesa yote yale, kwa mfano, haina maana kwamba inatarajia atikise nyavu zaidi ya wengine wala kwamba ndiye mchezaji bora zaidi dunian |
SAYANSI ya soka ni kitu cha kuvutia japokuwa pia ina mkanganyiko wa aina fulani na ni vigumu kupata uwiano wa kete zake.
Kila mara vyombo vya habari vimekuwa vikizungumzia habari za mchezaji fulani kutaka au kutakiwa kwenda klabu hii au ile, hata kama sio msimu wa usajili.
Kumalizika kwa dirisha moja la usajili huwa mwafaka kwa wang’amuzi wa klabu mbalimbali na mawakala kutafuta madili kwa ajili ya wachezaji.
Tofauti na kutekeleza wajibu wao kikazi, wanatafuta pia ‘kula’ yao na pia kujijengea wasifu, maana hatimaye kinachowapandisha chati kama mawakala au wang’amuzi ni aina ya wachezaji waliowanasa au kuwezesha kusajiliwa.
Hili suala la Gareth Bale kusajiliwa Real Madrid kwa Pauni 85 milioni kwa mfano, linatakiwa kutazamwa kwa jicho la tatu.
Wapo wanaojenga hoja kwamba Real Madrid imepoteza fedha hizo au kwamba Rais Florentino Perez anataka tu sifa hapo Santiago Bernabeu.
Nimetazama suala hili kwa upande mwingine na pia nilipata nafasi ya kuzungumza na watu kadhaa wiki iliyopita katika udadisi wa masuala ya soka, thamani ya wachezaji, ununuzi wao na faida kwa klabu.
Mmoja wao ni mtu mwenye uzoefu wa muda mrefu katika masuala ya soka, Jol Kinneear. Ameanzia kucheza, ukocha hadi ukurugenzi wa soka.
Huyu ni raia wa Ireland aliyehamia hapa England tangu akiwa na umri wa miaka sita na sasa amefikisha miaka 66 na anasema maisha yake yote ni soka tu.
Alikuwa beki Tottenham Hotspurs kwa misimu 10 na baada ya hapo amekuwa kocha na sasa ni mkurugenzi wa soka.
Huyu ni mtu anayejiamini kweli kweli na alinieleza kwamba klabu inaposajili mtu mwenye jina kubwa, haitegemei tu kwamba atawafungia mabao, atadaka vizuri au atajenga ukuta imara au kiungo, bali tafakari inakwenda mbali zaidi ya hapo.
Real Madrid kumsajili Bale kwa mapesa yote yale, kwa mfano, haina maana kwamba inatarajia atikise nyavu zaidi ya wengine wala kwamba ndiye mchezaji bora zaidi duniani.
Lakini ukweli ni kwamba kwa muda macho na masikio ya mashabiki wa soka, makocha, mawakala, wang’amuzi, wakurugenzi wa klabu na kampuni za matangazo yalielekezwa kwa kijana huyu aliyezaliwa Wales miaka 24 iliyopita.
Tayari Real Madrid walikuwa na mchezaji ghali kuliko wote – Cristiano Ronaldo, lakini bado waliweka shinikizo wampate Bale licha ya kwamba hawakuwa na mahitaji makubwa sana kwa mtu wa nafasi yake uwanjani.
Lakini nimekuja kung’amua, kama alivyonigusia Kinneear, Real Madrid inajijengea jina na sasa macho yote yaliyokuwa kwa Bale, yanaunganishwa kwa Real Madrid, hapo tayari wamefanya biashara kubwa sana na mauzo yamepanda ajabu.
Kampuni nyingi kubwa zitataka kutangaza kwenye mabango yaliyopo Bernabeu, kwenye mtandao wa klabu hiyo na katika jezi za wachezaji wake, maana kuna miamba miwili ghali zaidi duniani.
Hatimaye, kwa kudunduliza namna hii, klabu inaweza kupata dili kubwa sana za biashara na pia vituo zaidi vya televisheni vitakimbilia kurusha mechi zake.
Utafiti wangu unaonyesha kwamba Real Madrid ni moja ya klabu mbili nchini Hispania zinazokomba pesa nyingi kutokana na matangazo ya televisheni, ambapo tofauti na England, kule Hispania hakuna usawa wa magawio. Klabu nyingine inayodaka kitita kikubwa ni Barcelona.
Kitu kama hicho cha klabu kutolipwa sawa ndicho kinapiganiwa na Liverpool hapa England, ambapo wanataka klabu kubwa zilipwe zaidi, badala ya Manchester United, Arsenal, Chelsea, Liverpool kulipwa fedha za matangazo sawa na Crystal Palace, Norwich, West Bromwich Albion na nyinginezo.
Japokuwa wazo lao halijakubaliwa, nguvu ya soko inaweza kulifanya likubalike siku zijazo. Uamuzi wa wamiliki wa klabu hiyo, John Henry na kampuni ya Fenway Sports Group kutaka malipo kwa kadiri ya thamani ya klabu unaonesha mantiki hii pia.
Uzuri wa wachezaji ni moja ya vigezo vya mashabiki kuzipenda, kwenda kutazama ambapo hulipa viingilio vikubwa tu hapa England.
Labda ndiyo maana Liverpool walikataa kumuuza Luis Suarez pia ili kuhakikisha wanazidi kufanya vyema mchezoni na kupanda chati, na tunashuhudia sasa wakienda vizuri.
Katika kujiongezea thamani pia, Liverpool wana mkakati wa kupanua uwanja wao wa Anfield ili kuipandisha timu ngazi na kuchuana na klabu kama Arsenal na Manchester United zinazoongoza kwa viwanja vikubwa na mapato.
Makusanyo ya Liverpool kwa siku za mechi mwaka 2011 yalikuwa Pauni 42.9 milioni, kidogo mno ikilinganishwa na yale ya Arsenal – Pauni 93.9 milioni au Man United iliyochuma Pauni 100.2 milioni
Tunaona pengo kubwa hapo ambapo linatosha kununua mchezaji nyota wa kimataifa kama Mesut Ozil labda ambaye kwenda kwake Arsenal tayari kumeanza kuleta mabadiliko chanya dimbani lakini pia
kwenye biashara ya mali zao mbalimbali.
Liverpool imekuwa inataka kuupanua uwanja wao lakini imebaki katika nadharia kwa muda mrefu, ambapo pamoja na kuongeza watazamaji na mapato ya tiketi, uwanja utakuwa na hadhi zaidi hivyo kuvutia matangazo ya kampuni mbalimbali.
Inataka kuongeza watazamani kwa asilimia 35 ili kunyanyua mapato yake, watalii nao watapenda kwenda Liverpool kuliona jiji lakini pia kushuhudia uwanja na kupiga picha humo na kwa ujumla vitabu vya akaunti za klabu zitanona.
Kwa hiyo viongozi wa klabu katika ngazi mbalimbali hukuna vichwa kila wakati kuhangaikia usajili, kutengeneza timu nzuri yenye ufanisi dimbani, viwanja bora na kuhakikisha uwiano wa hesabu unazipaisha klabu kiuchumi kwa ujumla ili zipate faida na si kuelekea kufilisika
No comments:
Post a Comment